Wiki tatu zilizopita, Rais Jakaya Kikwete alimteua John Mongela kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Mongela anachukua nafasi ya Kanali Fabian Massawe ambaye uteuzi wake ulipotenguliwa taarifa ya Ikulu ilisema atapangiwa kazi nyingine. Wapo waliofurahi, na wapo walionuna.

Kwa uzoefu wangu usio mkubwa wa walau miaka zaidi ya 20 katika kazi hii, Massawe ndo ‘ngoma’ imefikia mwisho. Nafahamu Massawe anapigiwa upatu. Nimemfahamu Massawe siku nyingi kidogo, tangu akiwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jeshi ya Jitegemee, Dar es Salaam.

Namfahamu Massawe akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, baadaye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, na hatimaye Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Massawe kila anapopita migogoro inamfuata. Akiwa Kinondoni, mgogoro wa ardhi Luguruni, Dar es Salaam haukuwa na kipimo.

Akiwa Karagwe tunakumbuka mgogoro uliofukuta pale hadi watumishi wa halmashauri wakasimamishwa kazi kwa zaidi ya mwaka, huku aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Lunyogote akitamba. Alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Massawe pale alivunja rekodi, akashiriki mgogoro wa ardhi Bukoba.

Nikiri kuwa “Baniani” anaweza kuwa mbaya, ila kiatu chake kikawa dawa. Kabla sijazungumza ya ovyo aliyofanya Massawe, nigusie kwanza zuri moja angalau. Usafi. Hakika Massawe alijitahidi kuhakikisha Mji wa Bukoba unakuwa safi. Kichungi cha sigara kilitosha kumpiga faini ya Sh 50,000 aliyekitupa. Mongela hili liendeleze.

Mji ukawa safi. Katika hili nampongeza Massawe. Hata hivyo, alijiingiza katika vitendo visivyokubalika duniani na mbinguni. Alijiingiza katika ushirikiano usio mtakatifu na manyang’au. Wazaliwa wa Bukoba Mjini wakapokwa kila chembe ya haki katika ardhi.

Sitanii, mgogoro wa ardhi unaoendelea katika halmashauri ya Manispaa ya Bukoba hadi leo una sura nyingi. Zipo tuhuma tisa zinazofahamika karibu kwa kila mtu, ila pia mazungumzo yaliyofanywa na JAMHURI mjini Bukoba hivi karibuni yamethibitisha uwapo wa wasiwasi mkubwa katika kila kona ya mji.

Julai 7, 2013 madiwani 15 wa Manispaa ya Bukoba waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba wakitumia Kanuni Na 80 ya Kifungu (1) na (2) cha Kanuni za Kudumu za Hamashauri pamoja na Tangazo la Serikali Na. 264 la Mwaka 1995 dhidi ya aliyekuwa Meya, Anatory Amani.

Baada ya kuwezeshwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), JAMHURI lilichunguza na kubaini kuwa tuhuma dhidi ya aliyekuwa Meya zilianza kupigwa danadana na zikawa zinahamishwa kutoka kwa aliyekuwa Meya kwenda kwa watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Diwani wa Kahororo, Chifu Adronikus Karumuna aliyelijulisha JAMHURI kuwa anamuunga mkono Amani, aliweka bayana kuwa waliopaswa kukaguliwa ni watendaji wa halmashauri na si aliyekuwa Meya, kwani aliyekuwa Meya si mtendaji. CAG alipofanya ukaguzi alibaini maajabu makubwa.

Sitanii, Mongela ni mmoja kati ya vijana wachapakazi wa kweli katika Tanzania. Nimemfahamu Mongela kitambo, akiwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na baadaye Mkuu wa Wilaya Kigoma, kisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha. Kote alikopelekwa alikutana na migogoro, lakini ameimaliza.

Kwa Mkoa wa Kagera, tuhuma kubwa iliyomgharimu Katibu wa CCM, Everine Mushi, Amani na sasa Mkuu wa Mkoa Massawe ni kutaka kupora wakazi wa Manispaa ya Bukoba ardhi.

Aliyekuwa Meya aliamua kuchukua mikopo bila kibali cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupima viwanja na kuuza. Madiwani waliozungumza na JAMHURI, walikiri kuwa walishirikishwa katika hatua za awali za kuandaa miradi hiyo, ila utekelezaji uligeuka wa upande moja.

Sheria ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982 kifungu cha 51 (1) – (7) inasema kwa kila mkopo lazima halmashauri ipate kibali cha Baraza la Madiwani, lakini Meya wa zamani Anatory alikopa Sh milioni 500 zaidi ya kiasi kilichokubaliwa kutoka UTT bila kupata kibali cha Baraza la Madiwani.

Awali alikuwa amekubaliwa kukopa Sh bilioni 2.4, lakini akakopa Sh bilioni 2.9. Ukiacha hilo, sheria inataka mkopaji awe Mkurugenzi na si aliyekuwa Meya.

Sitanii, hadi leo katika eneo hili, kuna malalamiko ya wananchi kupunjwa fidia kwa kulipwa wastani wa Sh 300 kwa mita ya mraba na kutakiwa kuinunua mita hiyo hiyo kwa Sh 4,000 baada ya kupimwa. Baadhi ya viwanja vya wananchi vimechuliwa bila kulipwa fidia, kama inavyokiri taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba aliyehamishwa Hamis Kaputa kuwa wamilikia 280 ardhi yao ilitwaliwa bila kulipwa fidia.

Soko la sasa la Bukoba lilitakiwa kuvunjwa na kujengwa jipya. Madiwani 15 walimtuhumu aliyekuwa Meya kuwa alikopa Sh milioni 200 kutoka UTT bila kufuata utaratibu wa kupata kibali cha Baraza la Madiwani. Aliyekuwa Meya anatuhumiwa pia kusitisha malipo na ushuru wa kila aina katika soko hilo, akitaka livunjwe ifikapo Januari 15, 2013. Hadi leo halijavunjwa.

Mkopo huu aliuchukua kwa riba ya asilimia 24, na wanadai pia kuwa aliyekuwa Meya alikopa fedha kiasi cha Sh milioni 450 kutoka Benki ya Posta, ambazo madiwani walielezwa kuwa sehemu ya fedha hizo ingetumika kulipa mkopo wa UTT. Wafanyabiashara wa sokoni walifungua kesi kupinga kuvunjwa kwa soko wakidai hawajashirikishwa.

Sitanii, madiwani walimtuhumu aliyekuwa Meya kuwa ametumia jumla ya Sh milioni 257 kuanzisha mradi wa kuosha magari, na wakasema taratibu za zabuni hazikufuatwa katika kutoa zabuni hii eneo la Kishenge. JAMHURI lilizungumza na wakurugenzi wanaosimamia mradi huo, ikathibitika kuwa taratibu zilivunjwa.

Madiwani walimtuhumu aliyekuwa Meya kuwa aliteua mkandarasi wasiyemjua kujenga Stendi ya Mabasi Kyakailabwa katika Kata ya Nyanga, na walielezwa kuwa mkandarasi alilipwa Sh 135,400,000. Hadi leo stendi imeota nyasi.

Katika eneo la sasa ilipo stendi ilikubaliwa kuwa ujengwe mradi wa kisasa wa kitege uchumi kwa kujenga jengo lenye urefu wa ghorofa 10 au zaidi. Madiwani walisema sheria, kanuni na taratibu za kuanzishwa kwa mradi huu zilikiukwa.

Aliyekuwa Meya alituhumiwa kufanya uamuzi wa kubadili matumizi yaliyopitishwa na Baraza la Madiwani kupitia kwenye Kamati ya Fedha na Uongozi. Kamati hizi zilidaiwa kuongozwa na watu waliomuunga mkonoMeya katika kila jambo alilofanya. Pia kamati hizi zinatuhumiwa kukopa kwa niaba ya halmashauri kitu ambacho ni kinyume na sheria.

Sitanii, madiwani walisema miradi mingi ilipitishwa kwa kauli za mdomo bila kuwapo maandishi yenye kuonyesha mchanganuo wa mradi, kinyume na kanuni Na 42 Kifungu cha 2 (f) cha Kanuniz a Kudumu za Halmashauri.

Mkuu wa Mkoa Mongela, aliyekuwa Meya alituhumiwa kutumia vibaya gari la halmashauri Na SM 8807 alilonunuliwa na halmashauri mwaka 2010. Gari hili inadaiwa kuwa liliharibikia kusikojulikana na hadi mwaka huu lilikuwa halijatengenezwa au kuondolewa katika orodha ya mali za halmashauri. Hata hivyo, Januari 2013 halmashauri ilitoa ankara ya ununuzi kwa ajili ya kutengeneza gari hilo, lakini hadi sasa halijarejeshwa kwenye halmashauri.

Si hayo tu, bali zipo taarifa kuwa Shule ya Msingi Kiteyagwa ilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu ambao ulikuwa unatumiwa na watoto, lakini kwa sasa aliyekuwa Meya Amani ameuchukua uwanja huo na kujenga majengo ya shule zake za Amani English Medium Primary School na Peace Secondary School. Uwanja huu ulikuwa unatumiwa na wanafunzi wa shule za Kiteyagwa, Rwemishasha na Rwamishenye, na hivyo sasa hawana mahala pa kuchezea mpira.

Sitanii, pia upo mradi wa maji ulipoaswa kujengwa kwenye Kata Nyanga kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, mradi huo aliyekuwa Meya Amani alituhumiwa kuuhamishia Kagondo Karuguru, lakini la ajabu zaidi tenki la maji limejengwa kilimani na kuelekeza maji zilipo shule zake za msingi na sekondari, hivyo wengi wanasema mradi huu aliuhamishia Kagondo si kusaidia wananchi bali kuwezesha shule zake kupata maji. Baada ya makala nilizoandika mradi huu ulirejeshwa Kata Nyanga.

Madiwani walimtuhumu aliyekuwa Meya kuwa hesabu zinazotolewa kwenye muhtasari wa halmashauri zinatofautiana kwa kiasi kikubwa na matumizi halisi. Kwa mfano, Muhtasari Na. 08/99/29/1/2013 unaonyesha kuwa fedha zilizotumika katika ununuzi ni Sh 485,269,842, wakati matumizi sahihi ni Sh 32,698,533.33. Wanasema fedha iliyopotea ni Sh milioni 452,571,309.33. Mihtasari mingi ina upungufu wa kutisha katika tofauti kati ya matumizi yanayotajwa na matumizi halisi.

Sitanii, kilele cha mgogoro kilikuwa Agosti 14, 2013 wakati Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera ilipowafukuza uanachama madiwani wanane Deusdedith Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Dauda Karumuna (Ijuganyondo), Samuel Ntambala Luhangisa (Kitendaguro), Yusufu Ngaiza (Kashai), Richard Gasper (Miembeni), Alexanda Ngalinda –aliyekuwa Naibu Meya (Buhembe) na Murungi Kichwabuta (Viti Maalum).

Hata hivyo, Kamati Kuu ya CCM ilibatilisha uamuzi huo na kuagiza ufanyike ukaguzi maalum kwenye halmashauri kubainisha tuhuma dhidi ya aliyekuwa Meya Anatory Amani. Tuhuma nyingi zilithibitishwa, aliyekuwa Meya akaenguliwa, Katibu wa CCM akahamishwa Mkoa na sasa Mkuu wa Mkoa amehitimisha orodha kwa kuachwa nje ya orodha.

Sitanii, nimeyasema haya si kwa nia nyingine, maana niliishayaandika, bali kumpa fursa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mongela awafahamu vyema watendaji na ajue sura halisi ya mkoa anaofanyia kazi. Zipo tuhuma za rushwa na kesi kadhaa zinaendelea, ila kinachotakiwa Kagera ni haki na mengine yote watayapata kwa ziada.

Mongela karibu Bukoba, karibu Kagera. Ukitenda haki, historia itakukumbuka. Ukiachagua mkondo wa mtangulizi wako wa kupoka wananchi wa Bukoba ardhi, tangazo litakalofuata utasikia redioni kuwa utapangiwa kazi nyingine. Mongela ijenge Kagera, maliza migogoro. Mungu ibaridi Tanzania.

By Jamhuri