Mikopo mingi yatumika kwa mahitaji binafsi

Fedha nyingi wanazokopa Watanzania kutoka vyanzo mbalimbali hutumika zaidi kukidhi mahitaji yao binafsi kuliko kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji na kununua rasilimali kama nyumba na ardhi, utafiti uliofanywa hivi karibuni na jarida moja la nchini Uingereza umebaini.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo yaliyo kwenye wasilisho lililofanywa hivi karibuni na Mwanahiba Mzee ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Ecobank Tanzania, asilimia 44 ya watu wazima wote nchini walikuwa wamekopa kwa njia moja au nyingine katika kipindi cha miezi 12 wakati utafiti huo unafanyika.

Jarida hilo la Global Banking & Finance linasema asilimia 74 ya wakopaji hao walikopa kwa ajili ya matumizi binafsi huku asilimia 19 ya mikopo yote iliyotolewa ilitumika kwa ajili ya uwekezaji huku asilimia saba iliyobaki ikitumika kununua rasilimali.

“Mara nyingi Watanzania hukopa kutoka kwa marafiki au ndugu na hii hufanywa kwa kiwango cha asilimia 69 ya wakopaji wote. Wakati utafiti wa jarida la Global Banking & Finance unafanyika, benki zilikuwa zimewakopesha asilimia tatu tu ya watu hawa. Mikopo iliyokuwa imepatikana kutoka vikoba na saccos ilikuwa asilimia 20,” Mwanahiba aliwaambia washiriki wa Mkutano wa Taasisi za Fedha nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga, alifafanua kwanini bado watu wengi hawakopesheki na kutoa sababu za mikopo ya benki kuwa ghali. 

Kwa mujibu wa Prof. Luoga, changamoto kubwa ni suala la utambulisho na utambuzi wa wakopaji binafsi ambalo huzipa mtihani mkubwa benki nyingi na kuzifanya kuweka riba za juu kwenye mikopo.

“Pamoja na jitihada zilizofanywa na Benki Kuu kuhakikisha kuwa benki na taasisi za fedha zinatoa mikopo nafuu na kwa wananchi wengi zaidi, bado kumekuwa na changamoto ya utambulisho na utambuzi wa wateja. Hali hii inasababisha benki kuweka riba za juu kwenye mikopo, hivyo kutoa mikopo kwa wateja wachache,” Prof. Luoga anasema.

“Tunatambua jitihada zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na serikali katika kutoa vitambulisho vya taifa na tunaamini kwamba kuongezeka kwa upatikanaji wa vitambulisho vya taifa kwa Watanzania wengi zaidi, hasa walioko vijijini, kunaweza kuchangia kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu zaidi kwa wananchi na wazalishaji wengine,” anasema.

Takwimu za taasisi hiyo zinaonyesha kuimarika kwa upatikanaji wa mikopo siku za hivi karibuni baada ya kudorora kwa muda mrefu kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu. BoT inasema utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi kumeanza kuwa na mafanikio, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi.

Ukuaji wa mikopo kwa sekta hiyo ulifikia asilimia 9.3 mwezi Septemba 2019 baada ya kuchukuliwa hatua mbalimbali na serikali kupitia Benki Kuu, kufuatia ukuaji mdogo wa wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2018 na wastani wa asilimia 2.2 mwaka 2017, kulikotokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la mikopo chechefu.