Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani) baada ya kuwasili kwenye kambi ya Uvuvi ya Kisiwa cha Galinzila leo na kuongea na wavuvi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomiah Chang’a (mwenye kofia) na kulia zaidi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe Frank Bahati leo. Mhe. Mpina alichoma moto nyavu haramu za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni mbili.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akiwahutubia wavuvi kwenye kambi ya wavuvi katika kisiwa cha Galinzila Wilayani Ukerewe ambapo baadaye alichoma moto nyavu haramu za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni mbili katika kijiji Kakukuru.
Umati wa wavuvi kwenye kambi ya wavuvi ya Kisiwa cha Galinzila wilayani Ukerewe wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayupo pichani) ambapo baadaye alichoma moto nyavu haramu za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni mbili katika kijiji cha Kakukuru zilizokamatwa katika operesheni maalum ya siku tano ya kutokomeza uvuvi haramu katika Wilaya ya Ukerewe leo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akiwa katika picha ya pamoja na kikosi kazi kilichofanya operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu katika Wilaya ya Magu na Busega mara baada ya kuteketeza kwa kuchoma moto zana haramu za uvuvi zenye thamani ya Tsh 457,075,000/= katika kijiji cha Kageye wilayani Magu leo. 
 
 
 
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina ametaifisha na kuteketeza zana haramu za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni 2 zilizokamatwa wakati zikitumika kwa shughuli za uvuvi katika visiwa vidogo vilivyopo ndani ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza huku Shilingi milioni 120 zikikusanywa kama sehemu ya adhabu kwa wavuvi na wafanyabiashara waliokutwa na zana haramu pamoja na makosa ya utoroshaji samaki na mazao yake nje ya nchi.
Waziri Mpina aliwaonya watu wanaotumia majina ya wavuvi kutishia kufanya migomo isiyoisha na kuandamana baada ya uamuzi wa Serikali kuanza kuchukua hatua stahiki za kudhibiti uvuvi haramu, na kwamba msimamo uliowekwa na Serikali ni thabiti na usiyoyumba hivyo migomo na maandamano ya watu wenye lengo la kukwamisha vita dhidi ya uvuvi haramu haitasaidia chochote na badala yake operesheni kali isiyo na mwisho itaendelea hadi pale uvuvi haramu utakapokoma ndani ya Ziwa Victoria.
“Rasilimali zilizopo ndani ya ziwa hili ni mali ya wananchi sisi viongozi mliotupa dhamana ya kuongoza kazi yetu ni ulinzi tu na endapo tutakomesha uvuvi haramu nyie ndio mtakaonufaika hivyo ni itashangaza tajiri aliyempa kibarua cha ulinzi, na mlinzi huyo akafanya kazi vizuri ya kulinda mali za bosi wake alafu tajiri akamlalamikia kibarua wake sisi na watendaji wa Serikali ni vibarua tu wenye mali ni ninyi hatua tunazochukua zitaleta manufaa makubwa kwenu”alisema.
Pamoja na kuteketeza zana haramu, Waziri Mpina alieleza hali ya upatikanaji wa samaki aina ya sangara katika Ziwa Victoria ambapo alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (TAFIRI) 2017 unaonesha kuwa samaki waliochini ya sentimita 50 ni asilimia 96.6 hivyo samaki hawa ni wachanga na hawarusiwi kuvuliwa ambapo samaki walio zaidi ya sentimita 85 ni asilimia 0.4 tu ambao ni wazazi na hawarusiwi kuvuliwa pia. Samaki wa sentimita 50 mpaka 85 ambao ndio wanafaa kuvuliwa ni asilimia 3 tu.
“Tafsiri yake ni kwamba ziwa halina samaki wanaostahili kuvuliwa kulingana na kasi ya uvuvi na pia samaki wazazi ni kidogo ambapo inatishia kumalizika kwa samaki na shughuli za uvuvi kukoma katika Ziwa Victoria’alisema .
Akizungumza kwa nyakati tofauti na maelfu ya wavuvi katika Visiwa vya Gagalini na Kakukuru wilayani Ukerewe Waziri Mpina amesema hatua kali zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya uvuvi haramu hazilengi kuwaonea wananchi wanyonge bali kuwatengenezea maisha bora ya kizazi cha sasa na baadae ili kiweze kunufaika na rasilimali zilizoko ziwani.
Akiwa katika eneo la Kakukuru Waziri Mpina alishiriki kuteketeza zana haramu zikiwemo vyavu za Makila 14,103, Kokoro 188 , Nyavu za dagaa 211, Nyavu za timba 450, Kamba za Kokoro 10,700 na ndoano 18,450 na Mitumbwi 109 zenye thamani ya sh. Bilioni 2.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwaidi Mlolwa amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 26 (i) (ii) kinamtaka kila mtanzania kulinda rasilimali za nchi yetu ikiwemo samaki na mazao yake huku Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 zikikataza vitendo vya kutumia zana zisizoruhisiwa kwa mujibu wa sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Estomihn Chang’a alisema Serikali ya wilaya hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na uvuvi haramu na kuwachukulia hatua stahiki kuwataka wananchi kuendelea kuwafichua wavuvi haramu ili kulinda rasimali hiyo muhimu waliyopewa na Mungu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ukerewe , Frank Bahati alisema halmashauri imewasimamisha kazi watumishi watatu kwa tuhuma za kujihusisha na uvuvi haramu.Kwa upande wao baadhi ya wavuvi walimuomba Waziri Mpina kuwasiliana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage ili kuona namna ya kudhibiti nyavu zisizoruhusiwa kutengenezwa na kisha kuuziwa wavuvi.

By Jamhuri