Kujisaili na Kujisahihisha: Mafunzo ya Watu wa Cuba juu ya Kutupwa kwa Azimio la Arusha

“Ujamaa utabaki kuwa tumaini na njia pekee kwa wanyonge kujikomboa. Leo, wakati maadui wa Ujamaa wakieneza propaganda dhidi ya Ujamaa, tunapaswa kuulinda na kuutetea zaidi Ujamaa kuliko wakati mwingine wowote ule,” Fidel Castro Ruiz, 1989

Cuba ni kisiwa mashuhuri ulimwenguni, zaidi ni nchi mashuhuri na ya fahari mno kwa wajamaa wote ulimwenguni. July 26, 1959 viongozi wa Kijamaa wa Cuba walifanya mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Rais Baptista, na kuitangaza Cuba kuwa taifa la kwanza la Kijamaa huko Amerika ya Kusini.

Njia zote kuu za uchumi wa taifa hilo zikawekwa kwa umma chini ya usimamizi wa dola, umma wa wanyonge wa Cuba kwa pamoja ukakubaliana kujenga taifa lenye usawa na linalothamini utu wa kila mmoja wao, wakulima wa miwa vijijini wakishirikiana na wafanyakazi wa viwandani mjini kuleta maendeleo ya taifa lao.

Miaka 25 ya Mapinduzi ya Cuba ilileta mafanikio makubwa ya kiutu ulimwenguni, yakiliwezesha taifa hilo kujitegemea katika kila nyanja, likifuta ujinga kwa takribani asilimia 95, likiweza kujitegemea kwa chakula, na likiwa mbele ulimwenguni katika mapinduzi ya sekta ya afya – sekta ya fahari zaidi kwa nchi hiyo. 

Sera ya nje ya taifa hilo nayo ilizaa matunda mno, likisaidia harakati za mapambano ya uhuru katika nchi mbalimbali za bara la Afrika, ikipeleka na wapiganaji katika mataifa kadhaa ya Afrika.

Mafanikio hayo ya Cuba kiuchumi na kisiasa, ndani na nje ya Cuba, yalikuwa pia na changamoto zake nyingi katika miaka 25 ya kutekeleza sera za Kijamaa.

Uhaba wa nyumba za umma za kuishi ulikuwa mkubwa, hasa mji mkuu wa Havana, uhaba wa chakula na kupanda kwa bei za chakula kulikotokana na urasimu na ufisadi wa maofisa wa serikali waliohusika na usambazaji wa chakula nchini humo likawa jambo la kawaida, upendeleo jeshini na utaratibu wa kupeana kazi kwa kupendeleana ukatamalaki.

Msingi mkuu wa Mapinduzi ya Cuba ulijengwa juu ya wananchi kujitolea, miaka 25 baada ya Mapinduzi morali wa watu wa Cuba kujitolea ulishuka sana, hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, hata sekta ya fahari ya afya ikaanza kulegalega, kukawa na ucheleweshwaji au upungufu wa ujenzi wa vituo vipya vya afya na pia kuvunjika moyo kwa matabibu kulikotokana na sababu mbalimbali za kiutawala.

Haja ya kujisaili na kujisahihisha ikajionesha, tathmini iliyofanyika juu ya usahihi na upungufu wa sera za Kijamaa za nchi hiyo mwaka 1984 ilisaidia mno kuainisha matatizo hayo. 

Mwaka 1986 mpango maalumu wa serikali wa ‘Kujisahihisha’ ukaanza, ukihusisha kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya uongozi kwa zaidi ya asilimia 50 ya Chama cha Kijamaa cha Cuba pamoja na serikali, mabadiliko ambayo yalihusisha kuleta nguvu mpya ya vijana, wanawake na Wacuba weusi.

Mabadiliko hayo hayakuishia hapo, yalihusisha pia kukata minyororo ya urasimu na ufisadi, kutoa motisha na morali kwa wafanyakazi, kupeleka sehemu kubwa ya fedha za umma katika miradi yenye kuzalisha ajira zaidi, kuchochea uzalishaji na kuhamasisha watu kujitolea – msingi mkuu wa Mapinduzi ya Cuba.

Wakati Cuba wakifanya hayo nchini mwetu Tanzania tulikuwa na matatizo kama yao tu. Mwaka 1967 tulitangaza Azimio La Arusha, mwongozo wa kiuchumi na kisiasa uliotoa matumaini na matarajio mapya kwa tabaka la wafanyakazi na wavuja jasho wengine. 

Azimio liliongea lugha ya ukombozi wa wanyonge, likanadi usawa wa kiutu, likapinga unyonyaji wa mtu na mtu au kundi moja kulinyonya jingine, na likaweka miiko ya uongozi ili kuwazuia “kisheria” viongozi kutumia nafasi za uongozi kujilimbikizia mali wao binafsi na familia zao.

Azimio lilileta mafanikio makubwa sana nchini, kama ilivyo Cuba lilihakikisha njia kuu za uchumi zinashikwa na umma kupitia dola, likafuta ada kwa ngazi zote za elimu nchini – msingi kwa ajili ya mpango wa elimu kwa wote (UPE). Mpaka mwaka 1982 kila kijiji kilikuwa na shule yake ya msingi nchini, watoto wote wakipata fursa ya kusoma bila kujali hali zao.

Ilipofika mwaka 1984 idadi ya watoto walioandikishwa ikaongezeka zaidi, zaidi ya asilimia 90 ya watoto wakawa wanahudhuria shuleni, asilimia 95 ya watu wazima wakawa wanajua kusoma na kuandika. Mafanikio makubwa mno kwa wakati husika.

Katika kipindi hiki cha Azimio, pia Serikali ilijenga viwanda mbalimbali, hususan viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo kama vile viwanda vya nguo ikiwamo viwanda vya kuchambua pamba, viwanda vya nyuzi na nguo. Jumla ya viwanda 12 vya nguo vilijengwa nchini na kuzalisha maelfu ya ajira kwa wananchi. 

Serikali pia ilianzisha viwanda vya ngozi, vya kubangua korosho, vya kuzalisha sukari, vya kubangua na kusaga kahawa, vya kamba za katani na magunia ya katani na kadhalika. Serikali pia ilijenga viwanda vikubwa viwili vya kutengeneza vipuri.

Kulikuwa na mafanikio makubwa pia kwenye sera zetu za nje, tukiwa kituo kikuu cha mapambano ya kupigania uhuru wa nchi za Afrika, ‘Kamati ya Ukombozi wa Africa’ (Liberation Committee) ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ikiongozwa na Watanzania Sebastian Chale, George Magombe na Hashimu Idd Mbita, majeshi yetu yakipambana Msumbiji, Namibia na Angola. 

Tukiufunga Ubalozi wa Israel na kufungua Ubalozi wa Palestina nchini, tukiwa watetezi wakuu wa nchi za Sahara Magharibi na tukisimama kidete kuwatetea ndugu zetu wa China kule UNO. Kama ilivyokuwa kwa Cuba, Taifa letu likawa sauti ya kila mnyonge ulimwenguni.

Pamoja na kutoa matumaini na kuleta mafanikio yote haya, Azimio lilikuwa na upungufu wake, badala ya kuwainua utekelezwaji wake uliwabinya wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi vikafanywa dhaifu chini ya dola, utekelezwaje wake ukaachwa chini ya warasimu wa Serikali ambao hawakuamini kwenye Ujamaa, miradi na sera za kijamii kutungwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.

Kufa kwa viwanda na mashirika kulikotokana na sababu mbalimbali pamoja na ufisadi, kushuka kwa huduma za kijamii (elimu, afya, chakula n.k) kulikotokana na athari za vita ya Kagera na kusitishwa kwa misaada ya ufadhili wa mashirika ya kigeni katikati ya miaka ya 1980.

Mwaka 1971 Chama cha TANU kilitoa mwongozo kujaribu kupunguza baadhi ya upungufu wa Azimio, tathmini ndogo ilifanyika pia iliyosaidia kutoa mwongozo mwingine wa mwaka 1982. Lakini kwa kiasi kikubwa miongozo miwili hiyo haikutekelezwa mpaka Mwalimu Nyerere alipong’atuka madarakani mwaka 1985. 

Kuanzia mwaka 1992 Tanzania ilianza kuvunjavunja misingi ya Azimio la Arusha na kurudi miaka 25 nyuma. Kimsingi, uvunjaji ulianza kidogo kidogo kuanzia mwaka 1986 na ndiyo maana mwaka 1987 hapakuwa na tathmini iliyo wazi ya Azimio kama ilivyokuwa mwaka 1977. 

Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa mwaka huu wa 2017 tunaadhimisha miaka 50 ya Azimio la Arusha kwa kufanya tathmini ya miaka 25 ya utekelezaji wa Azimio na miaka 25 ya kutupwa kwa Azimio. Nafurahi kuwa chama chetu cha ACT-Wazalendo kimetangaza kufanya maadhimisho hayo Machi 25 jijini Arusha, ni fursa muhimu kwetu vijana kujadili mustakabali wa nchi yetu.

Muhimu: Mwandishi ni Katibu wa Mambo ya Nje wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo.

1510 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!