Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) Kanda ya Ziwa imeingia ‘vitani’ na Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikizuia maofisa wa jiji hilo kufanya ukaguzi kwenye maduka ya vipodozi, dawa na maeneo mengine ya kibiashara.
Haya yanafanyika huku Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ikiwa imekwisha kumwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa TFDA ikimuomba kufanya kazi kwa ushirikiano na TAMISEMI.

Barua hiyo ya Januari 16, mwaka huu iliyosainiwa na Dk. Ntuli Kapologwe, kwa niaba ya Katibu Mkuu OR -TAMISEMI, inahimiza pande hizo kushirikiana katika kazi.
“OR-TAMISEMI kupitia Idara yake ya Afya imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa kazi na majukumu ya Mamlaka ya Chakula na Dawa katika kanda zake kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kubaini yafuatayo, yanayopaswa kufanyiwa maboresho.

“OR-TAMISEMI na Sekretarieti za Tawala za Mikoa kutokushirikishwa katika kazi za TFDA, wala kupatiwa mrejesho wa kazi za TFDA zinazoendelea, chini ya maeneo yake ya usimamizi na utawala ilhali changamoto zinapotokea au kujulikana, ndio wanapaswa kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu,” inasema sehemu ya barua hiyo ambayo JAMHURI imeiona.
Hata hivyo, TFDA haitaki Jiji la Mwanza lifanye ukaguzi kwenye maduka ya vipodozi na kwingineko.
“Wanatuita sisi matapeli. TFDA wamefika pabaya, Januari 25, 2019
wamekwenda kwenye duka dogo la raia wa China lililopo Barabara ya Nyerere wakang’oa leseni halali iliyotolewa na uongozi wa jiji.
“Wamepata wapi kiburi cha kung’oa kibali cha biashara kilichotolewa na mamlaka ya jiji, tena kina saini na mhuri wa mkurugenzi ambaye ni mteule wa rais?” amehoji ofisa aliyezungumza na JAMHURI.

Anasema Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009, pamoja na kanuni zake, zinaruhusu mtaalamu wa afya na mazingira wa halmashauri kufanya ukaguzi.
Anasema kuwa wanapofanya ukaguzi katika maduka ya wafanyabiashara wa vipodozi, dawa na viwandani hukuta vitu vilivyozuiliwa na serikali, licha ya kwamba ukaguzi wa TFDA ulikwisha kufanyika maeneo hayo.

Anasema mwaka 2017 alitishiwa na mmoja wa watumishi wa TFDA, kitengo cha ukaguzi (jina tunalo), baada ya kukamata bidhaa zilizopigwa marufuku na serikali, vikiwamo vipodozi vyenye viambata vya sumu.
Anasema biashara hiyo haramu inawahusisha baadhi ya maofisa wa TFDA Kanda ya Ziwa wanaowalinda wahalifu hao.

“Stoo za vipodozi vikali zinazidi kukua siku hadi siku. Na watu wanajiamini kana kwamba ni kitu halali kinacholipiwa kodi, na hakina madhara ya kiafya. Ushahidi upo. Hao jamaa wanakula rushwa hadi wanaanza kutetea wafanyabiashara…wanasema ni machimbo yao ya kuvuta hela,” anasema.
Anaongeza: “Dawa zilizo expire [kwisha muda wa matumizi] zinauzwa ovyo tu kwa watu. Na hawa jamaa ukiingia dukani kukagua dawa hizo wanawajaza watu ujinga kuwaambia ni TFDA tu ndio wana ruhusa ya kuangalia lebo ya dawa hizo. Wapo kimasilahi sana.”
Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa, Moses Mbambe, anasema maofisa wa jiji hawaruhusiwi kufanya ukaguzi wowote, bali kazi hiyo inafanywa na wataalamu wa mamlaka yake pekee.
“TFDA tunakagua na kukamata bidhaa zote zinazouzwa kinyume cha sheria za nchi. Nikikufungulia stoo yetu utaona vitu vingi tulivyovikamata vimo humo. Huwa tunaviteketeza kwa moto,” anasema Mbambe.

Alipoombwa na gazeti hili afungue kuona vitu vilivyomo ndani ya stoo hiyo, meneja huyo aligoma.

“Hao wa jiji wanawadanganya tu watu, hawana mamlaka ya ukaguzi. Sasa wanapokamata mali za wafanyabiashara wanazipeleka wapi? Wanaziteketezea wapi kama siyo sisi TFDA?” amehoji.

Wakati Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa akisema hayo, Ofisa anayeshughulika na masuala ya afya Jiji la Mwanza, Sophia Kiluvia, anasema iwapo mamlaka inazuia,  lazima iwape mwongozo wa maandishi.
Anasema kuwa wanayo mamlaka ya kufanya ukaguzi madukani kisha kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Mratibu wa Kitengo cha Ubora na Usalama wa Chakula Jiji la Mwanza, Sabbo Shilinde, anasema Ofisa Afya wa Jiji wanaruhusiwa kufanya ukaguzi.
“Endapo itabainika kwamba mkaguzi amekiuka taratibu kwa kutoa upendeleo, ama kumwonea; mamlaka husika haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu za kiutumishi.
“Taarifa ya ukaguzi ni sharti iandaliwe ikionyesha upungufu na hatua zilizochukuliwa. Kwa hiyo, tuna mamlaka ya kukagua,” anasema Sabbo.

JAMHURI imeelezwa kuwa Buhongwa na Mkolani ni miongoni mwa maeneo ambayo biashara ya vipodozi na dawa hizo imeshamiri.

Novemba 16, mwaka jana TFDA kupitia maofisa wake (majina yao tunayo) walifanya
ukaguzi katika duka moja jijini hapa, kisha wakaandika taarifa ya kutokuwapo vipodozi vyenye viambata vya sumu.
Lakini Desemba 12, mwaka huo huo ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Jiji la Mwanza katika duka hilo hilo ulibaini kuwapo vipodozi vyenye viambata vya sumu vilivyopigwa marufuku.
Ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Jiji Desemba 21, mwaka jana ulibaini duka lililopo Mtaa wa Nkrumah kutokuwa na usajili wala kibali cha kibiashara cha TFDA, huku vipodozi vyenye viambata vya sumu vikiuzwa dukani humo. Duka hilo halikuwa na leseni ya biashara ya Halmashauri ya Jiji. Baadhi ya bidhaa zilizouzwa humo ni unga wa lishe usiokuwa na tarehe ya kutengenezwa na mwisho wa matumizi.

Desemba 28, mwaka jana ofisa wa polisi alikamata vipodozi vilivyopigwa marufuku kuuzwa nchini katika duka la mfanyabiashara (jina tunalo) lililopo Buhongwa.

Inadaiwa kuwa baada ya bidhaa hizo kukamatwa, ofisa mmoja wa TFDA alipigiwa simu na mwenye duka, akafika dukani na kuzuia mfanyabiashara huyo mwanamama asichukuliwe hatua zozote za kisheria.
JAMHURI limepata majina ya maofisa wa TFDA Kanda ya Ziwa wanaotajwa kuwa vinara wanaoshiriki kulinda wafanyabiashara wa vipodozi haramu jijini Mwanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, anasema Jiji na TFDA ni mamlaka kamili zilizoundwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kila idara inaruhusiwa kufanya ukaguzi kulingana na sheria.
“Inategemea nani anakagua nini. Mfano kiwanda hakina choo, ukaguzi wake unafanywa na mimi jiji. Lakini kama kuna tatizo sisi watumishi tutakaa kulizungumza,” anasema Kibamba.

Anasema hata Mahakama inajua mamlaka yake inaruhusiwa kutoa vibali kwa wafanyabiashara kwa mujibu wa sheria. Amewaonya watumishi wa TFDA akisema: “TFDA hawapaswi kuja huku kama chooni. Kila kitu kina utaratibu wake. Mimi nina kata 18, hauwezi kuja tu kukagua bila mimi kujua. Ukipigwa kule!”
Kuhusu kuondolewa vibali vilivyotolewa na Jiji la Mwanza, Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa amekiri kuwa  mamlaka yake imeviondoa.

“TFDA ilikasimu baadhi ya mamlaka kwa halmashauri kwa mujibu wa sheria. Nasema baadhi, siyo yote. Jiji hawaruhusiwi kutoa vibali kwenye maduka ya jumla. Wanaruhusiwa kutoa vibali kwenye bucha, migahawa na maduka ya rejareja,” anasema.

Anasema mamlaka yake pekee ndiyo yenye uhalali kisheria wa kutoa vibali kwenye maduka ya jumla, na si jiji.

Anasema halmashauri haina maabara kwa kuwa haikagui ubora wa bidhaa. “Sisi tuna utaalamu wa kukagua na kuzuia bidhaa zilizopigwa marufuku ili binadamu asizitumie. Sasa TFDA wanatuzuia tusizuie hayo madhara kwa watu. Tuna orodha ya vipodozi na dawa zilizopigwa marufuku na serikali,” anasema.

Anasema TFDA inawazuia watumishi wa jiji kukagua hata lebo ya muda wa matumizi na ukomo wa bidhaa. “Wanaokagua ubora ni TBS ndio wana maabara. Pia TFDA wana maabara na wana mamlaka ya usajili,” anasema.

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, anasema hajapokea taarifa ya tuhuma za rushwa kwa watumishi wa TFDA.

1050 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!