*Viongozi waendelea kufitiniana kupata urais, ubunge 2015

*Kinana aonya, akemea wabunge wasiokwenda majimboni

*Aikubali hoja ya Dk. Slaa, ataka wawekezaji feki watimuliwe

*Ataka wagombane kuboresha maisha ya watu si kuingia Ikulu

Mgogoro mpya wenye sura ya kuwania madaraka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama uliotokea mwaka 2007 ukaivunja Serikali, sasa unafukuta upya katika hatua tatu tofauti, JAMHURI imebaini.

Hatua ya kwanza ni mgogoro uleule wa mwaka 2007 unaendelea katika ngazi ya urais, hatua ya pili baadhi ya wabunge walioko madarakani wanafurukuta kwa kila hali kuwadhibiti wajumbe wapya wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM wenye nia ya kunyakua ubunge na hatua ya tatu ni baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya kuanza kurejesha mfumo wa chama kushika hatamu bila kujua.


Fukuto hili linafahamika katika ngazi zote za chama, kuanzia Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ambao kwa nyakati tofauti wameamua kuwakemea wanaoendekeza migogoro hiyo.

Mgogoro wa Urais

Taarifa za uhakika zilizolifikia JAMHURI, zinaonesha kuwa makundi yanayousaka urais, hadi sasa hayajaacha kuhasimiana. Pamoja na ukimya uliotawala baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa NEC ipo mikakati mingi ya chini kwa chini inayoendeleza fitina.


Inaelezwa kuwa karibu wagombea tarajiwa wote ndani ya CCM wanamwogopa Edward Lowassa na hivyo wamefikia hatua ya kuunganisha nguvu kupambana naye wazi wazi na kimkakati. Baada ya chama kudhibiti matendo ya Wana-CCM kushambuliana hadharani, kwa sasa wamebadili mkakati.


“Siku hizi hawamtaji tena Lowassa kwa jina, bali wanatumia maneno yanayomlenga kuwaomba wapigakura wasimchague. Utasikia wanasema huyu anayetoa michango makanisani na misikitini aeleze anakozipata fedha. Ni wazi wanamlenga Lowassa lakini kwa kuwa chama kimezuia malumbano, wanashindwa kumtaja moja kwa moja,” kimesema chanzo chetu.


Kimakakati, mgombea mtarajiwa anayeitumia mbinu hii kwa kiasi kikubwa, ni aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta. Yeye kila anapopata fursa ya kuhutubia sehemu mbalimbali, bila kutaja majina ya anaowalenga anasema wasichaguliwe watu wenye fedha nyingi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe yeye anatajwa kuwa na mkakati wa chini kwa chini. Mkakati huu unaoelezwa kuwa unafanya kazi mno usiku, unatajwa kuwa ndio uliomsukuma Kada wa CCM, Hussein Bashe anayefahamika kuwa kwenye kambi ya Lowassa kumshambulia Membe bila kificho kuwa ni mtu hatari.


Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI zinasema Membe amemlalamikia Bashe rasmi kwenye chama na tayari Bashe amepewa barua ya kumtaka kuthibitisha tuhuma alizotoa dhidi ya Membe.


Hadi sasa, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kwa upande wake ameamua kujikita katika kuchapa kazi badala ya maneno ya kushambulia watu wanaodhaniwa kuwa ni wagombea watarajiwa.


Inaelezwa kuwa baada ya afya ya Profesa Mark Mwandosya, ambaye Mwakyembe alikuwa mpiga debe wake mkuu kudhoofika, Dk. Mwakyembe sasa ameamua kuchukua nafasi hiyo.

 

Amebaini kuwa siasa za majukwaani pekee bila kuchapa kazi haziwezi kushawishi wananchi kumfikiria katika nafasi ya urais. Kwa mantiki hiyo anathibitisha uwezo wake kwa kuchapa kazi kama alivyosafisha bandari, shirika la reli na kampuni ya Ndege Tanzania.


Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amekuwa mkimya kwa kiwango cha kuwashitusha walio wengi, lakini naye inaelezwa kuwa ni mkakati wake wa kupima upepo.


Hatua ya Dk. Salim Ahmed Salim kuteuliwa na Rais Kikwete kuingia kwenye NEC na hatimaye kuchaguliwa kwenye Kamati Kuu, imeibua hisia mpya kuwa sasa anaweza kurejea kwenye uringo wa siasa, hasa nafasi ya urais baada ya mwaka 2005 kuishia tatu bora.


Kundi la wana-CCM wengine wanaotajwa kuwa na nia ya kukisaka kiti cha urais, linahusisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (mstaafu), Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri wa Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Rais (mstaafu) wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.


Kinana anasema wananchi wanataka kusikia wanasiasa wanagombania miradi ya elimu, afya, maji, barabara na maendeleo ya jamii kwa ujumla, lakini si mbio za kuingia Ikulu.


“Wanagombania nani anafaa kuwa Rais, ubora au usafi wako unamsaidia nini Mtanzania? Watanzania wanataka kujua kama unachapa kazi ili maisha ya Mtanzania yawe bora. Hawagombanii kwamba bei ya pamba imeshuka, walimu hawalipwi mishahara kwa wakati, tutapunguzaje ukali wa maisha, ada mbalimbali kuziondosha na kero za aina hii, si ubora wa mtu binafsi,” anasema Kinana.


Alipoulizwa juu ya hoja ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa kusema saruji inaweza kuuzwa kwa Sh 5,000, amesema: “Hayo ndiyo tunapaswa kutekeleza. Ukimsikiliza unaona ana hoja, na CCM tunao uwezo wa kuitekeza vizuri hii. Tuangalie wapi tupunguze kodi za kero, tumpunguzie mwananchi ukali wa maisha, na hili tunaliweza.”

Wabunge na Wa-NEC

Kuna baadhi ya wajumbe wa NEC wanaopita kwenye majimbo mbalimbali na kuwafitini wabunge walioko madarakani wakidai kuwa wameshindwa kazi. Hali hii imezaa mgogoro mkubwa kwa kiwango cha baadhi ya wabunge na wajumbe wa NEC kutosalimiana, wakabaki kupishana kama magari kila wanapokutana.


Katibu Mkuu wa CCM Kinana ameliambia JAMHURI kuwa wanaufahamu mgogoro huu: “Wapo wabunge wasiokwenda majimboni. Wakitoka Dodoma wanakuja Dar es Salaam kwenye Kamati, mara wanakwenda kwenye safari zao nyingine, kisha wanakuta muda umekwisha wanarejea tena Dodoma hadi Bunge linamalizika [miaka mitano] hawajaenda jimboni. Hawa, mjumbe wa NEC akizunguka wananuna wanajua atachukua nafasi yao. Lakini wapo [Wa-NEC] wanaotafuta ubunge kweli, hao wanastahili kufanya hivyo ni wa kukemewa,” Kinana ameliambia JAMHURI.


Katika kudhibiti hili, Kinana anasema Rais Jakaya Kikwete amewaonya baadhi ya wajumbe wa NEC kuwa utaratibu walioanza wa kwenda majimboni kuwachafua wabunge waliopo madarakani haukubaliki hivyo akawataka wawasaidie wabunge kumaliza muda wao ndipo waendelee na harakati za kuwania majimbo.

Wenyeviti wa CCM kuvuka mipaka

Mgogoro wa tatu umeibuka kati ya watendaji wa Serikali na wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya. Kinachotokea ni kwamba baadhi ya wenyeviti wamefikia hatua ya kwenda kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri wakadai moja kwa moja utekelezaji wa ahadi za CCM, hali inayowafanya watendaji wa Serikali kuhisi kama nchi imerejea miaka ya 1970, ambapo chama kilitangazwa kushika hatamu.


“Kutembelea miradi wanaweza kutembelea kuona kama mambo yanafanyika au hayafanyiki, lakini hawapaswi kutoa amri. Kwa mfano mimi natembelea miradi, nikiona nazungumza na Waziri Mkuu au baada ya ziara namwandikia taarifa yeye anakwenda kusimamia hayo niliyoyaona kwa watendaji wa Serikali.


“Tukumbuke sasa kuna mfumo wa vyama vingi. Chama kikishashinda kikaunda serikali, utekelezaji wa Ilani unahamia serikalini. Lakini sisi [CCM] tunapaswa kuwa wa kwanza kufahamu ni lipi limepwaya, ni lipi limetekezwa vyema. Maana bila kufanya hivyo mwaka 2015 tutaishia kuvuna mabua,” amesema Kinana.


Kinana anasema chama kina vikao katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya, kata na kijiji ambapo watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali wanaingia kwenye vikao hivyo, na kwamba chama kinapopitisha maazimio, utekelezaji unapaswa kubebwa na watendaji wakaenda kuyatekeleza.


“Lakini njia nyingine unaweza kuzungumza naye mtendaji kirafiki tu, si kwa kumpa amri. Ukamkubusha wewe kama Mwenyekiti wa CCM wa wilaya au mkoa kuwa ahadi zetu ni hizi, tuzitekeleze. Mkizungumza kirafiki inafanya mambo yaende, badala ya kudai ripoti kiimra.


“Tusingependa kuona Katibu wa CCM anamwita Afisa Ardhi na kumtaka taarifa, ila akitumia njia isiyo rasmi vingozi wa kichama kujenga mahusiano ya kiutendaji na watendaji, unazungumza naye mtendaji kwamba jamani eheee, tuliahidi daraja unaweza kwenda kwa mkuu wa mkoa ukamuuliza hili daraja tuliahidi vipi? Atakueleza wamefikia wapi, si kwa kumtaka,” anasema.


Anasema utaratibu wa sasa unataka kila miezi sita, watendaji wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu, wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wa halmashauri, wanatoa taarifa juu ya utekelezaji wa Ilani ya chama.


Kinana ameliambia JAMHURI kuwa viongozi wasione aibu kusema ukweli. Anasema wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda walivyokabidhiwa inabidi, ama wavirejeshe wenyewe serikalini, au sheria itumike kuvirejesha.


“Mimi nawambia ukweli wanasema hawa wanarudisha Azimio la Arusha. Nilikwenda pale Mtwara, kati ya viwanda 12 vya kubagua korosho vilivyobinafsishwa, vinavyofanya kazi ni viwili tu. Wale walipovinunua walisema watavifufua maana yake kama hawafufui tunaibiwa.


Ukibangua korosho, kodi inalipwa, thamani ya korosho inaongezeka, ajira zinazalishwa, mauzo ya nje yanaongezeka, lakini kwa kufunga kiwanda na kukigeuza kuwa ghala, uuzaji nje hauongezeki. Nasema turudishie mali zetu,” amesema Kinana.


Katibu mkuu huyo anasema kama sheria zilizopo haziruhusu, Bunge litunge sheria ya kurejesha serikalini mali zilizobinafsishwa na wahusika wakashindwa kuziendeleza.

Umuhimu wa NEC wilayani

Kinana anasema katika mkutano wa NEC uliopita, chama kimeamua kuwa hakitafuti umaarufu kwa wananchi, bali kinawatumikia wananchi nao wakisharidhika na utendaji wake watakipa ushindi wa kishindo mwaka 2015.


Anasema katika mkutano huo uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, imethibitika umuhimu wa kuchagua wajumbe wa NEC kutokea wilayani, badala ya utaratibu wa zamani ambapo wengi waliishia kuwa Wa-NEC wa kutokea Dar es Salaam.


“Alisimama mjumbe mmoja wa NEC ni headmaster (Mkuu wa Shule) moja huko Shinyanga Vijijini, sote tulivyomsikiliza tukasema kweli anazungumzia wananchi.


“Akasema zile Daladala, akimaanisha baiskeli, zinabeba mtu mmoja mmoja polisi wanawasumbua sana hawa vijana. Akasema mtu anasimamishwa mara nyingi hadi unahofu safari yake atafika saa ngapi?


“Akasema kijana kwa siku anatengenza Sh 6,000 lakini anasumbuliwa hadi inabaki 2000. Yeye akasema kama CCM ina nia ya kuboresha ajira huyu ni wa kumwezesha akaweza kupata 10,000 kwa siku kwa maana ya Sh 300,000 kwa mwezi na hivyo ataiona CCM imemsaidia. Tukaona kuwa kweli hii ni hoja ya msingi na huyu M-NEC anazungumzia wananchi,” amesema Kinana.


Katibu Mkuu huyo, amesema siku zilizopita kulikuwapo mkatiko wa mawasiliano kati ya CCM makao makuu na ngazi ya vijiji na vitongoji, lakini sasa Chama kimefufua uhusiano huu na kwa sasa kinazidi kutanuka kila kukicha na umaarufu wake umerejea kwa kasi.

1225 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!