Museveni: Waafrika hatujui kuomba

“Tatizo letu sisi Waafrika hatujui kuomba, na hata tunapopata fursa ya kuomba hatuombi kwa akili. Nilipokwenda kwa Gaddafi [wakati napigana vita ya kumuondoa Idi Amin) aliniuliza ‘Nikupe pesa?’ Nikasema hapana. Akasema ‘Nikupe sare za askari?’ Nikamwambia hapana. Akasema ‘Unataka nini sasa kwangu?’ Nikamwambia bunduki na risasi.”

Maneno haya aliyasema Yoweri Kaguta Museveni Novemba 31, 1999 wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki inafufuliwa. Aliwaambia marais Ali Hassan Mwinyi wa Tanzania na Daniel arap Moi wa Kenya kuwa viongozi wengi wa Afrika wakipata fursa ya kuomba wanaomba chupi za watoto badala ya kuomba miradi ya maendeleo.

********

 

Merkel: Ujerumaini watu wanaikimbia

“Kwa miaka michache iliyopita, watu wengi wamekuwa wakiondoka katika nchi yetu kuliko wanavyoingia. Kwa njia yoyote, yatupasa kupunguza vizuizi vya kuingia kwa wale wenye fursa ya kuipeleka mbele nchi yetu.”

Kauli hii ameitoa Kansela wa Ujerumani hivi karibuni Bi. Angela Merkel, baada ya kushuhudia taifa la Ujerumani na mataifa mwengine ya Ulaya yakikaza kamba kufukuza wanaowaita wahamiaji, kitu alichosema wapo wahamiaji wenye tija.

************

 

Kennedy: Mawazo hayafi milele

“Mwanadamu anaweza kufariki dunia, taifa linaweza kujengeka na kuangula, lakini milele mawazo huishi.”

 

Haya ni maneno ya Rais wa zamani wa Marekani, John Fitlzgerald Kennedy, aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwaka 1963. Kennedy alikuwa akipingana na mfumo wa ubepari. Kifo chake hadi leo kina utata mkubwa nchini Marekani.

******

 

Ravalomanana: Demokrasia ifuatwe

“Sitajiuzulu kamwe. Tunapaswa kufuata mkondo wa kidemokrasia [kuniondoa madarakani].”

 

Haya yalikuwa maneno ya Rais wa Madagascar, Marc Ravalomanana, baada ya mambo kumchachia alipokabwa koo na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Andry Rajoelina, mwaka 2009. Rajoelina alikuwa DJ. La ajabu, Ravalomanana naye aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi akitumia nguvu ya umma kumwondoa madarakani Didier Ratsiraka mwaka 2002 bila kufuata mkondo wa demokrasia. Ratsiraka alikuwa madarakani tangu 1975.