Mussa Azzan Zungu Achanganyikiwa na Hoja ya Mbunge wa Chadema

Mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan Zungu amejichanganya wakati wa kutoa majibu ya kura ya uamuzi na kufanya wabunge wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani kulipuka kwa furaha kwa kupiga makofi.

Hilo limetokea wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya Bunge zima kupitisha Muswada wa sheria ya bodi ya Kitaalam ya Walimu kwa mwaka 2018 bungeni leo Septemba 5 2018.

Zungu amejichanganya wakati wa kutoa matokeo ya kura za uamuzi kuhusu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Suzan Lyimo ambaye alitaka muswada huo kuainisha sifa za mwenyekiti wa bodi hiyo.

Suzan amesema kuwa ni vyema muswada huo ukaainisha sifa za kuwa mwanataaluma mwandamizi ili kuepusha mtu ambaye hana uzoefu katika kazi ya ualimu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa bodi.

Kwa mujibu wa mapendekezo yake muswada huo uweke kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo awe na uzoefu wa miaka 10.

Baada ya wabunge kupewa nafasi ya kujadili hoja hiyo, Zungu aliwahoji wabunge akisema:

“Wanaoafiki hoja ya Susan Lyimo waseme ndiyo, kisha akauliza wanaopinga hoja ya Lyimo waseme ndiyo pande zote zilisikika zikisema ndiyo kwa sauti za juu.

Baada ya hapo wabunge wa upande wa upinzani walianza kugonga meza na kushangilia huku wabunge wengine wakiwa kimya ndipo makatibu wakamkumbusha Zungu na akabadili uamuzi.

“Mie ni binadamu hoja ya Lyimo imekataliwa,”akasema baada ya kushtuliwa na makatibu.