Timu ya Mkuranga African maarufu kama Apollo imeibuka kidedea katika mashindano maalumu ya kutafuta timu itakayoshiriki Ligi Daraja la Nne ngazi ya wilaya.

Apollo ilifanikiwa kupata nafasi hiyo baada ya kuinyuka Mwalu City 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa katika uwanja wa Mkuranga.

Mkuranga African ilijipatia bao hilo la pekee katika dakika ya 30 ya mchezo. Timu hiyo ilitinga fainali baada ya mpinzani wake katika nusu fainali, Amazon, kushindwa kutokea uwanjani.

Kabla ya hapo, Mkuranga African iliibugiza Smart Boys ya Kimanzichana magoli 6-2.

Kocha wa timu hiyo, Fimbo Abdul, amewashukuru wachezaji wake kwa kujituma na kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya Ligi Daraja la Nne ngazi ya wilaya na Ligi Daraja la Tatu ngazi ya mkoa.

Fimbo amesema kuwa baada ya kuipata nafasi hiyo, kwa kuwa wataiwakilisha wilaya, basi anapanga kuzishirikisha klabu katika kata mbalimbali wakati wa kuiandaa timu yake.

Amesema lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kushinda katika kila hatua ili hatimaye timu yao ipate nafasi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza na hatimaye Ligi Kuu.

Hata hivyo, ameziomba kampuni mbalimbali kujitokeza kuzidhamini timu za wilaya hiyo ili zifanye vizuri katika mashindano mbalimbali.

Amesema kukosekana kwa wadhamini na viwanja vizuri vya michezo ni changamoto kubwa zinazorudisha nyuma maendeleo ya michezo wilayani humo.

Ameongeza kuwa kama wadhamini wakijitokeza kwa wingi kudhamini ligi hiyo na kusaidia kuinua klabu ndogo, itainua hali ya michezo hasa kwa vijana.

Amesisitiza kuwa wilaya hiyo ina fursa kubwa ya uwekezaji hasa katika kada ya viwanja vya michezo.

Amelitaja eneo jingine ambalo mtu au taasisi inaweza kuwekeza na kupata faida ni uanzishwaji wa shule za michezo (academy), kwani kuna vijana na waoto wengi wenye vipaji vya michezo lakini wanakosa fursa ya kuviendeleza.

By Jamhuri