Wakati maelfu ya wanafunzi Tanzania katika shule za msingi nchini wanakosa madawati na vitabu, nchini Rwanda nusu ya wanafunzi wanamiliki kompyuta mpakato.

Rwanda inayoongoza katika kuwekeza kwenye teknolojia ya mawasiliano Afrika, ilianzisha mpango huu mwanzoni mwa mwaka 2006 ikiwa na lengo la kutoa kompyuta moja kwa kila mwanafunzi.

 

Balozi wa Rwanda nchini, Dk. Ben Kagangazi, katika mahojiano na JAMHURI amesema Serikali ya Rwanda imeamua kutoa kompyuta kwa kila wanafunzi kupunguza ghrama katika ununuzi wa vitabu.

 

Amesema Rwanda inaona elimu kama mboni ya jicho katika maendeleo yake kuelekea uchumi imara.

 

“ Rwanda tumechagua kuwa elimu ndiyo silaha yetu kuu kwa kuwa tunaamini kuwa uchumi wa Rwanda utakua iwapo vijana watasoma na kuelewa baadaye wainyanyue Rwanda . Tunafanya hivyo tukitambua kuwa elimu ni rasilimali kuu itakayoikomboa nchi yetu, hivyo hatufanyi mchezo katika elimu,” amesema.

 

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anakwenda shule na kumiliki kompyuta yake bila kujali uwezo alionao kifedha.

 

Dk. Rugangazi amesema Serikali inahakikisha kuwa watoto wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini wananunuliwa kompyuta na Serikali.

 

“Serikali ya Rwanda inajali usawa. Haina huyu ni masikini na yule ni tajiri, wote wana haki sawa. Hakuna matabaka kwa kuwa shule zote zinamilikiwa na Serikali, zote zina haki sawa, tuna shule chache sana ambazo ni za kimataifa nazo ni kama tatu hivi, lakini zilizobakia ni za Serikali.

 

“Mtoto wa waziri na mtoto wa raia wa kawaida mwenye kipato cha chini wote wana haki sawa ya kusoma katika shule nzuri, lengo likiwa kuhakikisha matabaka yanaondoka kila mwananchi afaidi matunda ya nchi yake,” amesema.

 

Rwanda yaongoza katika teknolojia ya mawasiliano

Dk. Rugangazi amesema nchi yake imewekeza zaidi katika teknolojia ya mawasiliano, na inafanya vizuri kutokana na mipango mizuri ya Serikali ya Rwanda kuendeleza miundombinu ya mawasiliano humo.

 

“Sekta ya ICT nchini  ikiwa ni pamoja na simu za mikononi na mitandao ya ‘fibre optic’ pamoja na PC na upatikanaji wa Intaneti – imekuwa lengo la msingi kwa umma wa kimataifa na wawekezaji binafsi katika miaka ya hivi karibuni nchini kwetu.

 

“Tumepewa jina la namba moja kwa ICT katika Afrika Mashariki na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), Rwanda imefaidika kutokana na vitegauchumi vinavyolenga ICT,” anasema.

 

Bajeti ya ICT nchini humo kwa sasa iko sanjari na Viwango vya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), ambalo linaundwa na mataifa tajiri 30 na wako asilimia 1.6, juu ya wastani wa Afrika.

 

Rwanda ilizindua “Dira yake ya mwaka 2020” mwaka 2000 ili kujenga na kufufua kikamilifu uchumi wa Rwanda , kwa lengo la kuwa na hadhi ya Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.

 

“Moja ya kazi ngumu inaegemea katika kuimarisha vitegauchumi na hususani mwelekeo wa kisera ili kupata faida kubwa.

 

“Serikali ya Rais Paul Kagame imefanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa, ikiwa inachochea sera bora za ICT na kwa ujumla kusaidia mazingira yanayovutia biashara zaidi,” amesema.

 

Mkakati wa Dira ya 2020 unaangalia kilimo, viwanda, na masuala ya kijamii pia, ukosefu wa bandari nchini Rwanda , bei za juu za nauli za ndege, na kukosekana kwa utulivu kumeifanya Serikali ya Rwanda kuwekeza katika uchumi uliojikita kwenye ICT kama msingi mkuu.

 

Pia imezindua programu ya utafiti wa kisayansi na elimu, teknolojia na ugunduzi, na usambazaji wa mawasiliano.

 

Dira ya 2020 ina lengo la kutoa “wanasayansi wenye elimu kubwa na mafundi ili kutimiza haja ya uchumi wa kitaifa” ambao utaingizwa katika mkakati mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya wakazi wa Rwanda .

 

Dk. Rugangazi amesema Rwanda inaona ICT kama dirisha la fursa kufikia hatua ya maendeleo ya viwanda na kubadili uchumi na kukabiliana kikamilifu na changamoto za maendeleo nchini humo na wakati huo huo ikitumia fursa mpya za kiuchumi na kijamii.

 

Rwanda ina vituo vya Intaneti, viwanja vya ICT, Kituo cha Kompyuta cha Taifa, na Mtandao wa Telemedecine, ambao unaunganisha hospitali za Rwanda na vyuo vikuu katika kujaribu kuleta mabadiliko na kupanua huduma za afya katika maeneo yenye huduma duni.

 

Amesema kuwa Serikali ya Rwanda inaendelea kutoa cha kupeleka teknolojia katika shule za msingi na sekondari, kwani zaidi ya shule za msingi 1,200 zina kompyuta na kwa uchache asilimia 10 ya shule za sekondari nchini Rwanda zina Intaneti zisizounganishwa kwa waya.

 

“RITC inaandaa mafunzo ya ICT kwa walimu wa sekondari wote kutoka mikoani nchini Rwanda . Mafunzo yaliandaliwa kuwasaidia kusambaza ujuzi katika ICT kwa vizazi vichanga,” Dk. Rugangazi amesema.

 

Rwanda imekuwa moja ya nchi za mwisho kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na inatarajiwa kuwa na jukumu kubwa katika kuendeleza sekta ya ICT kwa majirani zake na wanachama wenzake wa EAC.

 

Nchi hiyo tayari imeshaanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa ICT kutoka Afrika Mashariki na ya Kati kuongeza idadi ya wanasayansi na kuongeza kiwango cha maarifa katika teknolojia hiyo katika kanda.

 

Rwanda pia ilichaguliwa kama makao makuu ya kijiografia ya mradi mpya wa Nyaya za Majini wa Afrika Mashariki, mradi mkubwa wa ‘fibre optic’ ambao una lengo la kupeleka mawasiliano ya simu katika vijiji kwa nchi zote kati ya Sudan hadi Afrika Kusini kupitia pwani ya Afrika Mashariki.

 

Sekta ya Afya

Dk. Rugangazi amesema kuwa Rwanda imepiga hatua katika sekta ya afya, hali inayosababisha wananchi kuipenda Serikali yao .

 

Amesema kwa sasa asilimia 95 ya wananchi wa Rwanda wako katika mfumo wa huduma ya bima ya afya, hivyo hakuna mwananchi anayekufa kwa kukosa matibabu. Serikali yake imeongeza bajeti katika Sekta ya Afya, kila mwanachi nchini humo anapata huduma za matibabu bila kujali uwezo wake wa kifedha.

 

“Wananchi wote wanapata haki ya matibabu, kwani tumeboresha mfumo wa bima ya afya, hali ambayo imezaa matunda mazuri nchini kwangu.

 

“Serikali inazingatia sera, kanuni na sheria za manunuzi ya dawa. Tija na ubora wa huduma za hospitali ni vitu vinavyopangiliwa kwa umakini zaidi nchini Rwanda ,” amesema.

Amesema mafanikio yaliyopatikana yamesababisha Shirika la Afya Duniani (WHO), kupeleka wajumbe wake kujifunza jinsi mfumo huo unavyofanya kazi watoe elimu kwa nchi nyingine.

 

Amesema hatua hiyo ililenga kusaidia wanachama wa WHO kusaidiana kwa kubadilishana uzoefu, uamuzi na sera, ili kusukuma mbele maboresho ya afya kwa watu wengi zadi duniani.

 

“Matibabu kwa Wanyarwanda si suala la kuchezea bali ni suala la lazima kwani ukiwa na watu walio na afya yenye walakini huwezi kujenga nchi.

 

“Huduma ya Bima ya Afya inatusaidia sana tunapeleka watu nje ya nchi wanatibiwa kwa huduma hii. Wapo waliopelekwa Afrika Kusini , India na pia wapo walioletwa hapa Tanzania katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na wamepata matibabu yao vizuri na mfuko huo umelipa amesema,” amesema.

 

Mikataba ya uongozi katika uwajibikaji

Dk. Rugangazi amesema mafanikio ya serikali hiyo yanatokana na uwazi katika utendaji wake. Kila kiongozi wa nchi hiyo anatakiwa kusaini mkataba utakaoonesha jinsi anavyotakiwa kutekeleza majukumu yake kwa mwaka mmoja.

 

“Hivi unavyoniona hapa kila mwanzo wa mwaka natakiwa kupeleka jinsi nitakavyofanya kazi yangu na hadi kwa wananchi na mwisho wa mwaka, Rais anakuja kukagua kama nimefika katika viwango vilivyopangwa na nikishindwa nafukuzwa kazi, natakiwa kufika asilimia 70 ya mlengo yangu,” amesema.

 

Amesema Serikali hiyo imepeleka madaraka kwa wananchi, hivyo Meya wa Wilaya anatakiwa kuangalia nini wananchi wake wanataka kufanyiwa kwa ajili ya maendeleo yao.

 

“Ukitoa ahadi lazima utekeleze, kila mwanzo wa mwaka Rais anatuita unaeleza matatizo ya wilayani kwako au kazi yako, unaandika kuwa hakuna shule au hospitali unatakiwa kujenga.

 

“Na mwisho wa mwaka unatakiwa kutoa taarifa ya utekelezaji, kama hujafikia asilimia 70 unafukuzwa kazi. Kagame hataki mchezo katika utendaji, anasema Serikali ya Rwanda si yake ni ya wananchi na hana urafiki katika utawala, hacheki na mtu,” anasema.

 

Dk. Rugangazi  amesema kuwa jambo la kuwafukuza viongozi wazembe hufanywa hadharani na kila mwananchi anaona na kusikia.

 

Amesema kuwa kufanya hivyo kunasababisha ushindani katika kuwajibika kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa, kwani hakuna mtu anayependa kufukuzwa kwa aibu kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi.

 

Uwekezaji

Amesema uchumi wao una mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji. “Tunashukuru kwa mambo ya uwekezaji tuko juu sana . Sisi sheria zetu ziko wazi mno. Hatuna ubabaishaji.

 

Mfano, kama unataka kusajili kampuni yako leo, ni baada ya siku tatu unapata usajili kila kitu kipo sawa. Wawekezaji wengi wanakimbilia kwetu,” amesema.

Kuwawezesha kiuchumi wananchi masikini.

 

Dk. Rugangazi amesema Serikali ya Rwanda inahakikisha wananchi wanaishi katika mazingira mazuri. Anasema imeanza kutoa ng’ombe kwa mwananchi wa kipato cha chini ili waweze kujikimu na ugumu wa maisha.

 

Amesema kuwa mpango huo unajulikana kama ‘Giragirika’ kwa lugha ya Kinyarwanda ukiwa na maana ya ng’ombe mmoja kwa kila familia umefaulu kwa kiasi kikubwa kuondoa umasikini.

 

Hatua hiyo, unaona kuwa unatoa ng’ombe mmoja huyo mtu anapata maziwa, mbolea na pia fedha na anaishi maisha mazuri yeye na familia yake.

 

Amesema mpango huo ulianzishwa na Rais Kagame na sasa imekuwa kila mwenye kipato kikubwa Serikali inamtaka kuchangia maskini nchini Rwanda . Yeye, kwa mujibu wa cheo chake, anatakiwa kuachangia ng’ombe 66 anaporudi likizo.

 

Wanawake washika nafasi za juu

Dk. Rugangazi amesema Rwanda imeweka rekodi ikiwa ndiyo nchi yenye idadi kubwa ya wanawake bungeni duniani, na kushika nafasi ya kwanza kutoka asilimia 23 na kuwa na wabunge wengi wanawake ulimwenguni. Rwanda ina wabunge 56. Wanawake nchini Rwanda wamepigana muda mrefu hadi kufikia hapo.

 

Amesema sasa wanawake wanafanya vizuri  katika Serikali hiyo, uwakilishi huo mkubwa wa wanawake umeleta maendeleo katika siasa za Rwanda .

 

1613 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!