Mjasiriamali na nguvu ya fedha

Katika maisha yangu, ninaamini na kusimamia mambo makubwa matatu – ujenzi wa roho, ujenzi wa familia na ustawi wa kiuchumi. Naamini kuwa mafanikio ya kweli katika nyanja zote za maisha lazima yaanzie rohoni mwa mtu.

Kwamba ninaamini ustawi wa roho yangu ni kuwa na uhusiano mzuri wa kudumu na nguvu kuu ya uumbaji (nguvu hii naamini kuwa ni Mungu aliyemtuma Yesu Kristo duniani). Baada ya roho yangu kuendelea kuimarika ninatambua kuwa lazima niwe na uhusiano mzuri wa kudumu kwa familia yangu (mke na watoto wangu, ndugu zangu na jamii nzima).

 

Wakati naendelea kujenga familia yangu naamini kuwa lazima niweke nguvu na akili ya kutosha katika kustawisha uchumi wangu niweze kufanikisha upelekeaji mbele wa kazi za Mungu (zinazojenga roho za wengine), niweze kusaidia familia yangu kwa sasa hadi kizazi cha wajukuu zangu na niweze kuigusa jamii yangu kwa upana wake kwa kusaidia wengine kuboresha maisha yao kwa jumla. Nafahamu binadamu tunatofautiana katika kuchagua. Huenda mwingine asiwe na hata moja kati ya mambo ninayoamini mimi.

 

Ni sawa! Ni sahihi! Kwa sababu kila binadamu ana kusudi lake la kuwapo duniani ambapo kusudi huamua matakwa ya mtu, ndoto zake, vipaumbele vyake, tabia yake, mawazo yake na namna anavyoendesha maisha yake na kugusa maisha ya wengine. Pengine hasara kubwa anayoweza kuwa nayo mtu duniani ni ikiwa hajatambua kwa usahihi kusudi lake la kuwepo duniani. Kutokutambua kusudi la kuwapo duniani ni sawa na msafiri asiyejua anapoenda; anaweza kupanda gari lolote linaloenda kokote, anaweza kuahirisha safari wakati wowote na anaweza kushuka popote  wakati wowote.


Hata hivyo, wajasiriamali wote tunakutana kwenye kipaumbele cha uchumi. Iwe unajua kusudi lako ama hujui kama wewe ni mjasiriamali ‘miundombinu’ ya kiuchumi huikwepi. Katika pilikapilika hizi za uchumi ukweli ni kuwa tunahangaika kusaka fedha ama wengine wanaita mshiko, noti, mapene, mkwanja, kisu, ngawira, sabuni ya roho, na kadhalika.

 

Fedha inapomjia mtu huwa inaambatana na nguvu fulani kubwa yenye chembechembe za ‘umiliki’. Ni vema tukafahamu kuwa duniani kuna nguvu nyingi lakini ya fedha na ya mamlaka zinatawala nguvu nyingine kwa sehemu kubwa.


Nguvu ya fedha na ya mamla zinaingiliana na kutegemeana ijapokuwa kuna sehemu zinaachana. Mathalani, mtu anaweza kuwa na mamlaka lakini asiwe na fedha lakini kila mwenye fedha ana mamlaka (hata kama si rasmi, na ndivyo huwa mara nyingi).


Kwamba nguvu ya fedha haitafutwi, isipokuwa humjia mtu ‘automatically’ kwa kadiri fedha zinavyoongezeka. Nimekuwa nikichambua kitaalamu na kiuzoefu mbinu, mikakati na fursa za watu kuboresha uchumi wao (kupata fedha). Lakini nimeona ni busara tusaidiane kufunga vidhibiti mwendo dhidi ya nguvu inayoambatana na fedha.

 

Utakuwa ni msiba mkubwa (na nitahesabu kushindwa) ikiwa mikakati, fursa na mbinu ninazowapa watu kupata fedha, zikaishia kwa watu hao kupata fedha zitakazowaangamiza. Usipoifahamu nguvu ya fedha na usipojihami kuimudu; lazima itakuangamiza!


Unapokuwa na fedha kuna mambo makubwa mawili hutokea. Unakuwa na nguvu ya utiisho  na mvuto mkubwa. Katika kipengele hiki ndipo hasa hutokea mamlaka. Kutokana na utiisho huo kila unachosema watu wanakitii, kila unakowatuma wanakwenda na kila unachoagiza kinafanyika. Kutokana na mambo hayo ni rahisi mjasiriamali kujisahau na kudhani kuwa kila muda upo sahihi.


Unapokuwa na fedha unakuwa kama umejipaka gundi iliyochanganyika na sumaku. Utajikuta unawavuta watu wengi wa kila aina kuja kwako. Wanaokuwa karibu nawe watakuganda na watanasa kwako muda wote. Kwa kuwa unawavuta watu wa kila aina kuja kwako; mara nyingi unawavuta hata maadui.


Kazi kubwa ya maadui hawa ambao mara nyingi huanza kama marafiki; ni kuhakikisha unachafuka, unabomoka ama unaanguka. Kwa kadiri fedha inavyoongezeka ndivyo pia na maadui wanavyoongezeka. Hili lisikusumbue nitalichambua katika makala ya ‘Mjasiriamali na kigoda cha utajiri’ wiki chache zijazo.


Nguvu ya fedha inapumbaza sana kwa sababu pia huambatana na manukato ya utakaso. Ukiwa na pesa unaonekana ‘handsome’ hata kama sura na mwonekano wako hautofautiani na ngedere. Utakaso huu huwa unawaliza wajasiriamali wengi katika maisha yao. Kikawaida manukato haya ya utakaso (ambayo yapo kwenye nguvu ya mvuto) huja katika umbo la mapenzi.

 

Kadiri fedha inavyoongezeka ndivyo unavyozidi kuvutia kimapenzi kwa wanawake wengi. Sote tu mashahidi kuwa wajasiriamali wengi husaliti ndoa zao kwa kujihusisha na vimada mara tu mambo yanapowanyookea kiuchumi.


Mwanzoni utakuta mjasiriamali anasota kutafuta fedha na mke wake wa ndoa lakini zikishawajia anaanza kuhangaika na vimada wa nje. Kiukweli wengi huwa hawajitumbukizi katika mtego huu kwa makusudi ila inawatokea bila kujitambua. Tunajifunza hata kutoka kwa Mfalme Suleman, Daudi, Samson na wengine wengi katika Biblia


Ndiyo maana nilianza na mambo matatu ninayoamini nikiwa nimetanguliza ujenzi wa roho kama msingi wa kupata mafanikio mengine. Kwenye ujenzi huu wa roho ni kwamba unakuwa na uhusiano na Mungu, unakuwa na mfumo sahihi wa kufikiria, unakuwa na utamaduni bora wa kiuamuzi na kubwa katika yote unakuwa na malengo unayoweza kuyasimamia na kuyapigania.

 

Mara zote ukipata fedha kubwa kuliko maono (malengo) yako ni lazima itakusumbua. Hili unaweza kulipima hata mitaani kwetu. Kuna mtu anaweza kuwa na vilaki viwili tu lakini akasumbua mtaa mzima anaweza kupita baa hadi baa akifanya kufuru. Na wakati huo huo jirani yake anaweza kuwa na milioni kumi lakini ametulia.


Tatizo lililopo hapo ni utofauti wa malengo na maono yao. Yule wa laki mbili huenda amebabatiza fedha hiyo pasipo kuwa na malengo nayo, lakini huyu mwenye milioni kumi huenda ana malengo ya kujenga nyumba kwa maana hiyo hakuna hela anayoweza kuchezea.

 

Maadam tunaendelea kuzisaka fedha, nguvu na usumbufu unaoambatana na fedha hautakoma kutuandama, lakini mjasiriamali unatakiwa kuwa na mfumo sahihi wa kimaisha kupambana nazo. Ili uweze kuhimili mikikimikiki ya nguvu ya fedha ni lazima uwe na malengo unayoyaheshimu na unayoweza kuyasimamia.


Kwenye malengo yako lazima utangulie kumuweka Mungu kwanza, ufuate maslahi ya kifamilia; ndipo Mungu na familia yako wakuunge mkono katika harakati za kiuchumi (ujasiriamali wako). Wale wajasiriamali wenye utamaduni wa kuwaficha wake zao mipango yao ninawatahadharisha kuwa nguvu ya fedha itawamaliza. Isipowapata kiafya itatafuna furaha yao, isipotafuna furaha yao itawapenyezea kuyeyuka kwa upendo katika familia.


Imani yangu kuhusu ustawi wa kiroho naamini inasaidia kukuweka kwenye mstari wa kimaadili wakati wote. Kwanza huwezi kupunguza upendo kwa mke wako wakati wote iwe fedha imeongezeka ama mmepita katika upungufu. Kutokana na upendo huo (unaowezeshwa na nguvu za kiroho) ni sawa na ngamia kupenya tundu la sindano kwa wewe kumsaliti mke wako ama kuitelekeza familia yako kwa sababu ya kuogelea kwa vimada.


Shida nyingine inayoletwa na fedha ni kiu ya kuendelea kuongeza fedha kadiri unapopata fedha. Jambo hili mara zote hupelekea mjasiriamali kushindwa kusawazisha (kulinganisha) mambo. Akili inapokuwa kwenye fedha wakati wote ni rahisi kusahau mambo ya msingi kabisa.


Ndiyo maana si ajabu kumkuta mjasiriamali akijishughulisha sana na biashara zake kiasi kwamba anasahau kabisa kutenga hata muda wa kumwabudu Mungu walau mara moja kwa juma. Kwa kufanya hivi tayari mjasiriamali anakuwa amepuuza ujenzi wa roho yake.

Kwa kutumia muda mwingi kutafuta fedha, wajasiriamali wengi huwa wanasahau kutenga muda wa kukaa na familia (mke na watoto) na kuwaonesha upendo wao. Jambo hili ni hatari sana kwa sababu mwisho wa siku familia haitaona umaana wa mafanikio yako kiuchumi.


Wapo wake wa wajasiriamali ambao hufanya maombi rasmi kwa Mungu; ili waume zao wasifanikiwe katika miradi na biashara fulani kwa sababu biashara na miradi hiyo inawakosesha wasaa wa kufurahia mapenzi na upendo kutoka kwa waume zao. Sasa angalia, mjasiriamali unakazania kutafuta fedha, umemsahau Mungu na familia yako.

 

Mungu anakuchukia na familia inakuchukia! Kama unahangaika na fedha ambazo zinaharibu uhusiano wako na Mungu na zinavuruga mapenzi na upendo katika familia yako; nakuthibitishia kuwa hautafika popote na kama ukiwa na mafanikio katika eneo hilo la uchumi; hutaiona radha kamili ya mafanikio.

[email protected] 0719 127 901