Milioni 50 kila kijiji, walipa kodi wapya

Kwa mara ya kwanza Serikali mpya ya Rais John Pombe Magufuli, imesoma bajeti yake ambayo tumeona fedha nyingi zikipangwa kwenye miradi ya maendeleo. Ni jambo jema kwa kuwa wakati wa kampeni tuliahidiwa Serikali itatatua matatizo ya wananchi hasa kuwapatia maendeleo. 

Napongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikichukua katika kuweka nidhamu ya matumizi na kazi. Sasa tunaona mabadiliko katika utoaji huduma na ni matumaini yangu Serikali hii itaendelea na kasi hii na tutaikumbuka kama Serikali ya Mwendokasi. 

Bajeti hii imejikita katika kusimamia nidhamu ya mapato ya Serikali, kujenga uchumi imara wa viwanda, kutatua matatizo ya wananchi na kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabishara wa ndani na wale wa nje ambao wapo tayari kuwekeza nchini. 

Kuna mambo mengi ya kupongezwa katika bajeti hii na yapo masuala machache ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebesho kabla ya utekelezaji wake na ni matumaini yangu wabunge watafanya marekebisho. 

Nimependezwa na hatua ya Serikali kuyataka mashirika ya umma yanayofanya biashara kupeleka asilimia 15 ya faida kabla ya kodi serikalini. Ni nzuri na itajenga uwajibikiaji kwa watendaji wanaoendesha mashirika haya na tunatarajia kuona mashirika haya yakitengeneza faida kila mwaka.

Ni muhimu kwa Serikali kuweka utaratibu au sheria ambayo itasema mapato kama yatakayopatikana kutoka kwenye haya mashirika yatatumika katika shughuli zipi za maendeleo au kijamii kwa mfano kujenga madarasa, zahanati au nyumba za walimu.

Ni matumaini yangu Serikali itaangalia namna ya kupunguza kodi kwenye miamala ya simu na taasisi za fedha kwani Watanzania wachache wanatumia huduma hizi ambazo zimerahisisha maisha ya kila siku.

Makala yangu itajikita katika Sh bilioni 59 ambazo zitatolewa katika vijiji mbalimbali kusaidia makundi hasa wanawake na vijana kutengeneza ajira na kuongeza kipato. Hatua hii ni nzuri ila nategemea kabla ya utekelezaji Serikali itaweka utaratibu mzuri wa jinsi pesa hii itakavyotumika sababu siyo mara ya kwanza kwa Serikali kutoa pesa kwa wananchi na wengi tunakumbuka “Mabilioni ya Kikwete”. 

Kabla ya kutoa pesa hizi lazima Serikali ifanye utafiti kujua pesa zilizotolewa kipindi cha nyuma zilitumikaje, zilisaidia watu wangapi na zimechochea vipi kukuza uchumi wa nchi. 

Bilioni 59 zikitumika vizuri zinaweza kusaidia Serikali katika kuongeza mapato na pia kupunguza tatizo la ajira nchini. Bila kuwa na mpango mkakati mzuri, taarifa za kutosha na kuweka matarajio ni vigumu kutatua tatizo lolote na kuna hatari ya kuendelea kurudia makosa ya nyuma bila kujifunza. 

Serikali ina mpango wa kuhakikisha sekta isiyo rasmi inaanza kulipa kodi na kwa kutumia hizi pesa inaweza kuwa fursa ya pekee ambayo itachochea sekta hii kuanza kulipa kodi.

Ili pesa hii iweze kutumika kwa lengo linalokusudiwa, ni vyema Serikali ikaweka utaratibu ambao utahakikisha pesa hizi zitaenda kusaidia kukuza biashara na kuongeza ajira kwa vikundi kuliko kumpatia mtu mmoja mmoja. Pesa zinapokuwa ndani ya kikundi kunakuwapo na uwajibikaji kwa watendaji na matumizi yatakuwa yanafuatiliwa.

Tunafahamu wapo vijana na kina mama wengi ambao wamejiajiri katika shughuli mbalimbali kama utengenezaji wa viatu, ufugaji, kilimo, ushonaji na ufundi mbalimbali ambao unawapatia kipato cha kila siku. Watu hawa ni wengi na biashara zao zimekuwa hazikui kwa kasi na pia hawajapata fursa ya kupata mikopo ambayo itawasaidia katika kukuza biashara zao. 

Hili limechangia wao kutokolipa kodi kwani hawana uhakika wa kipato cha kila siku na hivyo ni muhimu kusaidia watu ambao watarasimisha biashara zao walipe kodi. 

Mapendekezo yangu ni kuwa kabla ya kutoa milioni 50 kwa kila kijiji, wakuu wa wilaya wakishirikiana na watendaji wa kata na mitaa wapewe muda wa kukusanya taarifa za watu wote ambao wanajihusisha na shughuli za maendeleo, wafahamu wanaingiza kipato gani na wanahitaji kiasi gani waweze kukuza biashara au shughuli zao. 

Katika kukusanya taarifa hizi ni lazima pia kufahamu kiasi cha pesa ambazo watu hawa wamewekeza, wametoa ajira kwa watu wangapi na kama wakiwezeshwa watatoa ajira kwa watu wangapi. 

Taarifa hizo zikipatikana zitaisaidia Serikali ya Kijiji kutoa kipaumbele cha pesa hizi kwa wananchi ambao tayari wana shughuli zinazoingiza kipato na pia kuchochea watoe ajira kwa watu wengine. Taarifa kuhusu watu au vikundi ambavyo vinajishughulisha na maendeleo zinaweza kuwekwa kwenye mtandao kama kuna taasisi za kifedha au watu binafsi wanaweza kuzipata na kutoa mkopo au msaada ambao utakuza biashara, iweke wazi.

Kwa sasa kuna vikundi mbalimbali vya kusaidiana na kuwekeza (VICOBA) ambavyo watu wanachanga kila mwezi ila hawana sehemu ya kuwekeza hivyo hivyo uwepo wa taarifa hizi utatoa mwanya kwa watu wengi kujua fursa zilizopo na kuwekeza.

Napendekeza pesa hizi ziwekwe kwenye mfuko maalumu ambapo utakuwa unasimamiwa na kamati maalumu itakayoundwa na wilaya au kata ambayo itahakikisha mfuko huu unakuwa endelevu na kila kikundi ambacho kitafaidika na pesa hizi kitapewa muda wa kurudisha kiasi walichopewa kutoka kwenye mfuko kikiwa na riba ndogo riba kila mwezi.

Lengo la uwepo wa riba ni kuhakikisha vikundi vinakuwa na nidhamu katika matumizi na pia kuhakikisha mfuko unakuwa kwa ajili ya kusaidia vikundi vingine ambavyo vitakuwa vinasubiria pesa hizi.

Usimamizi wa mfuko huu utabaki chini ya Mkuu wa Wilaya kama Mwenyekiti huku akisaidiwa na wataalamu mbalimbali kutoka ngazi na kada kama maafisa biashara, maafisa kilimo na watendaji wengine ambao watahakikisha pesa inayotoka inakwenda kwenye shughuli itakayorudisha faida. Madiwani na wabunge wanaweza kushirikishwa pia katika kufanya uamuzi.

Kukuza sekta binafsi na kutatua ukusanyaji wa mpato kila kikundi au kampuni itakayopata pesa kutoka kwenye mfuko huu wa milioni 50 ni lazima isajiliwe katika ofisi ya biashara ya wilaya na TRA walipe kodi kidogo ambayo itasaidia kukuza pato la Taifa.

Hapa TRA inaweza kuweka sheria ambayo itatoa unafuu wa kodi kwa sekta isiyo rasmi ambayo itafaidika na pesa hizi. Maafisa wa kodi na  wale wa biashara watapaswa kuwafuatilia hawa wajasiriamali wapya ambao watakuwa wamepewa pesa na Serikali kwa lengo la kuhakikisha biashara haifi na pia kutoa ushauri wa kitaalamu.

Kwa utaratibu huu utaiwezesha Serikali kutengeneza walipa kodi wapya ambao wataongeza mapato na hivyo kufikia lengo la kuhakikisha sekta binafsi inalipa kodi.

Katika kudhibiti matumizi na kutengeneza uwajibikaji, mfuko wa kila kijiji utakuwa unafanyiwa ukaguzi kila baada ya muda kuhakikisha pesa zinatolewa kwa walengwa na zinatumika katika shughuli iliyokusudiwa.

Ngazi ya mkoa inaweza kuunda kamati nyingine ambayo itakagua miradi yote na kuhakikisha pesa imepelekwa katika mradi husika na pia kuwabana watendaji wa wilaya ambao watakuwa wanaisimamia.

Kama nilivyosema awali, taarifa kuhusu watu wanaojishughulisha na biashara au ujasiriamali ni muhimu katika kuandaa sera za kodi na pia kuweka mipango mizuri ambayo itakuza biashara, uchumi na kutengeneza ajira.

Wizara zenye dhamana ya kusimamia kazi na biashara watapaswa pia kukusanya taarifa kujua ni kwa kiasi gani hizi bilioni 59 zimesaidia kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa Watanzania wengi.

Wizara watapaswa kutoa taarifa kila baada ya miezi sita kuonesha ni ajira ngapi zimetengenezwa, kodi kiasi gani imekusanywa na ni vikundi vingapi vimefaidika na pesa hizi.