Seif_hamad(17)Hakika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa Tanzania visiwani (Zanzibar) imepata wakati mgumu kutokana na uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 uliojaa vituko vingi kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) chini ya mwavuli wa UKAWA. Uchaguzi ulikuwa na dosari nyingi kutoka pande zote za ushindani katika urais, wawakilishi na madiwani kutokana na malalamiko kutoka pande zote za vyama vya CCM na CUF. Kila chama kilitoa malalamiko yake ya kuonewa na chama kingine hivyo kuifanya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo yote na Maalim Seif Shariff Hamad(mgombea urais-CUF) akaamua kutangaza kuwa yeye ndiye anaongoza katika kura za urais na wawakilishi wa Zanzibar. Hapo ndipo vuta nikuvute ya kurushiana maneno makali kutoka pande zote Zanzibar ilipoanza.Mvutano huu wa kisiasa Zanzibar una historia ya muda mrefu zaidi ya mwaka 1964 baada ya kufanyika Mapinduzi Matukufu ya kuuondoa utawala wa kifalme wa Waarabu wenye asili ya Oman ambao waliitawala Zanzibar kuanzia  mwaka 1805 mpaka 1964 baada ya hayati, Sheikh Abeid Aman Karume na makomredi wenzake akina Yusuph Himid, Seif Bakari, Mussa Maisara na wengine kuamua kujitolea maisha yao kwa ajili ya kuung`oa utawala wa kifalme ulioitawala Zanzibar kwa muda mrefu bila ridhaa ya Wazanzibari. Baada ya kufanyika mapinduzi hayo na kufanikiwa kuundoa utawala wa kifalme hayati Karume aliamua kuzungumza na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akitaka waziunganishe nchi mbili za Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Viongozi hawa walikubaliana haraka juu ya Muungano wa Tanzania ambayo imedumu leo, japo kwa misukosuko ya hapa na pale kutokana na maslahi ya watu wachache katika Muungano huu. Kwa ufupi Zanzibar baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 wafuasi wengi wa mfalme aliyeondolewa madarakani kwa nguvu na wao waliamua kuondoka Zanzibar na kuelekea Mombasa, Oman, Falme za Kiarabu (UAE) na sehemu nyingine za dunia kama wakimbizi wakisiasa ambao walidai wananyanyaswa na utawala wa Karume na wenzake 12 (wajumbe wa Baraza la Mapinduzi) hivyo Waarabu hao walikwenda Falme za Kiarabu na hasa Dubai. Mfalme wa Dubai wa wakati huo alikuwa Sheikh Rashid Al- Maktoum aliyewapokea vizuri na kuwapa hifadhi ya makazi eneo maarufu kwa jina la RASHIDIYA. Hapo ndipo walipoweka makazi yao ya kuishi na baadhi yao walielekea Oman (Muscat) kwa mfalme QUABOOS na kufanya makazi yao ya kudumu kwa vile mtawala wa mwisho wa Zanzibar alikuwa Mwarabu mwenye asili ya Oman. Zanzibar hawakuondoka Waarabu wote. Wengine walibaki na kuendelea na maisha ya Zanzibar chini ya utawala Waafrika ambao waliupokea kwa shingo upande kwa kuwa hawakuamini kuwa ingetokea siku Mwafrika Mweusi akaitawala Zanzibar katika ramani ya dunia. Oman iko Asia, haiko Afrika kama Libya, Misri, Tunisia, Morocco na Algeria japo wote hao ni Waarabu na wanazungumza lugha moja ya Kiarabu. Machotara wa kwanza waliochanganyika damu na Waafrika weusi walikuwa baba zao Waarabu wenye asili ya Oman na Yemen na mama zao Waafrika weusi. Huo ndio uchotara ulioanza kabla ya mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964 kwa vile wazee hao wa Kiarabu waliokuja kwa ngalawa kutoka Uarabuni hadi Zanzibar wasingeweza kuja na familia zao kutokana na hatari kubwa ya baharini kwa kutumia ngalawa na meli ndogo hivyo walipofika Zanzibar wakaamua kuishi na bibi zetu na mama zetu wa Kiafrika na kutokea machotara wa Kiafrika na Kiarabu. Baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 hayati Karume aliamuru kuwa kuanzia wakati huo ilikuwa huru kuoleana kwa maana kuwa mwanaume mweusi ruksa kuoa mwanamke wa Kiarabu, Mhindi, Mzungu, n.k. Hapo ndipo chuki ilipoelekezwa kwa Karume kuwa kwa nini ametoa amri hiyo kwa wanaume wa Kiafrika kuoa wanawake wenye asili ya Kiarabu na Kihindi.Baada ya mwaka 1964 walianza kutokea machotara ambao baba zao ni Waafrika na mama zao ni Waarabu au Wahindi na wale ambao waliona fedhea waliamua kuikimbia Zanzibar kuja Tanzania Bara au Mombasa, Kenya, na nchi za Kiarabu na hasa Oman na U.A.E. Waarabu hao ndiyo waliokuwa wakiulaani utawala wa Sheikh Karume na chama chake cha Afro Shiraz kuwa kinawanyanyasa. Aprili 7, mwaka 1972 Afisa wa Jeshi la Zanzibar, Luteni Humud aliamua kulipiza kisasi kwa kumpiga risasi Sheikh Abeid Aman Karume na kumuua. Yeye Luteni Humud alipigwa risasi na walinzi wa Rais wa Zanzibar Abeid Aman Karume. Inadaiwa kuwa Humud alidai kuwa baba yake Humud aliuawa na askari wa Karume katika mapambano ya vita ya Mapinduzi ya Zanzibar.Mwalimu Nyerere alikuwa anaijua vizuri historia ya Zanzibar na tabia ya Wazanzibari. Katika maisha ya kila siku na hata maamuzi ya kuunganisha vyama vya ASP na TANU ilikuwa ina madhumuni ya kuzidi kuimarisha Muungano wa Tanzania na kuondoa migongano visiwani humo kwa vile chama cha siasa kilibaki kuwa kimoja kuanzia mwaka 1977. Pamoja na chama kuwa kimoja CCM, chokochoko za hapa na pale ndani ya chama na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilikuwa zikidhibitiwa haraka na vyombo vya usalama na Mwalimu alikuwa akifuatilia kwa umakini mwenendo wa Serikali ya Zanzibar na viongozi wake.Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 hapa nchini chama cha CUF kwa upande wa Zanzibar kilipata wanachama wengi machotara wenye asili ya Oman ambao walikuwa wamemezwa na CCM katika mfumo wa chama kimoja. Baada ya kuanzishwa vyama vingi wengi wao walihamia CUF ndipo vuta nikuvute ilipoanza visiwani humo kati ya Wapemba na Waunguja.Wapemba wengi wakaingia CUF na Waunguja wengi wakawa CCM (AFRO SHIRAZI PARTY). Hapo yalianza mapambano kati ya viongozi wa CCM na CUF akiwemo Salmin Amour (Komandoo) na Maalim Seif Sharif Hamad. Vuta nikuvute hiyo iliendelea kwa kuonyeshana ubabe wa kisiasa visiwani humo kwa maneno makali kati ya viongozi wa CCM na CUF na wanachama wao kila mmoja anajiona bora kuliko mwingine. CUF kila uchaguzi uliofanyika walidai kushida na kwamba CCM Zanzibar inawapora ushidi kwa kutumia dola.Mwalimu Nyerere alipoona Muungano wetu umeingiliwa na nyufa, aliamua kufanya mkutano na wanandishi wa habari pale Kilimanjaro Hotel na kuzungumzia nyufa za Muungano.Wakati huo Rais alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi na Waziri Mkuu, akiwa Mzee John Samwel Malecela. Mwalimu alihisi kuna njama za kutaka kuuvunja Muungano. Mwalimu alifoka mno hivyo na kuwakemea watu wote waliokuwa na nia hiyo kutoka bara na visiwani kwa vyovyote Mwalimu aliwajua kwa majina yao waliotaka kuuvunja Muungano. Mwalimu Nyerere alilazimika kutoa maneno ya mafumbo kwa kuwambia Wazanzibari kuwa “Mnajiita Wazanzibari ndani ya Muungano, nje ya Muungano hamtakuwa hivyo bali itakua nyie Wapemba na nyie Waunguja.” Mwalimu alizifahamu vizuri tofauti zao za kihistoria. Mwalimu alielewa kuwa visiwa vya Unguja na Pemba haviwezi kuwa salama bila Muungano wa Tanzania Bara. Alijua kuwa nje ya Muungano kuna Waunguja na Wapemba. Usalama wa Zanzibar pia umechangiwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi imara la Wananchi wa Tanzania kuwa moja, vinginevyo ingekuwa historia nyingine. Nashawishika kusema Wazanzibari wenye mapenzi mema lioombeeni jeshi hili liendelee kuwa imara kwa maslahi mapana ya usalama wa Wazanzibari wote. Jeshi hili ndani ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kuwa maadui wa nje na wa ndani hawaichezei Zanzibar na Tanganyika  (TANZANIA).Yeyote anayetaka JWTZ waondoke Zanzibar huyo ni adui mkubwa wa Wazanzibari kwani haitakii mema Zanzibar na wananchi wake. Pia Wazanzibari kuweni macho na wanasiasa wanaotoa maneno ya uchochezi kuwa Zanzibar itawaka moto. Wazanzibari tumieni nguvu zenu zote kuhakikisha kuwa amani yenu haipotei kwa kuwanufaisha wanasiasa ambao wameweka maslahi yao mbele kuliko maslahi ya taifa. Pia epukeni ushauri wa kutoka nje ya nchi wanaowashawishi kuanzisha fujo huku sisi tutawatumia fedha na silaha wakati wao hawatakabiliana na mapambano na jeshi kwa kuepuka. Wazanzibari nawaombeni muwe na subira kama waswahili wasemavyo hasira hasara. Kuweni wavumilivu wa misukosuko ya siasa nawashauri mkubali kwa moyo mmoja kufanya uchaguzi utakaokuwa huru na haki apatikane mshindi halali ikibidi hata uchaguzi ahirisheni hadi Mei, 2016 mfanye maandalizi ya kutosha ya uchaguzi kuimarisha amani miongoni mwa Wazanzibari. Kama kuna kasoro mnaziona rekebisheni kabla ya uchaguzi huo wa marudio wekeni mbele maslahi ya Zanzibar kuliko maslahi ya vyama vyenu kasoro zote zilizojitokeza hakikisheni mnaziondoa kabla ya Machi 20,2016 uchaguzi ufanyike kwa amani na mshindi apatikane bila ya manung’uniko ya upande moja. Wazanzibari lindeni utulivu kuepusha kumbebesha mzigo usio wake Rais John Magufuli kwani yeye ni mgeni katika kiti cha urais, hivyo kumwingiza kwenye mgogoro wa Zanzibar ni sawa na kumuonea. Binafsi naona mgogoro huu ni vyema marais wastaafu waedelee nao kuliko yeye. Mfano kama Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete naamini anaujua kwa undani kuliko viongozi wengine. Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi ameshakuwa mtu mzima tusimsumbue amelitumikia taifa kwa muda mrefu. Rais mstaafu wa Zanzibar Aman Abeid Karume wana-CCM Zanzibar hawamwamini kwa kutojua ana msimamo gani kama yeye ni CCM au CUF. Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanzania.

 

Mwandishi wa Makala hii ni Mwanajeshi Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  0785 042078.

2207 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!