Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis Van Gaal hana amani tena katika timu hiyo.

Amezungumza mambo mawili ambayo yamemshtua wikiendi iliyopita.

Jambo la kwanza, ni kuthibitishwa na watu wake wa karibu kwamba Kocha machachari, Jose Mourinho ameteta na uongozi wa timu hiyo.

Kadhalika, matokeo ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Sundeland ambako Mashetani Wekundu hao, walilala kwa mabao 2-1 Jumamosi iliyopita.

Van Gaal, raia wa Uholanzi, anasema hadharani kuwa ameshtuka kwa matukio hayo.

Amesema kuwa anakata tamaa na amesikitika akiwa bado anaio ngoza timu hiyo, mara moja anathibitishiwa taarifa juu ya uongozi wa Manchester United kufanya mazungumzo na Mourinho.

Japo Manchester United haijatoa tamko lolote baada ya ripoti hizo, lakini Van Gaal anadai, mazungumzo hayo yamefanyika.

Taarifa zinasema kwamba maofisa wa klabu hiyo maarufu kama Mashetani Wekundu, walifanya mazungumzo na Mourinho kadhalika wawakilishi wake na kocha huyo wa zamani wa Chelsea.

Akihojiwa iwapo anafikiri kulikuwa na mazungumzo, Van Gaal anasema: “Katika soka hilo linawezekana, lakini nimesikitika.

“Inauma, kwa sababu viongozi hawajaniambia lolote. Lakini, mwanzoni sikudhani kama kulikuwa na mazungumzo.”

Van Gaal anayeinoa timu hiyo kwa msimu wa pili sasa, anasema ana uhusiano mzuri na Mkurugenzi Mkuu wa United, Ed Woodward na mmiliki Glazers.

“Kwa  ukaribu kati yangu na Ed Woodward pamoja na Glazers, sikutarajia kama wangekaa kimya. Wangeniambia tu, lakini sijui kwanini?” alihoji kocha huyo.

Manchester United kwa sasa haishiriki michuano yoyote mikubwa kama vile Ligi ya Mabingwa Ulaya wala ile ya Uropa baada ya kufanya vibaya katika mechi za awali.

Katika Ligi Kuu ya England, timu hiyo ambayo inamsaka Mourinho inashika nafasi ya tano katika msimamo ikiwa pointi sita nyuma ya Manchester City ambao wako katika nafasi ya nne.

Alianza kuinoa timu hiyo mwaka 2014 na kuiongoza United katika nafasi ya nne msimu uliopita na walikubaliana na uongozi wa United kufanya vema zaidi msimu huu.

Sunderland ambayo inapigania nafasi ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao, ikaitia doa tena United Jumamosi iliyopita kwa kuichapa mabao 2-1, kipigo ambacho Van Gaal anakitafsiri kuwa ni mbinu mbaya za wachezaji.

“Wachezaji wameniangusha, sijui nia yao,” anasema Van Gaal katika mchezo huo ambako timu yake ilianza kufungwa kwa bao la Wahbi Khazri dakika ya tatu kutokana na mpira wa adhabu uliompita kila mtu katika lango hilo.

Anthony Martial alisawazisha United baada ya kuugusa mpira uliompita kipa Victor Manone, ambaye awali alikuwa ameokoa shambulizi la Juan Marta.

Lakini Sunderland walishinda mechi hiyo baada ya kichwa cha Lamine Kone kutokana na krosi safi iliopigwa na Khazri aliyeonekana kuwa mwiba mchungu kwa United.

Tayari Mourinho, amewaeleza rafiki zake wa karibu kwamba amemalizana na Manchester United, hivyo ataanza kuitumikia wakati wa majira ya joto mwaka huu.

Kocha huyo amekuwa nje ya uwanja tangu alipofukuzwa Chelsea, Desemba mwaka jana, lakini wiki iliyopita aliweka wazi kwamba amechoka kukaa bila kuifundisha timu hivyo yupo mbioni kurudi viwanjani.

Mourinho amedai kwamba kila kitu kimekamilika hivyo atachukua nafasi ya kocha Van Gaal. Hata hivyo, Van Gaal bado ana mkataba wa mwaka mmoja katika klabu hiyo ya United.

By Jamhuri