Wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alizungumza neno zuri. Sina hakika kama viongozi wetu waliweza kulisikia na kulitafakari, kutoka kwenye hotuba ya kiongozi huyo wakati akizindua Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, mkoani Arusha.

Alisema ujenzi wa chuo hicho ulikuwa ukwame baada ya wafadhili, wakiwamo Benki ya Dunia kukataa kutoa fedha. Kwa kutambua umuhimu wa chuo hicho kwa Tanzania na Afrika, Rais Kikwete alisema ilimlazimu kutumia mfumo uliotumika kwenye ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.


Mfumo huo ni wa kutumia fedha za ndani kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Sh bilioni 90 zimetolewa na Mifuko hiyo kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Chuo cha Nelson Mandela. Tunaweza kutofautiana na Rais Kikwete kwa mengi, lakini kwa hili anastahili pongezi.


Tunapaswa kumpongeza walau kwa hilo kwa sababu Tanzania si nchi masikini kiasi cha kushindwa kujiletea maendeleo. Tanzania ni kama familia iliyo na kila aina ya chakula ndani ya nyumba, lakini ikawa haiwezi kupika na kupakua, badala yake ikaenda kuhemea kwa majirani. Hiyo si aibu na fedheha tu, bali ni ujinga wa wenye nyumba hiyo.

 

Hatua hiyo ndiyo iliyonifanya nishawishike kuitazama picha ya maofisa wa Jeshi letu – Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Baada ya kuitazama, nikaingia kwenye mtandao na kukutana na maneno haya, “US Ambassador to Tanzania Alfonso E. Lenhardt (right), presents ambulance keys to the Chief of Medical Services of the Tanzania Peoples Defense Force (TPDF), Major General A.S Mwabulanga (left), during a donation ceremony held [yesterday] at the TPDF Headquarters in Dar es Salaam.”

 

Baada ya kusoma maneno hayo nikajikuta nikikosa amani kabisa rohoni. Nikaanza kujiuliza ni kwa namna gani Wamarekani au mataifa mengine ya Ulaya yanatutazama kwa kuikubali misaada ya ajabu ajabu namna hii. Thamani ya gari hilo la wagonjwa haikutajwa, lakini ni wazi kwamba si kitu kilichostahili kutolewa na “Wananchi wa Marekani” kwa chombo chetu nyeti na cha kujivunia kama JWTZ.


Umasikini ni mbaya. Lakini umasikini wa kukosa maarifa na staha ni mbaya zaidi. Naomba ndugu zangu wa JWTZ waniwie radhi kwa maneno haya. Sina nia mbaya. Ninachofanya hapa ni kujaribu kuondoa aibu hii kwa jeshi letu mahiri pamoja na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Sijawahi kuona picha za maofisa wa Marekani wakitukabidhi misaada ya ndege vita, vifaru na mitambo mingine yenye thamani kubwa. Msaada wa gari la wagonjwa, hata kama thamani yake ni Sh milioni 300 ni aibu kubwa kwa Jeshi na kwa nchi. Tena mbaya zaidi, gari hilo linapokuwa moja tu!


Ndugu zangu, Tanzania haijawa masikini kiasi cha kubembeleza msaada wa gari la wagonjwa kutoka kwa Taifa kama Marekani. Hivi kweli Rais mstaafu George Bush aliyeishi hapa nchini kwa siku zaidi ya nne na akajionea utajiri usio kifani, atatuweka kwenye kundi gani akisikia kuwa Jeshi la Tanzania limepewa msaada wa gari la wagonjwa?

 

Utajiri wa Ngorongoro, utajiri wa Serengeti, utajiri wa tanzanite, utajiri wa almasi, utajiri wa dhahabu, utajiri wa bahari yenye urefu wa kilometa karibu 1,000, utajiri wa maziwa – Tanganyika, Victoria, Nyasa, Rukwa – utajiri wa mito mamia kwa mamia, utajiri wa bandari zenye kupokea na kusafirisha mamilioni ya tani kila mwaka, utajiri wa hifadhi za

 

Taifa zaidi ya 14; nchi yenye pori la akiba (Selous) kubwa kuliko yote duniani, nchi yenye Mlima mrefu uliosimama pekee duniani (Kilimanjaro), nchi yenye mabonde mazuri yanayofaa kwa kilimo cha kila aina, hifadhi za miti zisizopatikana sehemu nyingi za Afrika, utajiri wote huu bado Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linawatuma majenerali kupokea msaada wa gari la wagonjwa?


Hivi kweli huu ndiyo msaada wa kuwafanya maofisa wetu wafunge ofisi ili waende kushiriki mapokezi? Kama hii si laana kwa Taifa lililojaaliwa utajiri, ni nini? Je, huku si kumkufuru Mungu? Tuna gesi, na kuna dalili ya mafuta. Vyote hivi tunaviacha na kwenda kuomba gari la kubeba wagonjwa? Au je, kuwa ombaomba ni kipaji kama cha ndugu zangu Wagogo, maana Mgogo hata akiwa na ng’ombe 1,000 bado atawaacha zizini na kwenda mtaani kuomba!


Ndugu zangu, wengi wetu, nikiwamo mimi, ni ombaomba. Lakini kuomba kunahitaji staha. Usipokuwa makini kwa kile unachokiomba, na yule anayeombwa akajiridhisha kuwa kweli unachoomba unastahili kusaidiwa, utadharauliwa.


Lakini wakati mwingine si lazima uombe. Mtu anaweza kujifanya anakuletea zawadi au msaada. Kwa mwerevu si lazima kila msaada uukubali. Mathalani, si lazima upokee samaki au mnyama usiomla kwa sababu tu yule aliyeamua kukusaidia kakuletea msaada huo. Tatizo la JWTZ kwa msaada huu kutoka Marekani ni kwamba inaelekea sisi ndiyo tuliouomba! Kama kweli tuliketi na kuona jambo la maana kabisa kwa jeshi letu ni kuomba msaada wa aina hii, basi tunapaswa kujitafakari upya.


Kwa nchi kama Marekani, msaada wa kuwaomba ni wa kuimarisha kiwanda kama cha Nyumbu ili siku moja tutengeneze, si magari ya suluba pekee, bali hata magari ya wagonjwa. Leo majenerali wetu wakikutana na Balozi wa Marekani, wakamwomba msaada mkubwa “wenye akili”, Balozi na Serikali ya Marekani watatuona tuna akili.

 

Lakini kwa kuomba gari la wagonjwa, inadhihirisha kabisa kuwa shida yetu si wagonjwa hao tuliowambea gari, bali tatizo letu ni la kupata msaada wa kiakili ili kuzifanya bongo zetu ziwaze na kuomba misaada ya maana. Kwa maneno mengine ni kwamba tunahitaji ambulance za kuutoa ubongo wetu kwenye utegemezi hadi kufika kwenye kujitegemea.


Kuna hadithi ya kweli inayomhusu mzee mmoja aliyekuwa akiishi Msasani; pamoja na kiongozi mmoja wa kitaifa. Inaelezwa kuwa baada ya mzee huyo kumsaidia kiongozi huyo eneo la shamba kwa ajili ya nyumba, kiongozi alifurahi na kumwambia, “Mzee nakushukuru sana, sasa unataka nikusaidie nini zaidi ya fedha nilizokupa?” Yule mzee hakusumbua kichwa, akamjibu; “Mheshimiwa nisaidie bia”. Akionesha kusikitishwa na aina ya msaada alioombwa, mheshimiwa akaagiza yule mzee epewe kreti tano za bia, na nyingine kwa idadi hiyo, za soda!


Hii ina maana gani? Hii ina maana kwamba wakati mwingine tunapokuwa tunaomba misaada, lazima tupime ni nani tunayemwomba na uwezo wake wa kusaidia unaweza kuwa katika ngazi gani? Inawezekana majenerali wetu walipoambiwa kinachowasumbua kwenye tasnia ya afya jeshini, kitu cha maana walichoomba ni gari la wagonjwa badala ya mitambo ya kuwawezesha wao wenyewe kuanza kutengeneza magari!


Nasema hivyo kwa sababu haiwezekani Balozi wa Marekani aombwe mashine za kiwanda cha Nyumbu, halafu yeye akaamua kutuletea gari la wagonjwa! Haiwezekani. Na kama kweli majenerali wetu huo ndo msaada waliouomba kutoka kwa Balozi wa Marekani, kwanini tusiseme kuwa wametuaibisha?


Mwisho, niseme kuwa sisi kama nchi, ili tupate heshima, tunapaswa kufikiria zaidi dhana ya KUJITEGEMEA. Misaada hii ya gari la wagonjwa, kusaidiwa kuchimbiwa vyoo shuleni, kuomba misaada ya madawati kwa wanafunzi wetu, kuomba msaada wa kuchimbiwa visima; kujengewa mageti kama pale Ngorongoro, ni aibu. Aina hii ya ombaomba inatufanya tuwe vilemba.


Kwa mara nyingine nasema msaada huu ambao Marekani imelipatia jeshi letu tukufu, ni aibu na fedheha kwa Watanzania.


Tuamue mgodi mmoja ugharimie vitu kama hivi! TanzaniteOne wanadaiwa kodi inayozidi Sh bilioni 3. Je, fedha hizo tukizipata haziwezi kununua magari ya wagonjwa “ya kienyeji” kama hili tulilopewa na “Watu wa Marekani?” Tutafakari.


1444 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!