Katika Gazeti la Raia Mwema la Februari 20-26, 2013, kuna makala yenye kichwa cha habari kisemacho “Mkuu wa Usalama wa Taifa Ang’oke”.

Mwandishi wa makala hayo ameelezea matatizo mengi yanayosababishwa au yanayosimamiwa na kitengo cha usalama wa taifa, kwa lengo la kuuhujumu umma na kulinda maslahi ya watawala na ya wanakitengo wenyewe.

 

Ningependa na mimi nichangie mada hii kama muhanga wa kitengo kwa miaka mingi sasa. Kabla sijaanza kuchambua shughuli za kitengo chetu hiki ambacho kina jina lisilofanana na shughuli wanazozifanya, ningependa kwanza nirudi nyuma nikumbuke kitengo hiki kilitokea wapi?

 

Kitengo chetu cha Usalama wa Taifa kiliundwa enzi za ukomunisti kwa kuiga muundo na taratibu zote za kitengo cha kigaidi na ujasusi cha Urusi ya zamani, ambacho kilikuwa kinajulikana kama “Komitet Gasudastiveny Bezopasnost (KGB)”. Kule Urusi hadi leo hii kuna watu ambao ukilitaja jina la KGB wanatokwa na machozi, hasa wakikumbuka mateso na dhuluma waliyofanyiwa na kitengo hicho wakati chama cha kikomunisti kipo madarakani.


Kitengo cha kigaidi na kijasusi cha Urusi – KGB, kilivunjwa mara tu baada ya kuvunjika kwa siasa za kikomunisti mwaka 1991, na serikali mpya ya Russia Federation iliitisha mdahalo wa kitaifa kukijadili chama cha kikomunisti na kitengo hicho, ambapo mbele ya runinga ya taifa madhambi yote yaliyofanywa na KGB dhidi ya raia wasiokuwa na hatia na hujuma zote zilizofanywa dhidi ya nchi, ziliwekwa wazi na wahanga walilipwa fidia na kuombwa radhi.

 

Vitengo vya usalama wa taifa vipo kila nchi na shughuli za vitengo hivi zinategemeana na mfumo wa utawala wa nchi husika. Kwenye nchi za demokrasia na utawala wa sheria, vitengo vyao vya  usalama wa taifa huwa vipo kwa ajili ya kulinda maslahi ya taifa ndani na nje ya nchi husika.


Lakini vitengo vya nchi ambazo hazina utawala wa sheria na demokrasia ya kweli, kitengo cha usalama wa taifa madhumuni yake makubwa ni kulinda maslahi ya watawala na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa serikali, na kuwadhibiti wanaoonekana kuweka mazingira magumu kwa watawala na viongozi wa ngazi ya juu wa serikali kufanya mambo mbalimbali.

 

Madhumuni ya kuwa na kitengo cha Usalama wa Taifa kwa uelewa wa wananchi wa Tanzania (walipa kodi) ni kama ifuatavyo:

 

(1) Ni kulinda maslahi ya taifa: kupambana na uhalifu mbalimbali; kulinda rasilimali zetu; kulinda na kutetea maslahi ya jamii; kukemea maovu katika jamii;

 

(2) Kuchunguza na kudadisi mafanikio ya kiuchumi na maendeleo kwa nchi za nje: kuleta habari ambazo zinaweza kuisaidia nchi yetu kupata manufaa ya kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia na kimaendeleo kwa ujumla;

 

(3) Kuweza kuwachagua watu wanaoweza kuwa viongozi katika jamii: kuijulisha Serikali mtu anayeonekana anaweza kutoa mchango mkubwa kwa jamii – kimawazo, kielimu, kimaarifa na hata kiuongozi;

 

(4) Kuwatambua watu wanaoweza kuhatarisha usalama wa raia na jamii kwa ujumla  kama vile majambazi; wauza na wala unga; wahaini; wabadhirifu wa mali za umma; mafisadi; watoa na wapokea rushwa; wahujumu uchumi; magaidi; na uhalifu wa kupangwa (mafia).

 

Madhumuni ya kuwa na kitengo cha usalama wa taifa kwa uelewa wa watawala wa kikomunist (kijamaa) na wanakitengo wenyewe kama vile Tanzania na kitengo chake cha hivi sasa ni pamoja na:


(1) Kumlinda rais na familia yake aendelee kutumikia wadhifa huo;

(2) Kumjengea rais umaarufu wakati wote na kuhakikisha kwamba anakubalika kila sehemu;

(3) Kulinda siri za rais na watawala wenzake zisivuje, zikiwamo zinazohusu maisha yao ya kila siku.

 

Kulingana na kazi zinazofanywa na kitengo cha Usalama wa Taifa ni kwamba hata kama utamng’oa mkuu wa Usalama wa Taifa na maafisa wote wa ngazi ya juu wa kitengo hicho, bado utakuwa hujafanya lolote kwa vile kitengo cha Usalama wa Taifa ni jeshi kubwa lenye watu wengi ambao kwa muda mrefu wamefundishwa mafunzo mbalimbali ya kutekeleza majukumu ya mtandao.

 

Ina maana kwamba wanamtandao wamefuzu katika fani mbalimbali na kila mmoja anajivunia kuijua na kuiweza kazi yake vizuri! Hivyo kumng’oa mkuu wa kitengo ambaye hajihusishi na vitendo vya kuteka nyara, kutesa na inapobidi kuua; sidhani kama Watanzania watakuwa wamepona! Labda kama kitengo hicho kivunjwe, jambo ambalo si rahisi!

 

Kulingana na uzoefu wangu na jinsi ninavyoijua nchi hii, ni kwamba mwandishi wa makala haya ama ni mtu wa Usalama wa Taifa ambaye ametumiwa na kitengo hicho kuandika makala hayo ili akinusuru kitengo hicho, na ili kujenga mazingira ya kumwezesha mkuu wa Usalama wa Taifa astaafu na kupewa mafao yake manono, au huyu mwandishi wa makala hayo haujui kwa undani wa usalama wetu wa taifa – kazi wanazozifanya kwa ujumla.

 

Mimi nahitimisha kwa kusema kwamba kulingana na uzoefu wangu, asilimia tisini na nane (98%) ya matatizo yote yanayoukabili umma wa Watanzania hivi leo, yanachangiwa na baadhi ya maofisa wa kitengo cha Usalama wa Taifa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.

 

Matatizo hayo ni pamoja na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma; umaskini uliokithiri miongoni mwa Watanzania ukiwamo wa ufisadi wa rasilimali za umma; udini kwenye sekta ya elimu na sehemu za kazi kwa ujumla; kuwagawa wananchi kwenye makundi ya imani za kidini wakati mwingine kwa maslahi ya kisiasa; biashara mbalimbali haramu hapa nchini; ujambazi na hujuma mbalimbali dhidi ya raia; kuchakachua matokeo ya uchaguzi mbalimbali, na mengime mengi tu!

 

Hivyo basi, kulingana na sababu hizo hapo juu za kimsingi na zenye mashiko mazuri, itakuwa si busara kabisa kuendelea kukaa kimya bila kushauri kitengo hiki kihamishwe kutoka Ofisi ya Rais na kupelekwa ama katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa au Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia kuna haja ya kitengo hiki kuongezewa watu wapya wenye mawazo safi na yenye tija kwa jamii.

Mwandishi wa makala haya, Dk. Noordin Jella (PhD in Economics), ni Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu Huria, Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa ni Mwandishi wa Kujitegemea na Mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kwa email: norjella@yahoo.com

Simu: +255 782 000 131


1733 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!