Msumbiji na Tanzania, ukweli ni nchi ndugu tangu zama. Msumbiji tangu hizo zama ni sumbiji. Tanzania ni nchi mpya iliyoundwa kutokana na nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar.
Katika ukweli huo nchi hizo ndizo hasa ndugu wa Msumbiji. Ndipo ninapothubutu kusema Msumbiji na Tanzania ni ndugu tangu enzi na enzi.
Ingawa kwa miaka ipatayo mia tano Msumbiji ilitawaliwa na ukoloni wa Kireno, Tanganyika ilitamalakiwa  na ukoloni wa Kijerumani na wa Kiingereza kwa jumla ya miaka mia moja na kumi; na Zanzibar ilimilikiwa na ukoloni wa Kiarabu kwa takribani miaka mia moja na thelathini hivi; na bado, haikuondoa hali na mazingira ya mshikamano wa wananchi katika udugu na umoja wao.


Hata walipokuja hao wakoloni, wananchi waliendelea na shughuli zao mbalimbali chini ya mwavuli wa unasaba na ushirikiano katika biashara na tamaduni kwenye miji ya Unguja, Kilwa, Lindi na Mtwara kwa upande wa Tanzania na katika miji ya Chilimbo, Tete, Pemba na Sofala nchini Msumbiji.
Ndiyo maana hata wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Afrika haikuwa shida kwa wenyeji wa nchi hizo kuelewana, kuungana na kushirikiana pamoja katika kumkomboa Mwanamsumbiji.
Utamaduni wa biashara ulidumu na kuwawezesha wananchi wa pande mbili za Mto Ruvuma kujenga makazi ya kudumu. Leo jamii ya Wamakonde, Wamawia, Wamakua na hata Wayao wanapatikana nchini Msumbiji na Tanzania.


Ndiyo maana wakati wa harakati za ukombozi wa Msumbiji haikuwa shida kwa wenyeji wa nchi hizo kuelewana, kushirikiana na kuungana pamoja kudai Uhuru  wa Msumbiji.
Nakumbuka vyema enzi za miaka ya 1960-1970, Tanzania ilivyosaidia na ilivyosimamia mapambano dhidi ya ukoloni wa Kireno katika kumkomboa Mwanamsumbiji kutoka katika dahari za dhuluma, mateso na mauaji hadi kuweza kufanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa mwanamapinduzi na shupavu, Samora Machel (sasa ni marehemu).
Kuna msemo wa Kiswahili usemao, “Mja asili aachi asili.” Msemo huo umejidhihirisha hivi majuzi Watanzania tulipompokea na kumkaribisha kwa taadhima, Rais wa Msumbiji, Felipe Jacinto Nyusi, na kumtamkia, “Karibu nyumbani kwetu Tanzania.” Baada ya yeye kutaka kuja nchini kuzungumza na ndugu zake.


Yeye ndiye hasa aliyefanikisha msemo huo. Naye mkuu wetu wa nchi, Rais Dakta Jakaya Mrisho Kikwete, kwa tabia yake ya tabasamu na ucheshi; upole na upenzi; utu na ukarimu hakusita hata chembe kumpokea, kumkarimu na kumkaribisha ndani nyumbani.
Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma. Rais Nyusi alivinjari na kuzungumza na nduguze pale Chuo cha Diplomasia, Ikulu Zanzibar na bungeni Dodoma. Ukweli alijimwaga na kunena yake ya moyoni.
Alisema kuwa ziara yake nchini Tanzania ni kudhihirisha dhamira ya Serikali na wananchi wa Msumbiji, wanaendelea kuimarisha uhusiano uliopo na kuthamini udugu wao huku wakidumisha masuala ya kijamii ikiwemo biashara na uchumi.


Hakusita wala hakuwa na mashaka pale alipotamka hadharani ndani ya Bunge la Tanzania na kuwataka Waheshimiwa Wabunge waikabili vita dhidi ya ufisadi, rushwa na ugaidi; na wala wasichoke kupigana na adui umaskini. Alisisitiza kuwa ili nchi iweze kwenda mbele katika nyanja za kiuchumi na nyinginezo, ni kupambana na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
Kwa lugha yake mwenyewe kaonesha uhusiano wa asili uliopo kati ya Msumbiji na Tanzania. Rais Nyusi anasema, namnukuu, “Tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja na kuendeleza uhusiano wetu na kuungana pamoja kujifunza demokrasia tuliyonayo kati ya Msumbiji na Tanzania. Milango ipo wazi, Watanzania wanakuja Msumbiji wanakaa na wanafanya shughuli zao bila shida yoyote.” mwisho wa kunukuu.


Maelezo hayo ni ushahidi unaodhihirisha ukweli kwamba watu wa Msumbiji na watu wa Tanzania wana asili ya uhusiano na uelewano. Kutoa ridhaa kwa Watanzania kwenda Msumbiji kuishi na kufanya biashara si jambo la masihara hasa alipotamka kufuta viza kati ya nchi mbili hizo.
Naamini Rais Nyusi amesema hayo katika kutambua mchango uliotolewa na TANU kwa FRELIMO wakati wa harakati za kupambana na Wareno.
Maneno pacha ya hayo yaliyozungumzwa yametamkwa pia na Rais  Kikwete ambaye alisema kuwa vyama hivyo vina historia kubwa ya ushirikiano kutoka kwa waasisi wake. Kaulimbiu hizo zinaweka wazi thamani ya nchi mbili.hizo.


Thamani hiyo haikushuka kama mvua kutoka angani wala haikuletwa kama tenga la machungwa kutoka shambani. Imeandaliwa, imejengwa na imedumishwa toka kizazi na kizazi hadi leo hii tunaendelea kuvuna na kula matunda ya thamani ya Msumbiji na Tanzania.
Ni matazamio yangu kusikia na kuona Wanamsumbiji na Wanatanzania wanakaa pamoja kubuni na kupanga mipango himilivu kuhusu utalii, Utamaduni na uchumi kunusuru nchi mbili hizi zisirejee kwenye ukoloni mamboleo wala uchumi tegemezi.
Inawezekana timiza wajibu wako na Aluta Continue.

 
1694 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!