“Mheshimiwa Mwenyekiti, usipopeleka mwanao shule, utashitakiwa. Lakini mtoto akipata kazi, wewe hakutumii hela, hauwezi kumshitaki. Hauruhusiwi kwenda polisi kulalamika, hauruhusiwi kwenda dawati la jamii. Haiwezekani.

“Mzazi anaposomesha mtoto wake, anapomwomba pesa au anapopiga simu, watoto hawapokei. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara ya Elimu na Wizara ya Ustawi wa Jamii watuletee sheria hapa ili mtoto asipopokea simu, hakutoa pesa, mimi niende Polisi ili nipate ‘Police Order’ anitumie pesa”. Mwisho wa nukuu.

Ni baadhi ya maelezo ya Mbunge wa Kahama Mjini,  Jumanne Kishimba, alipotoa hoja yake katika Bunge lililopita. Ukweli ni fikra yenye mashiko na kutoa changamoto kwa watoto dhidi ya wazazi wao.

Ipo dalili ya watoto (vijana) baada ya kumaliza masomo yao – iwe shuleni au chuoni, kupuuza na wakati mwingine kudharau au kutojali kutoa huduma kwa wazazi wao. 

Wanasahau haki, thamani na mapenzi ya wazazi wao kwao. Baadhi yao wanadhani wazazi hawana tena faida katika jamii na taifa.

Watoto hawa wanaeleza, eti wazazi walitumia wakati wao; na sasa ni muda wao kufanya watakavyo! Ni sahihi na kweli wazazi walifanya kikirikakara mitaani. Lakini enzi hizo za patashika mijini na vijijini bado waliwatunza, waliwalea, waliwaelimisha na kuwalinda wasipate maradhi na maafa katika maisha yao kutoka kwa watu wenye husuda.

Akijenga hoja yake na kusisitiza bungeni, Kishimba anasema: “Tunaomba Mhe. Waziri wa Elimu leta humu muswada. Mbona wanapofika ‘form six’ wewe unakopesha unawawekea na riba, wanapopata kazi unawakata, mimi mzazi ninakosa gani kumdai mwanangu?”

Profesa Kishimba anafafanua: “Wazazi tunahangaika kweli majimboni. Wazazi wanakwenda TASAF, mtoto yupo Dar es Salaam, wanayo maisha mazuri. Kila siku unasikia ana ‘birthday’. Mzazi aliyetumia ng’ombe nyingi sana kumsomesha mtoto anateseka.”

Anaendelea kusema: “Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zoezi hili serikali wameanza wao wenyewe, ruhusu na wazazi ili mtu anaposomesha shule, mjue na mimi kwamba nina ‘invest’ kuliko hivi naambiwa kwamba elimu unayomwachia ni urithi wa kwako wewe.” Mwisho wa kunukuu.

Uwezo wake mtoto wa kufikiri na kutambua mambo na maarifa aliyonayo kumpa nguvu na ujasiri kuwa tajiri au udhaifu na uzembe anaoukumbatia kumpa ulofa hauondoi sifa yake ya kuwa mtoto kwa wazazi wala haiondoi haki na mapenzi ya wazazi kwake, na wazazi hawatamkataa kwamba si mtoto wao.

Ndipo Mhe. Kishimba anasema: “Kwa nini wazazi tujiandae kutoa radhi? Kwa nini niandae kulalamika na kutoa radhi? Kwa nini serikali isitusaidie? Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo hapa?”

Anaendelea kusema: “Kwa nini nijiandae kuja kutoa radhi badala ya serikali kunisaidia sheria ndogo ili mtoto asipopokea simu, hakutoa pesa, mimi niende Polisi ili apate ‘Police Order’, anitumie pesa?

“Sasa urithi gani Mhe. Mwenyekiti, huyu anapata maendeleo yake, wewe unabaki unazubaa kijijini hauna chochote. Mheshimiwa Mwenyekiti maneno haya tunaongea kama mzaha, lakini wazee kule vijijini wana shida nyingi sana.” Mwisho wa kumnukuu Kishimba, Mbunge wa Kahama Mjini.

Serikali pamoja na kuweka Sera ya Mtoto na Sera ya Vijana kwa maana ya makundi haya ni ya taifa letu, ieleweke pia wazazi (wazee) nao ni sehemu ya taifa. Vipi kundi moja linapewa haki na stahiki muhimu na kundi jingine kutopewa haki na stahiki muhimu?

Kutokana na maelezo haya, watoto hawana budi nao sasa kutambua, kuelewa, kuthamini, kulea na kutunza wazazi wao. Vitabu vya dini vinazungumzia thamani, haki na stahiki zao. Wazazi sasa hawana nguvu za kuhemea mahitaji yao. Wanahitaji sana malipo waliyowekeza kwa watoto wao.

Hii ni hoja muhimu mno, inahitaji mijadala hai na mipana – iwe katika maskani, vijiweni, mitandaoni, kwenye jumuiya mbalimbali, asasi za kijamii na vyombo vya habari.

Serikali iandae muswada na Bunge lijadili na kuweka sheria. Tukumbuke na tuseme: “Tuwashukuru wazazi.”

703 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!