Kuishi miaka mingi ni kuona mengi pia – lakini yanaweza kuwa mema ama machungu kama shubiri, lakini bado ni mambo muhimu katika mapito ya maisha ili kuweza kujifunza kila kitu. Nimejifunza mengi sana hadi leo.

Nchi hii ni ya wakulima na wafanyakazi. Bado naamini hivyo kinadharia hata kama kwa sasa wameongezeka wanaoitwa wafanyabiashara. Najua kuwa hao ndiyo wameshika mpini lakini bado najipa matumaini kuwa ni yetu sisi wakulima na wafanyakazi.

 

Leo nimeamua kuwaandikia waraka huu kuwakumbusha kuwa nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi na si kama mnavyodhani na mlivyoamua. Najua hamtaki kuikubali dhana hiyo, lakini ndiyo ukweli wenyewe ambao utakuja dhihirika baada ya muda fulani wa mapito ya machungu kama yaliyotokea katika nchi kadhaa.

 

Wakati wiki jana mkisherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, nilijiuliza mambo mengi sana yaliyokuwa tofauti na enzi zetu za utumishi au uajiri, enzi zetu tulikuwa tukisherehekea kwa furaha na nyuso zetu zilionekana kujaa matumaini kwa kufanya kazi kwa bidii, ili kuleta maendeleo katika taifa masikini.

 

Ni vizuri nikawakumbusha wazee wenzangu na vijana wa leo, mkapata somo la ujinga la wakati huo. Sisi tulikuwa tukiandamana huku tukishindana kuonesha ufahari wa kile ambacho tumekitekeleza kwa mwaka mzima. Tulikuwa tukizungumzia mafanikio tuliyopata na kuvuka malengo, tulifanya hivyo na kuilazimisha serikali au mashirika kufikiria ni jinsi gani tunaweza kubadili mfumo wa mapato kwa mwaka unaofuata.

 

Tulikuwa tunajisikia fahari kuomba kupunguziwa mishahara ili kuongeza vitendea kazi bora na kuweza kuvuka malengo mapya tuliyojiwekea. Hatukujali mvua wala posho, hatukujali tumevaa nini au tutaahidiwa nini katika kilele cha sikukuu hiyo.

 

Julius hakuwa na kazi kubwa ya kufikiria siku hiyo atatwambia nini sisi wafanyakazi. Kazi kubwa aliyokuwa nayo ni kutueleza aliyoyaona kwa wenzetu na jinsi gani sisi tufanye kuwazidi wao tupate maendeleo mapema. Nakumbuka wakati fulani aliwahi kuombwa na wafanyakazi wa Wizara ya Afya kukatwa senti 20 ili kuboresha huduma za afya, alipokubali siku hiyo wafanyakazi hao walilipuka kwa furaha na nderemo kwamba ombi lao limekubaliwa japo kwa shingo upande.

 

Mtiririko ule uliendelea na Julius mwenyewe aliomba kukatwa shilingi 60 kutoka katika mshahara wake, ili ziingie katika mfuko mkuu wa serikali kuweza kusaidia maendeleo ya taifa. Miaka ya mwishoni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, naye aliomba kukatwa mshahara wake ili kusogeza gurudumu la maendeleo mbele.

 

Sisi ndiyo tuliokuwa wafanyakazi na hao ndiyo waliokuwa viongozi wetu. Kwa wakati ule mimi nilikuwa mfanyakazi nakimbiza kiberenge Reli ya Kati. Mshahara wangu ulikuwa mkubwa kwa maana ya kupata fedha zinazoweza kukidhi haja ya matumizi kwa mwezi mzima na nikawa na bakaa kidogo, tuliweza kufanya hivyo kwa sababu nyingi za Ujamaa na Kujitegemea.

 

Tulikuwa na shule zetu ambazo hazikuwa na ada lakini walimu wazuri na watoto ambao ndiyo nyie mnafaulu, tulikuwa na kitu kinachoitwa waranti ambazo mlikuwa mnapewa na kusafirishwa na serikali kwa kutumia mabasi yetu, treni zetu, meli zetu na ndege zetu. Sisi wazazi wenu tulikuwa hatuna mawazo na masomo yenu, tulichapa kazi tu.

 

Tulikuwa na hospitali na zahanati bora ambazo hazikuwa na gharama kumuona daktari, tuliwaandaa matabibu kwa viwango mbalimbali kama ilivyokuwa katika elimu, tulikuwa na chanjo za kitaifa, miradi ya afya ya kitaifa, dawa zilizotengenezwa na wazalendo ndani ya nchi yetu na sisi ndiyo tulioandamana Mei Mosi kusherehekea sikukuu yetu.

 

Hii ndiyo ilikuwa Mei Mosi ambayo haikuwa na posho wala sare, lakini yenye matumaini ya kweli, yenye uchumi imara wa ndani, yenye changamoto zinazotatulika, isiyo na hasira ya wafanyakazi kudai nyongeza ya mishahara wala posho, isiyo na risala za masikitiko na mfumko wa bei, iliyojaa wafanyakazi wa kweli na si wanasiasa na wafanyabiashara, sherehe ya wazalendo kwa taifa lao na si mafisadi.

 

Nimeishi miaka mingi, Mei Mosi ni moja kati ya vituko ninavyoshuhudia kutokea Tanzania. Kituko kingine ni Siku ya Wakulima yaani Sabasaba ambayo kimsingi tunafanyiwa na wageni na si sisi Watanzania, Siku ya Mashujaa inazidi kunichanganya.

 

Sisi tulikuwa tunajitolea mishahara yetu ikatwe, wenzetu leo mnadai miposho na mishahara ipande. Mnawaomba wafanyabiashara na si serikali yenu ambayo ilikuwa inatoa fursa ya ajira, kwa kuwa mabadiliko ya kimaendeleo mliyoona yanafaa ni uwekezaji ambao umeua viwanda na taasisi nyingi za serikali ambazo zilikuwa zikitoa ajira.

 

Anzeni kwa kuomba kukatwa mishahara ili mpitie marekebisho ya malumbamo. Tulipita na kuweza kuomba kukatwa mahela ya mishahara.

 

Wasalaam

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1051 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!