Istilahi za taaluma yoyote zisipotumika kwa uangalifu na maarifa zinaweza kupoteza sifa na heshima ya taaluma. 

Yaani, wanataaluma wenyewe kudharauliana na kugombana. Na watu wengine katika jamii yao huwabeza, huwacheka na kuwaona hawafai.

Hapa nchini kwetu zipo taaluma mbalimbali. Mathalani sheria, ufundi, siasa, kilimo na kadha wa kadha. Taaluma hizi na nyinginezo zipo kumsaidia mtu kufanya kazi kwa ustadi na ufanisi ili aweze kupata mahitaji yake muhimu ya chakula, mavazi na malazi wakati wote wa maisha yake duniani.

Baadhi ya istilahi katika taaluma ya siasa ni demokrasia, haki, kanuni na udikteta. Ninakusudia kuziangalia istilahi hizi kwa sababu taaluma hii inamgusa kila Mtanzania katika mahitaji yake ya kila siku na katika burudani zake za hapa na pale.

Unaweza kusema istilahi kanuni na haki unazipata pia katika taaluma ya utawala na sheria. Ni kweli. Zenyewe ni mtambuka. Nia hapa ni kuangalia namna zinavyozungumzwa, zinavyotafsiriwa na zinavyotumiwa na wanasiasa, na zinavyopokewa na wanajamii.

Demokrasia ni mfumo wa utawala ambao mamlaka yake yanatokana na matakwa ya umma. Udikteta ni hali ya kutawala watu au nchi nyingine kimabavu. Haki ni stahili ya mtu kupata kwa kufuata taratibu zilizokubaliwa.

Kisiasa tunaweza kusema kanuni ni masharti yanayopaswa kufuatwa na kufanywa na mtu yeyote katika chama na serikali kila siku. Katika fasili sanifu kanuni ni desturi, mila na nguzo katika kutekeleza na kusimamia shughuli za chama cha siasa na za serikali iliyoko madarakani.

Kwa hivyo, demokrasia, udikteta, kanuni na haki ni istilahi nyeti katika uga wa siasa, utawala na serikali wakati wa kufanya uamuzi. Zitumike kwa hekima kukidhi matakwa ya taifa lolote ambalo linakusudia kujenga jamii iliyo sawa na huru katika kuleta maendeleo ya kweli ya kiuchumi na kijamii.

Wanasiasa, wadau wa siasa na watetezi wa haki wote wanatambua kwamba demokrasia si aina moja duniani. Zipo nyingi tofauti kutokana na matakwa ya umma. Kwa hiyo taifa fulani halina haki kuingilia demokrasia ya mambo ya ndani ya taifa jingine. Ni ukiukwaji wa haki kwa taifa hilo.

Mara kadhaa tumepata kushuhudia viongozi wa siasa na wa serikali wanavyokwaruzana katika kutekeleza kanuni za demokrasia, kama kuku na mwewe wanavyogombea kifaranga cha kuku. Mwewe anataka kutoa uhai wa kifaranga. Kuku anakinga na kulinda uhai wa kifaranga chake.

Mkwaruzano kama huu huchukua muda mrefu, na hasa wadau na watetezi wa haki wanapojiunga na kumsaidia mwewe kupora kifaranga apate kukila matumbo tu, na kuacha mzoga kuliwa na wadudu. Wadau na watetezi hao hawafikiri wala kuwaza ukatili wanaoufanya kwa  kifaranga na msiba utakaompata mama kuku.

Viongozi wa serikali wanapobaini hila kama hizo, huwaza na kutafuta mbinu za kukabiliana na matendo hayo. Hutumia mlango mwingine wa demokrasia na kufanya uamuzi. Serikali inatumia utawala wa mabavu kuhakikisha usaliti na dhuluma zinatoweka.

Utawala kama huu hupigiwa kelele na kutolewa lawama na wale wasaliti na wadhulumati. Wanapiga propaganda kuficha mambo yao kwa jamii. Bila haya wala woga huchongea taifa lao kwa mabeberu ili taifa lao liwekewe vikwazo vya kiuchumi kwa sababu lina minya kanuni za demokrasia.

Si kuminya demokrasia, wanatafuta uokovu kwa kile methali ya Kiswahili isemacho: “Mkuki humuua mhunzi,” imewaangukia na kuwabana mbavu. 

Wanalia na kulalama kwamba wanaonewa na kusahau chanzo chake ni wao kutumia vibaya istilahi, demokrasia, kanuni, haki na udikteta.

Nawaomba niwashauri Watanzania wenzangu tuwe macho na wanasiasa kama hawa. Tukumbuke mabaya uwatendeayo wengine yaweza kurudi na kukudhuru mwenyewe, ndiyo maana ya “Mkuki humuua mhunzi.”

By Jamhuri