Moja ya mambo ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yatamfanya asisahaulike kwayo, ni kule kujiamini hata kuwakemea wakoloni na rafiki zao.

Mmoja wa watu wachache waliobaki leo wanaowasema moja kwa moja ni Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe, japokuwa kuna mahali amekwenda kinyume.


Hizi nchi zinazojitangaza kwamba zimeendelea na zinazotumia mamilioni ya pesa kujitangaza hivyo na kuzitangaza nchi zetu za Afrika kwamba zinadumaa, zinanitatiza sana.

Wiki iliyopita tangu Jumatatu hadi mwisho wa wiki kulikuwa na kichefuchefu cha aina yake, kilichosababishwa na Waingereza wanavyoisema vibaya Afrika.


Tangu alfajiri hadi usiku, Radio One ya BBC ilikuwa ikieleza jinsi watu wao walivyo Zambezi, nchini Zambia, kwa ajili ya kuchangia watoto wasiojiweza.


Pesa zao hatuzikatai, lakini hatutaki misaada ama ya masharti au ya kutudhalilisha sisi na Uafrika wetu na maendeleo yetu, kwamba eti si malikitu.


Sasa watu kama watano au zaidi wametoka Uingereza, wameingia Zambia na kwenda kupiga makasia kwenye Mto Zambezi, wanasema wanachangia watoto wanaokufa kila saa, wanaokosa chakula na wanaoumwa na mbu saa zote Afrika.


Wanatumia pesa nyingi kutangaza na kupiga simu na kuongea na hao jamaa walio Zambia, fedha ambazo zingetumika kuwasaidia hao watoto kama wapo.


Wale walioko huko Zambia wanatoa stori kwamba hali ni mbaya, watoto wamekonda, hakuna chakula wala shule na shule zilizopo zipo mbali, kila mahali wamezungukwa na mbu, mpango wao wanauita ‘The BT Red Nose Challenge: Hell and High Water.’


Pamoja na kujisikia vibaya, niliendelea kusikiliza tu, wakadai eti ili ulale usiku na usife lazima ujifungie kwenye neti ambapo usingizi hauji kwa kuogopa mbu wa malaria inayoua mara moja.


Halafu sasa wakajipamba wao kuwa wanapiga makasia kwenye Mto Zambezi, ambao ni hatari kubwa sana, kuna viboko na mamba na uwezekano wa kuliwa ni mkubwa. Eti wanafanya safari hizo kwa sababu wanaipenda sana Afrika na hao watoto, kwa hiyo wapo tayari kufa ili kuchangisha pesa hizo.


Hiyo ilikuwa tisa, kumi ni Ijumaa yenyewe fainali, ambapo waliamua kwamba jamaa mmoja aliyekuwa Zambia angevua nguo zote. Kwa hiyo tangu asubuhi wakatangaza kuhamasisha watu wachangie kwa ujumbe kwenye simu ambao ni paundi moja ili zikifika 50,000 Craig James avue nguo hadharani kwa ajili ya Afrika.

 

Hatuhitaji Mwingereza wala Mmarekani kutuvulia nguo kutuonyesha utupu wake na vikorombwezo vya ndani yake ili tupate pesa!


Hiyo ni pesa chafu na wabaki na uchafu wao, maana mtu mzima anavua nguo ili iweje? Halafu eti kuna mwenzake aliyekuwa kwenye ghorofa kubwa London, naye akatangaza kuvua nguo zote ila abaki na chupi tu. Halafu, nirudie tena jameni, kwa ajili ya Afrika na njaa na magonjwa na ujinga wa watu wake, akapanda na kushuka kwenye lifti ya jengo ambayo ni ya kioo anaonekana hadi nje.


Kweli pesa zile zilitimia, Zambia jamaa akasaula akabaki kama alivyozaliwa, akatembea mtoni na kuingia kwenye maji na huku London jamaa akavua na kubaki na boksa ya zambarau halafu anahojiwa moja kwa moja na Radio One.


Eti kwa ajili ya Afrika, eti kwa ajili ya masikini, huu ni udhalilishaji mkubwa na viongozi wetu wakemee. Kama unachangia kuwa basi kama Beckham aliyejisajili Ufaransa kwa heshima na anachangia yatima.


Kweli tuna shida lakini hatujafikia mahali hapo, kwa hiyo mimi sitambui hicho wanachoita ‘The BT Red Nose Challenge: Hell and High Water’. Mimi walikuja hospitalini kwangu nikawafukuza. Nachangia lakini sijitangazi, mwee.

Leejoseph2@yahoo.com


1149 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!