Uharibifu misitu: Janga linaloiangamiza Tanzania (1)

Tanzania ilibahatika kuwa na hazina kubwa ya misitu ya asili karibu katika kila wilaya na mkoa. Takwimu za mwaka 1998 zinaonesha kuwa Tanzania Bara ilikuwa na hekta (ha) milioni 13 za misitu iliyohifadhiwa kisheria (ikiwa ni zaidi ya misitu 600 ya Serikali Kuu na misitu 200 ikimilikiwa na Serikali za Mitaa, yaani, Halmashauri za Wilaya.

Wakati huo ilifahamika kuwa kuna maeneo mengi ya misitu ya asili ambayo haikuwa imehifadhiwa kisheria, na kujulikana kama msitu ya asili katika maeneo ya matajiwazi (general forest lands). Maeneo mengi yapo katika ardhi za vijiji. Misitu hiyo inakadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta zaidi ya milioni 20.

 

Natumaini wengi wetu tumezaliwa wakati hali ya misitu na mazingira kwa ujumla katika maeneo tuliyozaliwa ikiwa inatia moyo. Nakumbuka nikiwa mdogo (miaka ya 1950 na 1960), sehemu ya nyumbani ilikuwa na misitu mingi ya asili. Kijiji nilichozaliwa na vinginevyo vilikuwa na maeneo mengi ya chemichemi, vijito na mito ilionekana kila mahali.

 

Suala la maji halikuwa na mjadala na yalikuwa yanapatikana karibu na kwa urahisi sana. Nyakati za masika haikuwa rahisi kwa watoto kuweza kuvuka mito kutokana na maji kuwa mengi sana. Kwa baadhi ya mito, hata watu wazima ilikuwa inawawia vigumu kuvuka kutokana na wingi wa maji.

 

Vile vile misitu ilikuwa ikihifadhi wanyamapori na watoto tulikuwa tunazuiwa kwenda nje usiku, maana fursa za kukutana na wanyama kama chui au fisi zilikuwa kubwa. Ukiacha miti kuwa mingi, pia uoto mwingine wa asili kama nyasi za aina nyingi vilikuwapo. Nyasi zilikuwa ndefu kiasi kwamba njia za miguu ilikuwa vigumu sana kupita nyakati za mvua hasa mvua za masika (Machi hadi Juni).

 

Wengi wetu shule za msingi hazikuwa karibu na nyumbani kama ilivyo sasa. Nilipoanza darasa la kwanza mwaka 1958, shule ya karibu na nyumbani ilikuwa maili tano (kama kilomita 8). Kwenda shule na kurudi ilikuwa changamoto kubwa maana njia zilijaa umande na nguo hasa kaptura zilikuwa zinalowa kutokana na umande uliokuwa kwenye nyasi ndefu na nyingi. Wengi walichukia shule kwa kuogopa umande. Bahati nzuri mimi ni mmoja wa waliovumilia na hatimaye kuweza kuendelea na masomo hadi kufikia kiwango nilicho nacho sasa.

 

Nilipoanza utumishi serikalini mwaka 1977 nikiwa Afisa Misitu Daraja la III katika Wizara ya Maliasili na Utalii, hali ya misitu nchini ilikuwa inatia moyo na mazingira yalikuwa katika hali nzuri. Misitu iliyohifadhiwa kisheria ilikuwa na Walinzi Misitu (Forest Guards). Leo watumishi hao hawapo. Serikali ilifuta kada hiyo na hivyo kusababisha misitu ya asili ikose ulinzi na usimamizi wa kutosha. Kusema kweli nimestaafu Desemba 2012 na kuacha hali ya misitu ikiwa ya kusononesha sana.

 

Uvamizi katika misitu ni mkubwa sana. Uvunaji na ukataji miti kwa matumizi mbalimbali ya binadamu umekithiri. Hata kama idadi ya Watanzania imeongezeka sana, hali ya uharibifu kwenye misitu iliyo chini ya uangalizi wa sheria unatokea kutokana na kukosa ulinzi na usimamizi madhubuti (walinzi misitu hawapo). Misitu ipoipo tu bila ya kuwa na ulinzi wa kutosha. Kwa maneno mengine ni “rasilimali ambayo haina mwenyewe” (open access resources).

 

Watanzania karibu wote vijijini na mijini wanaielewa hali hiyo, hivyo wanafanya wanavyotaka wakifahamu kuwa hakuna wa kuwazuia. Utashi wa kisiasa kwa masuala ya misitu si mzuri sana. Idara imekuwa na watumishi wachache na sasa ni Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forest Service-TFS), lakini bado watumishi ni wachache na walinzi misitu hawapo. Hivyo kuna changamoto nyingi sana katika kulinda na kusimamia rasilimali misitu.

 

Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanalijua hili na wanajinufaisha na kujitajirisha kupitia misitu kwa kukwepa kulipa ushuru kwa mazao ya misitu. Hawataki kufuata taratibu zilizopo na isitoshe wapo watumishi katika idara na Serikali kwa ujumla wake, wenye uchu wa kujinufaisha binafsi kwa kushirikiana na wafanyabiashara ambao si waaminifu.

 

Utendaji wenye kufuata maadili mazuri umekuwa wa shaka sana katika maeneo mengi ya misitu nchini. Wengi tunaangalia namna gani tutapata fedha na ikafika mahali nyundo za idara za kuhalalisha mazao ya misitu hasa magogo na mbao, zenye viainisho vya FD (Forest Division) na kufuatiwa na namba, vikabatizwa jina na FD kuitwa “Fedha Daima”.

 

Kwa hali hiyo, Bwana au Bibi Misitu aliyebahatika kupewa hiyo nyundo alijiona anaogelea kwenye fedha kwa kuwahudumia wafanyabiashara wasio waaminifu na kuifanya Serikali ikose mapato. Kibaya zaidi ni kuifanya misitu ivunwe hovyo bila ya kuujali uharibifu unaotokea.

 

Mtaalamu yeyote wa misitu anastahili kuona fahari misitu inapostawi vizuri. Kinyume cha hapo ni kuisaliti taaluma aliyoisomea. Kusema kweli wengi wetu tumeisaliti taaluma ya misitu kwa kutenda kinyume cha maadili ya taaluma ya misitu. Kwa kupokea hongo na kushirikiana na wezi wa mazao ya misitu ni usaliti wa hali ya juu sana.

 

Tunalia na mishahara haitoshelezi mahitaji yetu, lakini ukiangalia kwa umakini baadhi yetu tunasababisha mishahara iwe midogo kutokana na tamaa zetu. Uamuzi tunaoufanya unasababisha Serikali ipate fedha kidogo na hivyo kuwa na uwezo mdogo sana wa kuendesha shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kuwalipa watumishi wake mishahara midogo.

 

Ukosefu wa usimamizi wa kutosha umesababisha misitu kama ya Kazimzumbwi na Pugu iliyo karibu na Makao Makuu ya Idara/TFS (kilometa 25 tu), ivamiwe na watu wenye uchu wa viwanja vya kujenga nyumba. Wengi ni waliohamia Dar es Salaam wakitoka bara, na baadhi yao wanaongezewa kiburi kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa wa ngazi za juu.

 

Hivi karibuni vibanda vilivyokuwa vimejengwa kwa ajili ya walinzi wa misitu ya Kazimzumbwi na Pugu vimevunjwa na watu wasiojulikana, pia maeneo mengine kuyachoma moto na polisi katika Wilaya ya Kisarawe hawako tayari kusaidiana na wataalamu wachache waliopo kuweza kudhibiti hali hiyo. Kwa nini? Kwa sababu utashi wa kisiasa wa uhifadhi misitu ya asili si mzuri sana.

 

Misitu si sekta muhimu kama ilivyo sekta nyingine kama maji, elimu, afya au kilimo. Watu wanafurahi kuona nyumba nyingi zinajengwa kila mahali katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kuliko kuiona rangi ya kijani. Kuwapo na rangi ya kijani ya kutosha katika mazingira tuishimo ni dalili za kuwapo uhai. Misitu ni uhai na tunapoiangamiza bila huruma tunajitangazia kiama chetu wenyewe kwa kujua au kutojua.

 

Kasi ya kutoweka misitu nchini ni takribani hekta zipatazo laki tano kwa mwaka. Hapa suala la kilimo kisicho endelevu linachangia sana kutoweka kwa misitu ya asili. Kilimo chetu bado ni duni na hivyo kusababisha uharibifu wa ardhi (land degradation).

 

Mbolea inapotea haraka hivyo mavuno yanakuwa hafifu na kusababisha wakulima kuvamia misitu ya asili wakitafuta sehemu zenye rutuba. Vilevile uchomaji mkaa ni balaa kubwa sana kwa uhai wa rasilimali misitu. Mahitaji ya mkaa mijini ni makubwa sana, yaani, zaidi ya tani milioni moja kwa mwaka na njia ya kutengeneza mkaa ni ya kiwango cha chini na haribifu sana kwa miti. Mfano, tani moja ya mkaa inatumia zaidi ya tani kumi za miti ambayo inachukua miaka mingi kufikia kiwango cha kukatwa (miaka zaidi ya 40).

 

Ili kupata tani milioni moja ya mkaa, zaidi ya tani milioni 10 za miti zinahitajika. Hiki ni kiasi kikubwa cha miti. Takwimu za Benki ya Dunia (2009) zinaonesha kuwa biashara ya mkaa nchini ni takribani dola milioni 650 za Marekani kwa mwaka, na nusu ya hiyo inafanyika katika Jiji la Dar es Salaam pekee (dola milionu 350).

 

Kusema kweli biashara hii inaangamiza misitu ya asili kwa kasi kubwa. Kukosa nishati mbadala ya kupikia ndiyo sababu kubwa na pia gharama kubwa za nishati mbadala kama Liquified Petroleum Gas (LPG), umeme na gesi asilia kutokana na kipato kidogo kwa Watanzania walio wengi, ndiyo baadhi ya changamoto kwa ongezeko la matumizi ya mkaa, hivyo kufanya watu wengi wajihusishe na biashara ya mkaa. Je, tufanye nini kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa?

 

Itaendelea

Mwandishi wa makala haya, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia, yaani Committee on Forestry-COFO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO). Ni Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Alistaafu Desemba 2012.

2574 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!