Ipo methali moja ya Kiswahili isemayo, “Usipoziba ufa utajenga ukuta”. Methali hii ina fundisho kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku.

Ufa ni dosari ndogo katika jengo, lakini ukiachiliwa utasambaratisha jengo zima, hata kulazimika kulibomoa ili kujenga upya. Hapo gharama za huo ujenzi inakuwa kubwa sana. Kumbe kama mara pale ufa ulipoonekana, mwenye jengo angeuziba, basi asingeliingia katika gharama ile ya kujenga upya ukuta mzima.


Hii kwetu sisi Watanzania inaanza kuonekana siku hizi. Tulipoungana Tanganyika na Zanzibar zilionekana kero chache katika Muungano wetu. Lakini ipo tabia iliyojengeka hapa nchini nayo ni ile ya kutokujali KUREKEBISHA ubovu uliopo mara unapotokea, na kwa lugha ya Kiswahili hakuna tabia ya ukarabati bali tuna utamaduni wa kitu kikiharibika – tupilia mbali, nunua kipya.


Wazungu au watu waliostaarabika wana utamaduni wa kurekebisha ubovu na kwa neno la Kiingereza wanasema “repair”. Sisi leo hii tunaona faida ya ukarabati. Tabia ile ya kuzembea dosari zinazojitokeza (au kero) tunaichelea sana hapa Tanzania na matokeo yake inakuja kutugharimu sana katika uchumi wetu.


Hivyo basi, kwa kuachilia zile kero chache zilizokuwa zikionekana pale miaka ya mwanzoni mwanzoni mwa Muungano wetu, sasa kero zile zimekuwa kubwa kama donda ndugu – kila mwananchi anazisikia kwa matokeo yake, ndiyo sababu leo hii Wazanzibari wanadai uhuru wa nchi yao na kudai wanamezwa na Tanganyika. Wanataka utambulisho (identity) wao kama Wazanzibari. Suala la mafuta ni kisingizio tu.


Lakini tujiulize kwa nini walianza kudai bendera yao kule Zanzibar, likaja dai la wimbo wao wa Taifa? Mimi nakumbuka nilipokuwa nafanya kazi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) (1978-1980), Mheshimiwa Aboud Jumbe alikuwa akisema mara kwa mara kuwa yeye ni Rais wa nchi, mbona hana ndege yake? Na kweli ilinunuliwa (sijui kama ndege ile bado ipo). Sasa kwa nini wenzetu hawa wanadai sana Uzanzibari?


Labda ni vizuri sote tukatazama historia ya Visiwani. Jambo la kutia moyo wakati huu ni mshikamano unaoonekana kule Visiwani kwa hii Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa kuangalia lile kongamano lililoendeshwa Jumamosi, Oktoba 6, 2012 katika Hoteli kongwe ya Bwawani, inadhihirika wazi kuwa Umoja wa Kitaifa ndiyo suluhisho la kudumu kwa amani na usalama Visiwani.


Kongamano lenyewe chini ya uenyekiti wa Profesa Abdul Sherrif, liliandaliwa hasa na Kamati ya Maridhiano chini ya Mwenyekiti Mzee Hassan Nassor Moyo.


Aidha, baadhi ya washiriki kutoka CCM na CUF kama waheshimiwa Mansour Yusuf Himid, Eddy Riyani, Abdubakar Khamisi Bakari, Salim Bimani na Ismail Jussa Ladhu ni uthibitisho tosha kuwa mshikamano na umoja wa Wazanzibari umesilibwa Visiwani.


Hakukuwa na maoni ya kukinzana katika maudhui. Aidha, ule ushiriki wa watu wa itikadi tofauti za kisiasa, kwa umoja wao wote walizungumzia UZALENDO wa WAZANZIBARI. Kufurika kwa watu katika kongamano lile, hasa vijana, kulidhihirisha kuwa maridhiano ndiyo yaliyowezesha pakapatikana hali ya amani na utulivu Zanzibar.


Hii ni njia ya kusonga mbele (the way forward) na kusahau chuki na majeraha ya zamani kutokana na upinzani wa kisiasa. (Wale wasomaji wa makala nadhani waliyaona haya katika Raia Mwema toleo la tarehe 10 Oktoba 2012 ukurasa wa 10 makala ya Ahmed Rajabu). Tunajua kabisa kuwa kila mwamba ngoma huvutia kwake. Hivi ndivyo Mwarabu anapoelezea historia ya Zanzibar.


Ataelezea kuonesha alivyoanza kufika Zanzibar na mimi Mbantu nikielezea historia ya Zanzibar nitaipamba kivyangu kuwa ni nchi ya Kiafrika, tena ya Wabantu. Katika kitabu cha Sheikh Issa Bin Nasser Al-Ismaily anasema hivi namnukuu “…tunaona kutokana na taarikhi za kale kwamba Waarabu waliishi na kutamakani kwa biashara na maingiliano ya ndoa na ndugu zao wa Pwani ya Afrika Mashariki kwa maelfu ya miaka huko nyuma.”


Basi, udugu baina ya Waarabu hasa wa Yemen na Oman na watu wa Zanzibar ya leo na Pwani ya Afrika Mashariki, ni udugu wa maumbile wenye mizizi ya taarikhi yaendayo nyuma kwa dahari ya miaka. Na anaonya uhusiano na udugu huo yeyote yule atakayejaribu kuuvunja hataweza kufuzu (tazama ZANZIBAR: Kinyang’anyiro na utumwa ukurasa wa 1 kabisa kwenye pongezi na shukrani).


Swali la kawaida hapa ni kumuuliza huyu Mwarabu, hiyo biashara Waarabu hao waliifanya na nani? Si na wenyeji wa nchi hii? Hawa wenyeji si ndiyo waliooana na hao Waarabu? Sasa hawa wenyeji ndiyo WAAFRIKA WANANCHI WA ASILI wa mwambao na visiwani Unguja na Pemba.


Hapo ni dhahiri Mwarabu hakuwa wa kwanza kukalia ardhi hii ya mwambao wala ya kule visiwani. Basi, wazo kuwa Waarabu ndiyo wenyeji wa Visiwani ni mawazo ya kipuuzi. Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa na wakazi wa asili – wana wa Afrika – ndipo Mwarabu akaweza kufanya biashara na hata kuoana na kuzaliana nao kukatokea watu tunaowaita WASWAHILI, ambao ni machotara wa Waarabu na Waafrika wananchi wa hii Zanzibar.


Umekuja UAMSHO. Huu umetokea tu ghafla na kudai haki ya Wazanzibari kuwa na nchi yao na Taifa lao nje ya Muungano.


Wana-uamsho wamekuja na gea kubwa ya kudai Zanzibar itambulike kama nchi na wala si sehemu ya Muungano tena. Basi, panapotokea hoja kadhaa kuonesha dhahiri kutokuridhika na namna Muungano unavyoendeshwa, ndiyo wakati mwafaka kutafutiwa njia za kuona nini kinachosababisha yote haya hadi kufikia watu wa nchi moja kuzungumzia kuvunja Muungano?


Huu Uamsho kadri nisomavyo kutoka magazeti mbalimbali (Nipashe toleo la Jumapili, Novemba 4-10, 2012 uk. 29. “Iundwe Tume kuchunguza mtandao wa Uamsho” na Mzalendo toleo Na. 2663 la Jumapili, Novemba 4-10, 2012 uk. 23 “Uamsho imetuamsha?) unaelekea kuwa na sura mbili. Moja ni ya udini; kugangamalia Uislamu eti ndiyo sababu ya wao kutaka kutoka kwenye Muungano, ya pili ni ukabila, kwa maana ya watu wenye asili ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara eti ndiyo maana wanataka Muungano uvunjike.

Itaendelea


Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).

By Jamhuri