Jumatano ya wiki iliyopita, Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, alitaja kikosi cha wachezaji 26 kitakachoingia kambini kujiandaa na mechi dhidi ya Kenya pamoja na ile

ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) nchini Gabon, ambao watacheza dhidi ya Misri mwanzoni mwa Juni mwaka huu.

Katika kikosi hicho, Mkwassa amemjumuisha nahodha wa zamani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, licha ya awali kutangaza kujiuzulu kuchezea timu hiyo ya Taifa.

Cannavaro ameitwa kuziba pengo la Kelvin Yondani, ambaye anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano na hivyo kuikosa mechi dhidi ya Misri Juni 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi hicho cha Stars kimeingia kambini jana Jumatatu, Mei 23 kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Kenya utakaopigwa Mei 29 jijini Nairobi.

Taifa Stars inaingia kambini mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imefikia tamati Mei 22 mwaka huu kwa kupigwa michezo mbali mbali.

Baada ya kucheza mchezo huo wa Mei 29, Stars itarejea Dar kwa kuanza kukamilisha maandalizi ya kuwavaa ‘Mafarao’ wa Misri katika mchezo ambao Stars inahitaji ushindi wa angalau wa mabao matatu ili kuweka hai matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Gabon mwakani.

Katika kikosi hicho ambacho Mkwasa amekiita wiki iliyopita, pia amemwita chipukizi Hassan Kabunda ambaye anayechezea Mwadui FC ya Shinyanga, baada ya kuonesha kiwango cha hali juu kwenye mechi za Ligi Kuu Bara siku za hivi karibuni.

Mkwasa pia amemwita Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons ya Mbeya, mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa Coastal Union ya Tanga, Juma Mgunda; na Juma Mahadhi wa Coastal Union, mjukuu wa kipa wa zamani wa Simba, Omar Mahadhi ‘Bin Jabir’(sasa marehemu).

Mkwasa amemrejesha kikosini kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ na kumtema Ally Mustafa ‘Barthez’, wote wa Yanga.

Kikosi kamili alichotaja Mkwasa Jumatano iliyopita kinaundwa na makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga SC), Aishi Manula (Azam FC), Beno Kakolanya (Prisons FC). Mabeki; Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam FC), Erasto Nyoni (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Juma Abdul (Yanga SC), Mwinyi Hajji Mngwali (Yanga SC), Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC) na Andrew Vicent (Mtibwa Sugar).

Viungo; Himid Mao (Azam FC), Mohamed Ibrahim (Mtibwa Sugar), Shizza Kichuya (Mtibwa Sugar), Jonas Mkude (Simba SC), Ismail Issa Juma

(JKU), Mwinyi Kazimoto (Simba SC), Farid Mussa (Azam FC), Juma Mahadhi (Coastal Union) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).

Washambuliaji; Thomas Ulimwengu (TP Mazembe-DRC), Mbwana Samatta (KRC Genk-Ubelgiji), Elias Maguli (Stand United), Ibrahim Hajib (Simba SC), John Bocco (Azam FC), Deus Kaseke (Yanga SC) na Jeremiah Juma (Prisons).

Kikosi hicho kilichoitwa na Mkwasa hakina tofauti kubwa na timu ambazo zimekuwa zikiitwa katika michezo iliyopita, ambayo imekuwa ikifanya vizuri.

Kimsingi, kwa sasa Stars haina cha kupoteza kwa vile katika kundi lao mbio za kufuzu fainali za mataifa zimesalia kwa Tanzania na Misri, kutokana na Nigeria kutokuwa na nafasi tena ya kufuzu baada ya Chad kujiondoa mashindanoni na kupokonywa pointi zote.

Ukiangalia katika msimamo wa kundi G, Misri inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi saba, ikifuatiwa na Nigeria ambao wana pointi mbili huku Taifa Stars ikiwa na moja.

Lakini Stars ina faida ya kuweza kuzifikia pointi za Misri kutokana na kubakisha michezo miwili, tofauti na wenzake ambao wamebakisha mechi moja moja.

Ila, kitu kinacholeta faraja kwa Watanzania ni kuwa wote wamebakisha mechi dhidi ya Taifa Stars maana itacheza na Misri halafu itakuja kumenyana tena na Nigeria.

Hivyo basi, ni wao wenyewe Stars kuzichanga vema karata zao kwa michezo hii miwili iliyosalia, ili iweze kutimiza ndoto ya miongo kadhaa ya kutofuzu fainali za mataifa hapa Afrika.

Umaana wa Stars kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika utakamilika ama kuleta hamasa ya kutimiza ndoto zetu za ‘kusadikika’ katika mioyo yetu endapo tutaweza kumfunga Mmisri mabao zaidi ya matatu hapa nyumbani.

Katika mchezo huo, tunahitajika kutumia nini maana ya kucheza uwanja wa nyumbani kwa kuwatungua ‘Mafarao’ wa Misri idadi kubwa ya mabao hapa nchini.

Tuna kazi kubwa kweli, hakuna asiyefahamu maana ukitazama kikosi cha Misri si cha kubeza, na kinahitaji kupata matokeo ili iweze kutangaza kufuzu kwenye ardhi yetu kutoka kundi G.

Ila nina imani kila kitu kinawezekana katika soka – tunaweza kuifunga Misri nyumbani na kupata matokeo chanya nchini Nigeria dhidi ya ‘Super Eagles’.

Lakini hayo yote yanahitajika kuwa na nguvu za kutosha na wala si kuitelekeza timu na kuiachia Shirikisho la Mpira wa Miguu hapa Tanzania (TFF) lihangaike peke yake katika suala hili la utaifa.

Muda huu ndiyo mwafaka kwa Serikali kupitia wizara husika ya Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo chini ya Waziri Nape Nnauye kutoa sapoti ya kutosha kwa kikosi cha Stars.

Nina imani, Stars inaweza kutimiza ndoto za Tanzania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) nchini Gabon kama tukiendelea kuuthamini utaifa wetu.

1382 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!