Mimi si mkulima. Babu na baba yangu walikuwa wakulima. Kadhalika bibi na mama na hata leo baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki zangu kule kijijini kwetu ni wakulima. Ndiyo ajira yao kuu inayowapatia riziki, mavazi na makazi.

Wanasiasa na wanauchumi wanasema kilimo ni uti wa mgongo. Wakimaanisha ni kazi inayojenga, inayoimarisha na inayoendeleza utu wa mtu na uhai wake katika kufanya kazi halali duniani. Bila kilimo mtu huyu asingeweza kupata mahitaji yake ya msingi ya chakula, mavazi na makazi.

Kilimo si kazi rahisi wala fani ya kuchezea mwanasesere au baiskeli ya mti. Ni kazi yenye utaalamu, ujuzi na uzoefu katika kutambua mbinu za kilimo, taratibu zake, majira ya kilimo, aina ya mbegu na kilimo chenyewe kiweje.

Wakulima wanatambua, ili kupata mazao mengi na bora hapana budi kuwa na mbegu bora, ardhi yenye rutuba, majira ya kilimo. Aidha, kutambua wakati wa kupanda mbegu, wakati wa kupalilia mimea na wakati wa kupalilia. Mwisho hutambua wakati wa kuvuna na kuhamisha mazao shambani na kupeleka nyumbani au sokoni.

Wakulima ninaowafahamu mimi huwa wanafanya taratibu kama hizo na kupata mafanikio mazuri bila mashaka wala misukosuko. Iwe katika kilimo asili cha majira au cha umwagiliaji wakati wote au kiangazi. Kwa kweli hicho ni kipindi kigumu na chenye kazi nzito ya kupata mazao kwa mahitaji ya jamii.

Wakulima wanaofanya hivyo huonekana na kupewa sifa ya wakulima wazuri au bora au wakulima stadi. Ustadi wao katika kilimo hutusaidia mno sisi ambao si wakulima kwani mazao yao tunatengeneza bidhaa mbalimbali viwandani zikiwamo nguo na samani na nyingine kuchuuza mitaani kama vile mboga za majani na matunda.

Shibe tupatayo majumbani mwetu inatokana na wao wanapolima na kutupatia mazao ya chakula na ya biashara. Shibe yetu wafanyakazi, wafanyabiashara na wanasiasa haiwapi wao bughudha wala kiburi kwetu. Kwao muda wote ni upendo, furaha na amani.

Wafanyakazi, wafanyabiashara na wanasiasa ndiyo tuliojaa kiburi na dharau kwao, hata wakati mwingine kuwafanyia hiyana kwenye mazao yao wasiuze au kutowapa usafiri kwa visingizio kedekede. Karaha ni wakati wa maandalizi ya kilimo kwa kuficha au kuchelewesha zana za kilimo na pembejeo.

Mara kadhaa tumesikia pembejeo hazijapelekwa mkoa fulani. Hakuna magari ya kusomba mazao kutoka shambani kwenda sokoni. Mazao kuibwa kwa hila za stakabadhi ghalani au mazao kuchomwa moto shambani na gulioni.

Yote hayo na mengineyo mengi anafanyiwa mkulima. Lini mkulima wa nchi hii atashukuru na kutembea kifua mbele macho mita mia moja kama mfanyabiashara? Lini mkulima ataserebuka kama mfanyakazi kwenye mabenki na majumba ya maana? Lini mkulima atabembea kwenye magari ya fahari kama wanasiasa kwenye barabara na mikutano?

Naamini mkulima anaweza kuwa mkulima mkubwa, bora na stadi. Anaweza kumiliki zana bora za kilimo na za kisasa. Anaweza kulima kitaalamu. Anaweza kusafirisha mazao yake bila kuonewa na kunyanyaswa na anaweza kupanga bei ya mazao yake bila kuingiliwa endapo sisi tusio wakulima tutaacha choyo.

Hayo yatawezekana iwapo wafanyakazi watawajali na kuwashughulikia wakulima katika mahitaji na stadi zao wakati wa maandalizi ya kilimo. Wakulima wataweza kuboresha maisha yao na wengi watakuwa mastadi wa kilimo na uchumi wa nchi utakua maradufu ya sasa.

Wafanyabiashara wakiacha ulaghai na ujanja katika ununuzi wa mazao na kulipa bei halali iliyopangwa na wakulima; na kutambua mkulima ni uti wa maisha ya mtu, ukweli watamwinua mkulima na kupunguza mwanya wa walionacho na wasionacho.

Wanasiasa wakiwa wakweli katika kauli zao vijijini na majukwaani na kuwaelekeza vyema siasa ya kilimo; yamkini wakulima watajivua joho la umaskini. Lakini wanasiasa hao wakiendelea na bla bla zao mikutanoni na maofisini kugombea madaraka na kujenga historia ya ubabe wao, kamwe wakulima hawatakuwa uti wa maisha ya wananchi.

Wafanyakazi, wafanyabiashara na wanasiasa tuache danadana za kisiasa na uchepe wa mitaani katika kuwavusha wakulima kwenye mto wa umaskini. Inawezekana tutimize wajibu wetu.

1132 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!