Aprili 8 mwaka huu, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo (pichani kulia), amezungumzia matatizo ya elimu yaliyoikumba Tanzania.

Akizindua tovuti ya elimu katika hafla iliyofanyika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Mulugo amesema anashangazwa na baadhi ya watu na wanasiasa kutaka yeye na waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, wajiuzulu nafasi zao kutokana na matokeo mabaya ya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2012. Mulugo amedai kuondoka kwao katika nafasi hizo si suluhisho la kuendelea kuanguka au kuinua kiwango cha elimu nchini, bali kinachotakiwa ni wananchi kushirikiana na Serikali.


Nataka, kwanza kabisa, kumhakikishia Mulugo kwamba kuondoka kwao Wizara ya Elimu, yeye na Dk. Kawambwa, litakuwa suluhisho kubwa katika kuinua kiwango cha elimu Tanzania.

 

Binafsi ni miongoni mwa watu wachache wasiokubaliana na madai kwamba maendeleo duni ya elimu yaliyopo leo Tanzania,  ni matokeo ya mfumo wa elimu tulionao. Hapana. Ni matokeo ya usimamizi mbovu wa elimu usioendana na uzalendo na usiojali maskini wa Tanzania.

 

Yote haya ni kwa sababu watoto wa wakubwa hawasomi shule za umma, na wana hakika ya kupata ajira baada ya kuhitimu masomo.


Kwa hivyo, kuondoka kwa viongozi hao wawili wakuu wa elimu, kunaweza kusaidia kupatikana kwa viongozi wazalendo na wenye uchungu na watoto wa maskini.


Chukua, kwa mfano, somo la stadi za kazi. Kushindwa kufanikiwa kwa somo hilo katika shule zetu hakuhusiani hata kidogo na mfumo wa elimu. Kunahusiana na usimamizi mbovu wa somo hilo.

 

Somo la stadi za kazi ni la ufundi lililokusudiwa kupunguza kama si kumaliza tatizo la ajira Tanzania. Lilikusudiwa kuzalisha wajasiriamali kutokana na wanafunzi wanaorudi nyumbani baada ya kumaliza elimu ya msingi.

 

Kilichotakiwa katika kusimamia somo hili, ni wizara kuhakikisha kwamba kila shule ina mwalimu wa somo la stadi za kazi aliyepewa mafunzo, na pia kwamba somo lina vitendea kazi. Badala yake tulichoshuhudia ni wizara kujaza shuleni vitabu tu vya stadi za kazi ambavyo havitumiki, ila kwa sababu tu utitiri wa vitabu hivyo unanufaisha walioko wizarani.


Halafu, Mulugo anadai bila kuona aibu kwamba matatizo ya elimu yatamalizika nchini kwa wananchi kushirikiana na Serikali. Anataka kutuambia chimbuko lote la matatizo ya elimu ni wananchi kutoshirikiana na Serikali. Uzushi mtupu!


Chimbuko la matatizo yote ya elimu Tanzania, ni viongozi wa wizara kuendesha elimu kibabe bila kuwashirikisha walimu – achilia mbali wananchi.

 

Kila siku walimu wanapiga kelele kuhusu vitabu visivyofaa vilivyopo shuleni. Lakini hivi sasa viongozi wa wizara wameruhusu mamilioni ya fedha za rada yatumike kuchapisha vitabu ambavyo walimu wameona siku nyingi kwamba havifai. Na hawakwenda kutafuta maoni ya walimu kuhusu vitabu hivyo kabla hawajaagiza vichapishwe upya ilimradi wao wapate asilimia kumi yao.

 

Kinachosisitizwa hapa ni ukweli kwamba Mulugo, Dk. Kawambwa na wote walio chini yao wizarani wameshindwa kusimamia elimu. Kwa kuwa wenyewe hawawezi kujiondoa, Rais awaondoe.


1039 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!