Katika makala ya wiki iliyopita nilihitimisha kwa kueleza kwamba Juni 3, 1998 nilipokea amri kutoka Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKURU) iliyonitaka kuwasilisha taarifa ya mali zangu zote pamoja na maelezo ya jinsi nilivyozipata; na kwamba niliweza kufanya hivyo.

Ingawa kichwa cha mada ile ambayo ninaiendeleza leo kinawaaminisha wasomaji kwamba kulikuwa na ugomvi binafsi kati yangu na Edward Hosea, wasomaji wengi watakuwa walibaini kwamba hadi wakati huo mapambano hayo yalikuwa kati ya Edward Hosea kama Mkurugenzi katika Taasisi hiyo na taasisi ambamo mimi nilikuwa mtumishi; na siyo kati yangu binafsi na Edward Gamaya Hosea.

Aidha, wakati huo sikuwa na taarifa yoyote kwamba ndani ya TRA kulikuwa na mfanyakazi mmoja aliyekuwa anatoka kwenye familia ya Edward Hosea aliyeamua au kuamriwa kuacha kazi muda mfupi kabla sijapokea ile ilani ya kujieleza chini ya sheria ya kuzuia rushwa. Hata hivyo, matukio yaliyofuata baada yangu kuwasilisha majibu ya ilani ile yalidhihirisha pasi na shaka kwamba Edward Hosea alinilenga mimi na siyo taasisi ya TRA kwa kuwa alifahamu kwamba mimi ndiye niliyemzuia swahiba wake kunufaika na yale makontena mawili ambayo yalikuwa yawe zawadi yake ya Krismas mwaka 1996.

Baada ya kuwasilisha majibu ya ilani hiyo Juni 1998 ulipita mwaka mzima bila kubughudhiwa na yeyote kutoka kwenye taasisi hiyo. Niliamini kwamba katika kipindi hicho walikuwa wanafanya kazi ya kuhakiki yale niliyokuwa nimeyaeleza katika majibu ya ilani. Ukweli ni kwamba hawakuwa wanafanya hivyo.

Nilithibitisha kwamba hakuna ofisa wa taasisi hiyo aliyewahi kwenda kufanya upelelezi au uhakiki wa mali nilizokuwa nimeainisha kuwa katika maeneo mbalimbali; ikiwa ni pamoja na mifugo kadhaa na mazao ya kilimo niliyoeleza kuwa mikononi mwa baba yangu mzazi huko nilikozaliwa!

Hata taasisi nilizokuwa nimeainisha kwamba zinanilipa marupurupu kama Mkurugenzi wa Bodi hazikuwahi kufuatwa na kutakiwa kutoa uthibitisho wa madai yangu! Hivyo ulikuwa mshituko mkubwa pale Juni 24, 1999 watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa walipofika ofisi za TRA kwa nia ya kunitia mbaroni wakiwa wameambatana na waandishi wa habari na wapiga picha kutoka kwenye vyombo vya habari kadhaa.

Kwa bahati mbaya kwao, siku hiyo sikuwa ofisini kwa vile nilikuwa nimeugua ghafla asubuhi hiyo wakati najiandaa kwenda kazini. Wakubwa hao walikwenda moja kwa moja kwa Kamishna Mkuu na kumtaarifu kwamba walikuwa wamekuja kunikamata. Kutoka hapo walikwenda ofisini kwangu ambako katibu muhtasi wangu aliwaarifu kuwa nilikuwa nimempatia taarifa kuwa ninaumwa, hivyo nisingekuja kazini siku hiyo.

Walimwomba awapatie anwani ya sehemu niliyokuwa ninaishi na namba zangu za simu akawagomea hata walipomtolea vitisho. Waliondoka kwa hasira. Walirudi maeneo ya ofisini mchana kwa madhumuni hayo hayo kwa kuwa waliamini lazima ningekuwapo ofisini kuhudumia kikao cha Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi ambayo mimi nilikuwa Katibu wake. Waliishia kupata aibu pale walipovamia gari moja na kumkabiri  kiongozi mwingine wa idara aliyefika  hapo Makao Makuu ya TRA ndani ya gari lenye rangi sawa na gari nililokuwa natumia!

Kesho yake, baada ya kuwa wamefanya uchunguzi na kufahamu nyumba nilikokuwa naishi, waliamua kunifuata huko. Bahati nzuri, jana yake nilikuwa nimepata taarifa za yote yaliyokuwa yametokea   kwenye ofisi za TRA. Kwa hiyo asubuhi hiyo ya Juni 25, 1999 niliposikia kengele ya kuashiria kuwapo mgeni nje ya uzio wa nyumba aliyetaka kufunguliwa mlango, ‘machale yalinicheza’, kama wasemavyo Waswahili.

Upigaji wa kengele ile mfululizo uliashiria kuwa mpigaji alikuwa na shari. Niliagiza mwanafamilia kwenda kumwambia mlinzi kutofungua mlango kabla ya mgeni yeyote kujitambuliha kikamilifu na mimi kutoa kibali cha kumruhusu kuingia ndani ya uzio wa nyumba. Baada ya kutoa agizo hilo nililetewa jina la mmoja wa ‘wageni’ kadhaa waliokuwa nje.

Ingawa ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusikia jina hilo niliamini kuwa wageni hao ndio wale waliokuwa wamenitafuta ofisini jana. Niliagiza mlinzi awaambie wageni wale kuwa mimi nilikuwa nimekwenda ofisini na asiwaruhusu kuingia ndani. Wageni wale walimjibu mlinzi kwamba walikuwa wametoka ofisini kwangu na kuthibitisha kuwa sikuwapo. Mlinzi alipogoma kufungua mlango  waliendelea kugonga kengele hadi iliposhindwa kuhimili na kufungua. Waliamua kupiga kambi mlangoni nje ya uzio.

Ilipofika majira ya saa nne asubuhi watu hao wakiwa bado nje ya uzio wa nyumba, nilipiga simu kwa watu wawili nikawapa maagizo ya kuja maeneo hayo na kufuatilia mwenendo wa wageni wangu hao. Walikuja na kukuta magari na watumishi wa PCB wakiwa nje ya uzio wa nyumba yangu. Walipita na kwenda kwenye eneo ambako waliweza kuona kinachoendelea nje ya uzio wa nyumba yangu bila kugundulika.

Saa moja baadaye, wale wageni wangu waliamua kuondoka, bila shaka kwenda kupanga mikakati mipya. Mara moja wale wenzangu waliokuwa wanafuatilia mwenendo wa wageni wangu walinipigia simu na kuniamuru kutoka nje mara moja. Huo ulikuwa mwanzo wa kipindi cha wiki moja nilipowindwa kwa kila mbinu na kikosi maalum cha watumishi wa PCB waliokuwa na kazi moja tu: kunikamata na kunisweka mahabusu kwanza; mengine yangefuata baadaye.

Nilikuja kufahamu baadaye kwamba wakati huo Edward Hosea alikuwa amesafiri nje ya nchi akiambatana na Mkurugenzi Mkuu. Kabla ya kusafiri alikuwa ameacha maagizo kwamba ni lazima nikamatwe katika kipindi hicho na yeye apelekewe taarifa huko ughaibuni alikokuwa.

Mara baada ya kunusurika kukamatwa pale nyumbani nilikwenda mafichoni na nikiwa huko nilipigiwa simu na ofisa mmoja kati ya wale wawindaji na kushauriwa kujisalimisha kwao. Alinitisha kwamba iwapo sikufanya hivyo, walikuwa na uwezo wa kunikamata na baada ya kufanikiwa kufanya hivyo ningejutia kuzaliwa. Nilimjibu kwamba kwa kuwa walikuwa na nia ovu na siyo kutekeleza majukumu yao, Mungu asingewaruhusu kunikamata; na kweli, kwa muda wa wiki nzima, wapelelezi waliokuwa wanatumia takribani magari sita ya taasisi hiyo walifanya kazi moja tu: kunisaka na kunitia nguvuni.

Nililazimika kuchukua likizo ya kutokwenda kazini na kutokanyaga wala kulala nyumbani. Siku kazi hiyo ilipoanza, magari matatu kati ya hayo nilipishana nayo kwenye barabara ya Tumbawe, mtaa nilikokuwa naishi nikiwa nimevaa kanzu na tarbushi. Nilikuwa nafuata taksi. Magari mengine yalikuwa yameegeshwa karibu na kanisa la St. Peters, wapelelezi wakiwa wamesimama nje kuangalia magari yaliyokuwa yanapita pamoja na wapita njia wengine.

Katika kipindi hicho nilishinda na kulala (kama kweli nilikuwa nalala) sehemu mbalimbali. Nikishinda Sinza  mchana, usiku nilikwenda Kurasini. Hata Kongowe niliwahi kushinda na kukesha huko!

Wakati niko mafichoni, Julai 13, 1999 maofisa wa PCB walikwenda nyumbani kwangu kwa ajili ya kufanya upekuzi, lakini ulikuwa upekuzi wa kisanii. Walifika nyumbani na kumkuta mke wangu ambaye aliwaruhusu kufanya upekuzi. Walianzia kwenye chumba chetu cha kulala. Ukiacha nyaraka kadhaa walizochukua, hata brief case kadhaa zilizokuwamo huku zikiwa zimefungwa hawakuzichukua. Miongoni mwa vitu walivyochukua katika upekuzi ule kama walivyoandika, ni ‘katiba ya Ngara Development Trust Fund, ‘folder ya 5th training course on customs valuation’, ‘barua mbalimbali binafsi’, ‘expired passports’.

Walipomaliza upekuzi kwenye chumba changu walitaka kukagua vyumba vingine vya kulala, lakini mtoto wetu wa miaka sita aliwagomea kwa kuwaambia, ‘this is my room and brother Job, and that one is the girls’ room’. Walimtii kwa kutoingia katika vyumba hivyo! Hata hivyo, kwa hasira walimchukua mke wangu na kumpeleka Kituo cha Polisi Oysterbay walikomfungulia mashitaka ya kuwatukana!

Kesho yake, Julai 14, 1999 walifanya upekuzi ofisini kwangu pale TRA wakimshirikisha katibu muhtasi wangu kwa kuwa nilikuwa bado mafichoni. Huko walichukua nyaraka kadhaa; nyingi kati ya hizo hazikuwa na thamani yoyote kwa uchunguzi wao. Miongoni mwa nyaraka hizo, kama walivyoainisha wenyewe, ni: ‘paper ya Dr. C. Gasarasi (Genocide in Rwanda), ‘Kagera na Ngara documents sita’, ‘curriculum vitae ya Nyambele, Muhozi, Buzoya, Nyanana na Ndayisaba’, ‘nakala ya cheti cha kuzaliwa cha Ester Kazosi’, ‘business card 3 ya Faith Patrick, Nyambele na Zarro. Sefu ndogo pamoja na brief case mbili zilizokuwa zimefungwa hawakuona umuhimu wa kuzichukua.

Julai 19,1999 nilipata taarifa kwamba Mkurugenzi Mkuu wa PCB alikuwa amerudi ofisini baada ya safari ya nje ya nchi niliyoeleza hapo juu. Kwa mbinu zangu nilikuwa nimekwisha kupata namba ya simu yake ya kiganjani. Nilimpigia simu na kujitambulisha. Baada ya hapo nilimwambia kwamba nimekuwa mafichoni kwa siku sita. Alinipa pole na kuniambia alikuwa amepata taarifa juu ya ‘kuwindwa’ kwangu. Alinitoa hofu na kuniomba kwenda ofisini kwake mchana ule. Nilisita. Nikamwambia kuwa ningekwenda tu iwapo angekubali niende na mwanasheria. Alikubali na kunihakikishia kwamba alikuwa amekwishatoa maagizo kwa wapelelezi kufanya kazi yao bila kunikamata au kunibughudhi kwa njia yoyote ile.

Nilikuja kuthibitisha baadaye kwamba hata ile ilani ya kunitaka kujieleza ilikuwa imetolewa kwangu bila yeye kujulishwa. Mchana ule nilipoonana naye nikiwa na mwanasheria wangu, nilimweleza kwa kina nilichoamini kuwa chanzo cha upelelezi ule. Baada ya kunisikiliza aliniomba nitoe ushirikiano wa dhati kwa wapelelezi wa taasisi hiyo ili waweze kumaliza kazi waliyokuwa wameianza. Baada ya hapo kwa muda wa wiki mbili sikufuatwa wala kukutana na mpelelezi yeyote.

Mara baada ya muda huo kupita, siku moja nilipigiwa simu kutoka huko na kuagizwa kufika ofisini nikiwa na pasi yangu ya kusafiria. Nilipofika tu ofisa huyo aliniomba pasi ile na kuihodhi. Niliambiwa siku kadhaa baadaye na Mkurugenzi Mkuu kwamba hawakufanya hivyo kutokana na kuogopa kwamba ningetoroka. Kumbe miongoni mwa tuhuma nyingi dhidi yangu ilikuwamo ya kupata pasi hiyo baada ya kutoa rushwa kwa maafisa wa uhamiaji kwa kuwa mimi sikuwa raia wa Tanzania!

Baada ya kuchukua pasi yangu, ofisa yule alinikabidhi Ilani ya nyongeza niliyoelezea katika makala iliyopita. Kama nilivyoandika, hoja nyingi katika ilani hiyo zilikuwa zimejibiwa na maelezo yangu ya awali.

Aidha, baadhi ya hoja  katika ilani ile zilitokana na hisia tu za waandishi wake na hazikutokana na walichokuwa wamepata katika upelelezi uliodaiwa kuwa ulianza dhidi yangu hata kabla ya mwaka 1998.

Septemba 13, 1999 niliitwa kwenda ofisini kwa Mkurugenzi Mkuu. Nilipofika aliitwa Edward Hosea. Mkuu huyo alileza kwamba alikuwa amepata hisia kwamba kuna uhasama kati yangu na Edward Hosea kutokana na masuala binafsi.

Alisema kuwa kwa kuzingatia nafasi zetu wawili katika taasisi tulizokuwa tunatumikia pamoja na ushirikiano uliotakiwa baina ya taasisi hizo, ilikuwa ni vema sisi wawili tuelewane. Nasita kueleza kwa undani mazungumzo yale yalivyokwenda. Itoshe kusema kwamba Mkurugenzi Mkuu huyo alinihakikishia kwamba uchunguzi ulikuwa umekamilika na kwamba hatua za mwisho za kiutawala zingefuata. Iliichukua taasisi hiyo takriban miezi minane kukamilisha ‘hatua za mwisho za kiutawala’. Kama nilivyoeleza katika utangulizi wa makala iliyopita, Mei 6, 2000 nilipokea barua iliyonitaarifu ifuatavyo: ‘We have reached a decision that the investigation which was being conducted against you be discontinued.”

Katika barua ya Januari 11, 2006 niliyomwandikia Rais Jakaya Kikwete kumpongeza kwa kuchaguliwa kuongoza taifa hili nilitoa mapendekezo kadhaa juu ya matatizo yetu ya kiuchumi na katika ukusanyaji wa kodi. Kuhusu taasisi ya kuzuia rushwa niliandika ifuatavyo:

“Mimi binafsi naamini kuwa bado kuna matatizo ndani ya PCB na haitatosha kwako kuletewa taarifa tu. Nashauri taasisi hiyo ifanyiwe ‘diagnostic review’ kuangalia kinachoisibu! Aidha, ni vema kuangalia ‘institutionalised corruption’ ambayo wananchi wanajua imo ndani ya baadhi ya vyombo nyeti kama Polisi, Uhamiaji na TRA (hususan ndani ya Idara ya Ushuru) na Mahakama.”

Naye, Karl Lyimo  ambaye ni mwandishi nguli wa makala katika magazeti mbalimbali ya Kiingereza, aliwahi kumshangaa Edward Hosea kwa matamshi  aliyodaiwa (Hosea) kutoa kwenye televisheni ya TBC kwamba “PCCB haiwezi kumaliza rushwa nchini kwa kuwa kazi hiyo ni nzito….itamalizwa kutokana na uadilifu wa Watanzania…msingi mkuu wa kumaliza rushwa ni uadilifu”

Katika gazeti la THE CITIZEN la tarehe 16 Desemba 2010, Karl Lyimo ali andika hivi:

“I was most dismayed to read the views of the anti-corruption czar in Tanzania, Edward Hosea, on fighting corruption. If the man is correct on this, then Tanzanians can kiss goodbye any hope of ever surmounting grand graft – let alone eradicating it!…..Now if I ever heard a defeatist attitude from the commander of a fight force, that is it!”

Hiyo ilikuwa takriban miaka mitano tangu nilipotoa kwa Rais Kikwete ushauri ambao sikuombwa (unsolicited advice)!

1359 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!