Siku chache zilizopita, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo; na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi wa TFS, Mohamed Kilongo, wametangaza mpango kamambe wa kuratibu biashara na matumizi ya mkaa nchini.

Taarifa ya wataalamu hao zinaonesha kuwa uharibifu wa misitu kutokana na matumizi ya mkaa ni hekta 372,000 kwa mwaka. Kiwango hiki ni sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye miti.

Uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za Taifa, unatajwa kuwa chanzo kikuu cha baa hili.

Viongozi hawa walizungumza mikakati mizito kwenye mkutano wao na waandishi wa habari, lakini ni bahati mbaya kuona kuwa vyombo vya habari, yakiwamo magazeti, hayakuzipa umuhimu unaostahili taarifa hizo.

Baada ya taarifa hiyo kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, kumejitokeza makundi mawili – moja likiunga mkono uamuzi huu wa Serikali, na jingine likipinga. Wanaopinga wanatoa mfano wa nchi ya Chad, ambako wakati fulani Serikali ilipiga marufuku biashara ya mkaa na kusababisha mtafaruku.

Tofauti na Chad, Serikali ya Tanzania haijapiga marufuku biashara na matumizi ya mkaa, isipokuwa inachotaka ni kuona uvunaji misitu unafanywa kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizotungwa. Serikali inataka watu wafanye biashara hiyo kwa njia halali na walipe ushuru na kodi kwa mujibu wa sheria.

Hii si mara ya kwanza kwa TFS kutoa msimamo wa aina hii. Mwaka jana ilitoa taarifa hii:

Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanatakiwa kutimiza masharti yafuatayo:

(i) Awe na hati ya usajili;

(ii) Awe na hati ya usafirishaji wa mazao ya misitu (Transit Pass);

(iii) Awe na leseni ya kuvuna mazao ya misitu;

(iv) Awe na leseni ya biashara ikiwa ni pamoja na TIN namba;

(v) Alipie ushuru wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kama ilivyobainishwa kisheria;

(vi) Awe na daftari la kumbukumbu ya kupokea na kuuza mazao ya misitu.

Kutokana na Kanuni za usafirishaji wa mazao ya misitu za mwaka 1999 hairuhusiwi mtu yeyote kusafirisha mazao ya misitu (kwa njia ya barabara au maji) kati ya saa kumi na mbili jioni na saa kumi na mbili asubuhi.

Atakayevunja masharti hayo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

 

Mkaa

Hairuhusiwi mtu yeyote kusafirisha mkaa hadi atimize masharti yaliyoko hapo juuu. Vilevile, mkaa, hata kama ni mfuko mmoja kwa ajili ya biashara au matumizi ya nyumbani, sharti ulipiwe.

Pamoja na kutimiza masharti yaliyoorodheshwa hapo juu, wafanyabiashara wa mkaa wanatakiwa kutimiza masharti yafuatayo:-

(i) Awe na leseni itakayotolewa na Afisa Misitu wa Wilaya au Wakala wa Huduma za Misitu;

(ii) Awe na hati ya kusafirisha mkaa (Transit Pass), ambayo itagongwa muhuri katika kila kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu.

(iii) Mkaa usafirishwe kupitia njia zilizoruhusiwa na Ofisi za Misitu.

(iv) Atatakiwa alipie ushuru wa Serikali kwa kila mfuko wa uzito wa kilogramu 28 kwa Sh 3,500 au kilogramu 56 kwa Sh 7,000.

Kwa mtu yeyote atakayesafirisha mkaa bila kutimiza masharti yaliyotajwa hapo juu, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Maelezo zaidi yanapatikana katika ofisi za Misitu za Wilaya na TFS.

Desemba 16, mwaka jana TFS ikatoa taarifa nyingine kwa umma iliyosomeka:

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inautaarifu umma kwa ujumla hususani wafanyabiashara na watumiaji wa mazao ya misitu kuzingatia yaliyomo kwenye, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 ambayo pia inatambulika kama Sheria ya Misitu Sura Namba 323 (RE: 2002), Kanuni na Miongozo inayoelekeza taratibu za uvunaji, usafirishaji na jinsi ya kufanya biashara ya mazao ya misitu. Sheria na Kanuni inaelekeza yafuatayo:

1. Kila mvunaji wa mazao ya misitu lazima awe na leseni halali ya uvunaji wa mazao ya misitu iliyotolewa na mamlaka husika. Aidha, kila gunia la mkaa lililobebwa na chombo chochote cha usafiri ni lazima liwe limekatiwa risiti halali ya malipo ya Serikali;

2. Kila msafirishaji wa mazao ya misitu lazima awe na kibali (Transit Pass – TP) cha kumruhusu kusafirisha mazao ya misitu ikionyesha mahali mazao hayo yalipotoka na yanapokwenda ikiambatishwa na leseni ya uvunaji;

3. Kila mfanyabiashara lazima awe amesajiliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuwa ni mfanyabiashara halali wa mazao ya misitu;

4. Usafirishaji wa mazao ya misitu ni kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni;

5. Ni marufuku kusafirisha mkaa kwa kutumia pikipiki zinazotumia matairi mawili

6. Biashara ya mkaa lazima ifanyike katika maeneo maalumu yaliyoainishwa katika kila wilaya;

7. Ni marufuku kwa wafanyabiashara ya mkaa kufanya biashara hiyo kandokando ya barabara;

8. Kwa wanunuzi wote wa mkaa kwa ajili ya matumizi ya kaya ni lazima wawe na risiti halali ya Serikali inayoonesha malipo yaliyofanyika kwa idadi ya magunia ya mkaa aliyonunua;

Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka utaratibu huu.

Ndugu zangu, faida za rasilimali misitu hazihitaji mtu kuwa na elimu ya uzamili au uzamivu. Wazee wetu licha ya kutokuwa na elimu hii ya kisasa, walitambua, waliheshimu na walilinda misitu.

Waliitunza misitu kwa kutumia mbinu mbalimbali. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuuaminisha umma kuwa kukata miti kwenye msitu fulani lilikuwa jambo la laana kwa kizazi cha familia yenye kutenda kosa hilo.

Kwa mfano, kijijini Butiama tuliaminishwa kuwa kukata mti au miti ndani ya Msitu wa Muhunda, ni kosa kubwa, na kwamba yule ambaye angepuuza amri hiyo, angepata laana ya kuzaa watoto walemavu!

Si hivyo tu, bali hadi leo kuna Wazanaki (Watyama) wanaoamini ndani ya msitu huo ndimo kwenye makazi ya ‘mungu’ wao aitwaye Muhunda.

Pamoja na Muhunda, kuna maeneo mengi ya misitu yaliyotunzwa na wazee. Watu waliruhusiwa kuokota kuni zilizotokana na miti iliyokufa kifo cha kawaida (kifo cha uzee). Utaratibu huu wa Wazanaki ndiyo huo huo unaopatikana katika makabila mengi nchini kote.

Licha ya wazee wetu kutokuwa na elimu kama hii ya kileo, bado waliweza kutambua faida za misitu katika mustakabali wa maisha yao ya kila siku. Walitambua kuwa kwenye misitu wanapata matunda, kuni, wanyama, ndege, vyanzo vya maji nk. Ni jambo la kusitikisha kuona leo, pamoja na elimu zetu, bado tuna watu wanaoshindwa, ama kwa makusudi, au kwa kutojua, kutambua umuhimu wa misitu kwa uhai wetu na viumbe wengine.

Ndugu zangu, matumizi ya mkaa nchini mwetu hayana tofauti na mauaji ya kukusudia. Tumeamua kuifanya Tanzania iwe nchi ya Watanzania wanaoishi leo, na si wa miaka mingi ijayo. Wazee wetu wangetenda dhambi hii inayotendwa sasa kwenye ukataji misitu, naamini tusingefaidi uhondo ambao baadhi yetu tumeufaidi.

Wale tuliopata muda wa kuishi vijijini, hata kama si kwa muda mrefu, tunakumbuka namna tulivyoburudishwa na mandhari ya kuvutia ya misitu yenye ndege na wanyama wa aina mbalimbali. Tulivutiwa na vipepeo wa rika na rangi za kila aina.

Asubuhi na mapema tulisindikizwa na wakubwa zetu mtoni kwenda kuoga kwa kuamini maji ya muda huo yaliyobubujika na kuleta raha yalikuwa yenye manufaa kwa siha zetu. Hatukuoga kwa kutumia bakuli au vikombe, bali kwa kujigaragaza katika mifereji iliyojaa maji.

Nyumbani kwetu hatukuwa na saa zilizotegeshwa kengele kwa ajili ya kutuamsha alfajiri, badala yake tuliamshwa na majogoo yaliyosaidiwa na sauti nzuri za ndege wa kila aina walioishi jirani na nyumba zetu.

Asubuhi wakati wa mawio, ndege walisafiri kutoka kwenye makazi yao katika maeneo oevu yenye majani mazuri – kwenda kusaka vyakula kilometa nyingi. Waliposhiba, walisubiri jioni wakarejea katika viota vyao ndani ya maeneo oevu yuasiyogushwa na binadamu.

Leo raha hii haipo. Imetoweka. Mhusika mkuu wa dhambi hii ni binadamu kupitia ukataji miti na uchomaji misitu. Tunapokata miti maana yake tunaondoa makazi ya ndege na wanyamapori. Tunaondoa vivuli vyenye kuhifadhi maji ambayo mwishowe ndiyo huungana kutengeneza vijito na mito.

Dunia tumeivua nguo na kuiacha ikiwa uchi! Ndiyo maana sasa inaponyesha mvua inakuwa shida maana maji yanatiririka bila breki. Linapowaka jua la wiki moja, ardhi yote inakuwa imeshakauka! Jua halipati kikwazo cha kulifanya lisiikaange ardhi.

Tumeharibu kote tunakoishi, na sasa, kwa ukaidi usio na kipimo, tumeamua kuvamia Hifadhi za Taifa, Mapori Tengefu, Mapori ya Akiba, Misitu ya Hifadhi na maeneo mengine ili kuendesha ujangili dhidi ya miti na wanyamapori. Hatuwezi kukwepa laana itokanayo na dhambi hii ya kuharibu mazingira. Kukomesha mauaji haya ya misitu, lazima tuwe na pa kuanzia. Tunapowapata kina Profesa Silayo na Kilongo, tunamshukuru na kumtukuza Mungu.

 

>>ITAENDELEA

3730 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!