Bendi ya MK Group ilikuwa maarufu kwenye miaka 1990, iliyokuwa imejikita kupiga muziki  katika hoteli za kitalii hapa nchini. Lakini kabla ya kuanzishwa kwake, kulikuwa na bendi ya mama, ya  African Stars iliyoanzishwa Julai 1, 1994, katika Hoteli ya  Bahari Beach Dar es Salaam.

Mmiliki wa bendi hiyo, Ali Baraka, baadaye akaanzisha bendi dada tatu za MK Group, MK Beat na MK Sound. Ali hakuiongoza kwa muda mrefu kwani baadaye aliachia uongozi kwa Msiilwa Baraka aliyekuwa Mwenyekiti na Asha Baraka akawa Mkurugenzi Mtendaji. Hii ilitokana na yeye kuwa na majukumu mengi kazini kwake katika  Shirika la Ndege la Zambia (Zambia Airways).

Wanamuziki Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’ akisaidiana na Mbombo wa Mbomboka, walikuwa waanzilishi wa bendi hiyo ya MK Group, iliyokuwa ikiporomosha muziki katika ghorofa ya Hoteli ya New Africa jijini.

Kasongo alikusanya wanamuziki mahiri kuunda kikosi cha mashambulizi dhidi ya bendi nyingine zilizokuwa zikitikisa jiji wakati huo. Zilikuwapo bendi za The Kilimanjaro Band ‘Wana Njeje’, Tatu Nane,

The Revolution na nyingine nyingi zilizokuwa zikipiga muziki katika hoteli nyingine.

Safu hiyo ilikuwa ni ya waimbaji mahiri — Kalala Mbwebwe, Paul Vitangi, Green Simutowe aliyekuwa akiimba nyimbo za Kizungu. Wengine ni mwanadada  Rahma Shaali na Clayton.

Bendi hiyo ilikuwa imesheheni magwiji wa kushika ‘mpini’ wa solo kwani walikuwapo akina Monga Stan, Kasongo Ilunga, Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ na Kawelee Mutimanwa. Omari Makuka alikuwa akipiga gitaa la kati (rhythm) na Andy Swebe alikuwa ikiliungurumisha gitaa zito la besi.

Kwenye midomo ya bata (saxophone) alikuwapo Mafumu Billari ‘Super Sax’ na tarumbeta zilipulizwa na Abdallah Tuba na Kayembe Ndalabuu ‘Trubloo.’ Kinanda alikuwa akibofya Asia Darwesh ‘Mama lao’ na upande wa tumba alikuwapo Sidy Morris ‘Tanzania One.’

Wakiwa na MK Group walitoka na nyimbo za Nikupe ukweli, Chako ni chako Kibera, Tukale Sangara na Nishike mkono. Nyingine zilikuwa Nipe ukweli, Kigeligeli, Kimasala, Dawa za kulevya, Maria Maria, Losa, Mwintope na nyingine nyingi zilizokuwa zikikonga nyoyo za wapenzi wa ‘Ngoma za maghorofani.’

Bendi hiyo ilijizolea sifa kubwa ambapo kila mwisho wa wiki wapenzi na washabiki wa bendi hiyo walisikika wakisema leo ‘Ngoma  maghorofani,’ ndiyo sababu ya bendi hiyo kupachikwa jina la ‘Ngoma za maghorofani’ kwa kuwa ilikuwa ikipiga muziki ghorofa ya pili ya Hoteli ya New Africa.

Ukumbi huo ulikuwa ukifurika wapenzi wa muziki huku wakipuliziwa na upepo mwanana kutoka kwenye viyoyozi vilivyokuwa ukumbini humo, wakicheza mtindo wa ‘Ngulupa.’

Aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo, Kasongo Mpinda ‘Clayton’, aliwahi kusimulia jinsi bendi ilivyopatwa na misukosuko baada ya mpiga gitaa Joseph Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’ wakati huo kuumwa. Naye Kawelee Mutimanwa alikuwa tayari  katimkia Ulaya na kuiacha MK Group ikikosa mpiga wa gita la solo.

Busara zilitumika kwa kumfuata Miraji Shakashia ‘Shakazulu’ ambaye wakati huo alikuwa ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mlimani, lakini alikuwa akifanya mazoezi ya kupiga gitaa la solo hapo MK. Group.

“Shakashia alikuwa bado mdogo kwa hiyo tulilazimika wakati mwingine kuchukua teksi, wakimtafuta alikokwenda kucheza na watoto wenzake, ili aje kupiga gita la solo…” alisema na kuongeza: “Kwa kusema ukweli wapenzi wa  ngoma za maghorofani walivumilia, wakimsubiri kwa saa kadhaa ili Shakashia aletwe kwa ajili ya kupiga gita hilo”.

Baada ya kumaliza mkataba wa kupiga muziki katika Hoteli hiyo ya New Africa, walikwenda Morogoro kupiga muziki katika Hoteli za Morogoro na Luna kwa mkataba.

Kasongo alieleza jinsi Miraji Shakashia ‘Shakazulu’ alivyookoa jahazi lililoekea kwenda mrama kwa kuweza kuzipiga nyimbo zote zilizokuwa zikicharazwa na Josepph Mulenga na Kawelee. Shakashia hivi sasa anatamba katika bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’. Baada ya mkataba wao wa kupiga muziki katika hoteli kubwa za kitalii kumalizika mjini Morogoro, walirudi jijini Dar es Salaam na kuwa Omega ya bendi hiyo.

Kifo cha MK Group hakikuwa cha upweke kwani hata bendi dada za MK Beat na MK Sound nazo zikayeyuka katika sura ya muziki ikiiacha bendi mama ya African Stars chini ya Kampuni ya ASET ikitamba hadi  sasa.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba:

0713331200, 0767331200 na 0784331200.

2721 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!