Michezo haihitaji siasa

Wadau wa mchezo wa riadha nchini wameombwa kuja na mbinu mbadala kama kweli wana nia ya dhati ya kufufua mchezo huo kutoka ngazi ya shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu kuliko kuwaachia wanasiasa wasiokuwa na ufahamu wa michezo.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wanariadha nguli waliowahi kuiletea sifa Tanzania, wanasema miaka ya 1980-1990 Tanzania ilitisha kwenye riadha kuanzia mbio ndefu na fupi.

Wanariadha kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa na John Stephen Akwari ni miongoni mwa wanariadha walioitangaza vyema nchi kupitia mafanikio waliyopata katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Filbert Bayi ni mmoja wa wanariadha wa Tanzania aliyevunja rekodi ya dunia kwa dakika tatu katika mbio za mita 1,500 kwenye michezo ya Madola huko New Zealand na kuwa mwanariadha wa kwanza wa Tanzania kufanya hivyo.

Anasema mwaka 1970, alianza kujulikana kama mwanariadha wa mbio za kati na mwaka 1974 aliweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch, New Zealand na kufuatiwa na zile za maili moja, mwaka mmoja baadaye.

Bayi anasema alikuwa miongoni mwa wanariadha wa timu ya Taifa iliyoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola, Christchurch, New Zealand wakati huo akiwa na miaka 21, na kuvunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500 kinyume na matarajio ya wengi.

“Tukiwa New Zealand, kila mtu alimtaja John Walker pamoja na mwanariadha kutoka Kenya, Ben Jipcho kuwa ndiyo watakaoshindania medali ya dhahabu, wengi walisema kama Walker akiwa wa kwanza, basi nafasi ya pili ni ya Jipcho, Tanzania haikutegemewa kushinda.

“Mita 300 kabla ya kuhitimisha mbio, Walker alianza kusogea, lakini tayari alikuwa kachelewa kwani kwa umbali niliokuwa mbele yake na kasi niliyokuwa nayo asingeweza kunifikia, kila mmoja alibaki akishangaa, Wazungu hawakutegemea, baada ya mbio kila redio ya New Zealand siku hiyo ilizungumzia ushindi wangu na rekodi niliyoivunja,” anasema Bayi.

Anasema wakati huo Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilikuwa karibu sana na michezo kiasi cha kuweka mazingira rafiki kwa vijana wengi  kupenda kushiriki katika michezo mbalimbali.

Anakumbuka sera nzuri za wakati huo na kusema sekta ya michezo iliheshimika ndani na nje ya nchi, hali iliyowafanya Watanzania kutembea kifua mbele kokote.

“Sisi tuliweza kufikia mafanikio yale kwa sababu Wizara ya Michezo kupitia BMT iliweza kujipanga na kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiza siasa ndani yake, hebu angalia leo kila mchezo ni hovyo,” anasema Bayi.

Anasema hakuna nchi inayoweza kupata mafanikio katika mchezo wowote ule bila ya kuwapo kwa mkono wa Serikali ndani yake, na kuongeza kuwa ni lazima pawe na mipango endelevu kwa vijana.

Bayi ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini (TOC), anasema tunapaswa kufanya uwekezaji mkubwa kwa wanamichezo kwa kuweka programu za muda mrefu kwa kuandaa wachezaji kuanzia ngazi ya chini.

Juma Ikangaa ni mwanariadha aliyetamba katika Olimpiki ya mwaka 1984 huko Marekani, ambapo alishika nafasi ya sita akikimbia saa 2:11:10 na ile ya mwaka 1988 huko Soul, Korea Kusini, akikimbia saa 2:13:06 na kushika nafasi ya sita.

Anasema ili kufikia mafanikio ya kweli kwenye mchezo wowote hakuna njia ya mkato, bali uwekezaji unatakiwa kufanyika kuanzia ngazi za chini.

Ikangaa anasema katika kufanikisha hilo, kila mdau atimize wajibu wake kuanzia kwa Serikali na mamlaka zake zote bila ya kuingiza siasa katika masuala ya michezo.

“Kwa kipindi cha miaka mingi sasa ukitazama ndani ya vyama vyetu vinavyoongoza michezo kuanzia soka, riadha, kuogelea na michezo mingine mingi ni migogoro tu kila kukicha huku michezo ikiendelea kudidimia,” anasema Ikangaa.

Anasema riadha ni miongoni mwa michezo inayoweza kuleta faida na utajiri mkubwa kwa mwanariadha, mchezo huu hapa nchini unaheshimika, ndiyo mchezo ulioliletea Taifa heshima kubwa kimataifa.

 “Leo tunawakumbuka na akina Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui, Mwinga Mwanjala, John Stephen Akhwari na wengine wengi ambao walipeperusha vyema bendera ya Taifa kwa sababu michezo ilichezwa kuanzia ngazi ya msingi hadi juu,” anasema Ikangaa.

John Stephen Akhwari, mwanariadha aliyeshiriki michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 1968 kule nchini Mexico upande wa mbio za marathon, anasema nchi imepoteza dira katika michezo kutokana na viongozi waliokabidhiwa madaraka kuongoza riadha kutanguliza ubinafsi.

“Leo kama nchi hatuna mipango thabiti ya kuvumbua vipaji na kuvikuza kama ilivyokuwa zamani; matokeo yake leo kila kitu kimebaki mikononi mwa wanasiasa wasiojua umuhimu wowote wa michezo,” anasema Akhwari.

Anasema, jitihada za makusudi zinahitajika ili kurudi katika mstari waliouacha wanamichezo ambao wameliletea Taifa heshima kubwa, hasa kuanzia miaka ya 1960 mpaka 1980, wakati Tanzania ilipokuwa ikifanya vizuri kuliko Kenya, Uganda na Ethiopia.

Anasema mwaka 1986 kabla ya kwenda kwenye mashindano ya Olimpiki nchini Mexico, alishiriki katika mashindano ya mbio za marathon zilizofanyika nchini Uganda na katika mashindano hayo alifanya vizuri kwa kuwashinda wapinzani wake kutoka Kenya na Ethiopia.

“Wale jamaa niliowashinda katika mashindano hayo kutoka Ethiopia na Kenya ndiyo walioenda kushinda nchini Mexico, hii ni mara baada ya mimi kuanguka chini na kuteguka mguu, kitu ambacho kimeendelea kuniumiza hadi leo katika kumbukumbu zangu,” anasema Akhwari.