Kama tujuavyo, Watanzania tuko katika mchakato wa kutafuta Katiba mpya ya nchi yetu. Katika kipindi hiki, vyama vya siasa vinatoa maoni mbalimbali kuhusu mchakato huo. Nacho Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakikubaki nyuma.

 

Kwanza niwapongeze ndugu zetu wa Chadema kwa mafanikio makubwa wanayopata katika kukusanya nyaraka nyeti.

Walianza kupata nyaraka nyeti za Serikali, sasa wanapata nyaraka nyeti za chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nawapongeza sana.

Haijulikani wale wanaotoa nyaraka hizo wanafanya hivyo kwa sababu ya njaa, au kwa chuki waliyo nayo dhidi ya chama tawala na Serikali yake. Hilo si langu.

 

Nazungumzia hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu. Akitoa maoni yake kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria, Lissu alitoa maoni mazuri na mengine ya kutilia shaka.

 

Kwa upande wa maoni mazuri hapana shaka wananchi wanaungana na Lissu katika kuhoji matumizi ya kutisha ya fedha za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 

Kwa mfano, kuna fungu la fedha wametengewa wajumbe wa Tume za kugharamiwa watakaokuwa wamepata maambukizi ya Ukimwi! Je, wajumbe wameandaliwa kwa zinaa?

 

Kwa upande wa mambo ya kutilia shaka katika hotuba ya Lissu ni kauli yake kwamba Dk. Asha-Rose Migiro, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Uhusiano wa Kimataifa), amehujumu mchakato wa Katiba.

 

Kwa mujibu wa Lissu, Machi 3, mwaka huu, Dk. Migiro alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC ya CCM inayoonesha kujipanga kuingia kwenye mabaraza ya katiba peke yao.

 

Lissu amedai kuwa moja ya barua hizo inasomeka, “Sambamba na hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya mwongozo wa Tume, sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wa watu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea.”

 

Ameendelea kudai kuwa barua pepe ya Dk. Migiro imekamilishwa kwa maneno yanayosema, “Tafadhali wanakiliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.”

 

Binafsi nimesoma tena na tena maneno hayo ya Dk. Migiro na sikuona mahali popote panapothibitisha kuwa Dk. Migiro amehujumu mchakato wa katiba.

 

Labda hapa tunalazimika kukubaliana kwamba hakuna chama cha siasa kisicho na mikakati yake na mbinu zake katika kulishughulikia suala hili la mchakato wa Katiba, hata Chadema ina mikakati yake, mbinu zake na azma yake katika suala hili, haikukaa kimya.

 

Ndiyo maana Chadema waliwahi kususia kikao cha Bunge kilichojadili sheria ya mabadiliko ya katiba. Ndiyo maana Chadema wametamka kwamba wanaweza kujitoa kwenye mchakato huu wa Katiba mpya. Ndiyo maana Chadema wamemtaka mwanachama wao, Profesa Baregu, ajitoe kwenye tume, na kadhalika.

 

Mbona hadi sasa hayupo aliyelalamika kuwa na Chadema inahujumu mchakato wa Katiba? Si ndivyo ilivyojipanga katika kulishughulikia suala hili? Kwanini CCM nayo isijipange?

 

Hizi ni siasa za kupakana matope. Uadilifu wa Dk. Migiro umethibitishwa hata kwenye Umoja wa Mataifa ambako Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-moon, alimsifu sana Dk. Migiro kwa uadilifu wakati alipoagana naye mwaka jana. Utendaji mzuri wa kazi wa Dk. Migiro katika Umoja wa Mataifa umeleta heshima kubwa kwa nchi yake ya Tanzania, kwa bara lake la Afrika, na kwa wanawake wote duniani.

 

Ni aibu kwetu Watanzania kuitangazia dunia kuwa Dk. Migiro amerejea nyumbani kwa lengo la kuhujumu masuala muhimu ya Taifa lake. Tulinde heshima yake na heshima ya taifa letu.

 

Katibu wa Sekretarieti ya NEC ya CCM, Francis Mwonga, amewekwa pia katika kundi la viongozi wa CCM waliohujumu mchakato wa Katiba. Kosa lake ni kuandika kwamba, “Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba mpya mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi.”

 

Kwa vyovyote, maneno hayo si ya kuhujumu mchakato wa Katiba ila yana nia njema tu ya kufanikisha mchakato huo. Mwonga hakusema kwamba vituo visiwe mbali na wanachama wa CCM bali visiwe mbali na wananchi bila kujali kama ni wanachama wa vyama vya siasa.

 

Mwisho, sisi sote tunajua Chadema inavyosumbuliwa na tamaa ya kuingia Ikulu. Katika mazingira hayo ya kutaka kuingia Ikulu kwa kuwapaka matope watu safi, tunalazimika kukumbushana kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kututaka tumwogope kama ukoma mtu yeyote mwenye tamaa ya kuingia Ikulu. Wanakimbilia nini?

1082 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!