Mitego kwa makocha wageni 2019/2020

Msimu mpya wa Ligi Kuu Bara umeanza hivi karibuni kwenye viwanja mbalimbali huku ukiwa na mvuto wa aina yake.

Ndiyo msimu wa mwisho wenye timu 20, kwani kwa mujibu wa waandaaji, kuanzia msimu ujao timu hizo zitapungua kwa matakwa ya wadhamini.

Msimu huu umeanza kwa matukio ya kushtua kwa vigogo wote watatu; ambapo Azam FC iliishinda timu ya Manispaa ya Kinondoni KMC, lakini Yanga ya Mfaransa Mwinyi Zahera iliangukia pua mbele ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa wakati Simba ikiwakung’uta JKT Tanzania.

Lakini msimu wa 2019/20 una mitego kadhaa kwa makocha raia wa kigeni hususan walioko kwenye klabu nne za Dar es Salaam; yaani Yanga, Simba, Azam na KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni.

Msimu huu huenda wakakumbana na majaribu makubwa ya kutakiwa kuthibitisha uhalali wa kile kilichowaleta nchini au kinachoingia kwenye akaunti zao za benki.

Patrick Aussems

Ni Kocha wa Simba, raia wa Ubelgiji. Msimu uliopita aliipa ubingwa timu hiyo na kuifikisha kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tayari ameshafeli mtihani mmoja baada ya timu yake kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, tena katika hatua za awali, ikiwa mbele ya mashabiki wake ndani ya Uwanja wa Taifa.

Ingawa huenda kibarua chake kikawa matatani kwa sasa, lakini bado ana mitihani ya kubeba makombe yote matano yaliyoko mbele yake – kuanzia ligi, Sportpesa, Kagame, FA na Mapinduzi.

Nyuma yake kuna wachezaji raia wa Brazil, Sudan, Zambia na DR Congo ambao hakuna lugha rahisi za kuwajengea heshima ndani ya Simba zaidi ya makombe matano.

Ni msimu ambao Simba imesajili wachezaji ghali zaidi kutoka nje ya nchi kwa lengo la kujitofautisha na timu nyingine za Bara, hususan watani wao Yanga.

Hivyo presha kubwa kutoka kwa uongozi, wanachama na mashabiki ni kuona wakifanya kitu cha tofauti, kuanzia kwenye ubora wa soka mpaka mafanikio ya kabatini ambayo ni vikombe.

 

Mwinyi Zahera

 Huyu ni Mkongomani aliyebadili uraia na kuwa Mfaransa. Msimu uliopita alisingizia kwamba timu yake haikuwa na usajili mzuri wala fedha ndiyo maana ilishindwa kubeba kombe lolote.

Msimu huu alipewa fedha na nafasi ya kuratibu usajili wake wote. Amenunua wageni kutoka Ghana, Namibia, Kenya, Rwanda na DR Congo. Ameanza ligi kwa kipigo dhidi ya Ruvu Shooting lakini hata kiwango cha wachezaji wake hususan kwenye fowadi mashabiki hawajavutiwa nacho, bado wameendelea kuwa wavumilivu wakisubiri maajabu.

Zahera ana mtihani wa kukisuka kikosi hicho kicheze kitimu na kufanya vizuri kimataifa pamoja na kwenye makombe matano ya ndani. Hakuna sababu yoyote anayoweza kuitoa msimu huu mashabiki au uongozi umuelewe.

Kama akifanikiwa kuitoa Zesco ya Zambia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanikiwa kupenya kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakuwa ni bonasi kwake, kwani mashindano hayo hayako kwenye vipaumbele alivyopewa mwanzoni mwa msimu na msomi Mshindo Msola.

Etiene Ndayiragije

Mafanikio yake akiwa na Mbao FC ya Mwanza na KMC yamewashawishi Azam FC kumpa mkataba. Yeye ni raia wa Burundi ambaye amepewa pia nafasi ya kukaimu ukocha wa Taifa Stars.

 Ana mtihani wa kutumia ujuzi wa wageni kutoka Ghana, Zambia na Uganda kuleta kitu tofauti Azam FC msimu huu.

Mrundi huyo ana mtihani wa kujitofautisha na watangulizi wake katika Uwanja wa Chamazi.

Ukiachana na makombe matano ya ndani, mtego wa Ndayiragije upo kwenye Shirikisho. Ni miongoni mwa makocha wenye presha kubwa ya kukabiliana na wakongwe Simba na Yanga kwenye ligi ya ndani na kuvunja utawala wao na kubeba kombe.

Jackson Mayanja

Amepewa kaa la moto KMC. Msimu uliopita timu hiyo ilifanya vizuri kwenye ligi ya ndani ikiwa chini ya Ndayiragije.

Mtihani wa Mayanja, kocha kutoka Uganda msimu huu ni kuvuka au kurudia mafanikio hayo ingawa tayari ameshatolewa kwa aibu kwenye Kombe la Shirikisho.

Bado mashabiki hawavutiwi na kiwango cha timu hiyo, lakini amekuwa akisisitiza kwamba mambo mazuri yanakuja ingawa wachambuzi wa soka wanatabiri anguko la timu hiyo msimu huu.

Ligi yenyewe

Msimu huu unaonekana kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi ya timu mbalimbali hususan kwenye usajili na miundombinu.

Timu nyingi zimefanya usajili mzuri wenye mseto wa wachezaji wazawa hususan chipukizi. Ujio wa udhamini wa Vodacom umesaidia kuongeza morali kwa timu nyingi kupata uhakika wa fedha za maandalizi na kukidhi gharama mbalimbali, tofauti na msimu uliopita.

 Mtego upo kwa bodi ya ligi ambayo msimu uliopita ilipunguza ladha ya ushindani kutokana na viporo na kupangua ratiba mara nyingi.

Msimu huu wamesisitiza kuongeza umakini na kuondoa upungufu wa msimu uliopita.