Ukweli ni kwamba Wazanzibari wengi zaidi ni watu wa mchanganyiko wa damu mbalimbali -mtu wa rangi yoyote anaweza kuwa Mzanzibari- ni hivi ndivyo vilivyo hivi sasa.

La muhimu ni kwamba mtu huyo amepata uzanzibari wake kwa njia ya halali na kwa kufuata sharia za nchi kuhusu uananchi wa Zanzibar.


Na ukishakuwa Mzanzibari ukubali kwamba hali yako na ile ya Mzanzibari mwingine ni sawa sawa, yaani hakuna Mzanzibari asili au mgeni, hakuna Mzanzibari wa Visiwani au wa Bara au wa Ulaya, au wa Arabuni. Uzanzibar hautaki ukabila, mbaguano au mtengano.


(Haya ni maneno niliyoona kutoka kwa maandishi ya Sheikh Issa bin Nasser Al-Ismaily – katika kitabu chake ZANZIBAR : Kinyang’anyiro na Utumwa- huyu ni yule Mwarabu aliyekimbilia Arabuni na sasa baada ya kuandika mabaya ya SMZ leo anatamka hayo! Ni mageuzi ya kifikra kutoka mtazamo hasi na kwenda kwenye mtazamo chanya.


Kitu kimoja kinachonishangaza ni uongozi wa vyama. CCM kule Visiwani inaongozwa na wazawa wa kule. Lakini kuna tofauti sana katika CUF Visiwani.


Kihistoria viongozi, kwa maana ya Mwenyekiti wa CUF hajawa Mzanzibari hata mara moja. Huyu amekuwa au Msukuma wa Shinyanga au Mnyamwezi wa Tabora.


Hapo haieleweki siri ya utaratibu huo ni nini? Chama kichwa chake ni Mwenyekiti na mikono yake ni Katibu, sasa iweje Wazanzibari kudai Bara inawameza huku wenyewe wanapenda kuongozwa na wa Bara? (Mzee Mapalala, Mzee Msobi Mageni (marehemu) na sasa yupo Profesa Ibrahim Lipumba).


Isitoshe uhusiano kati ya Wazanzibari na Watanganyika ulianza tangu zamani enzi za Wareno walipopeleka watumwa kwenye mashamba ya walowezi katika Visiwa vya Reunion.


Watumwa wengine walisalia Pemba na Unguja kwenye mashamba. Mwarabu Sheikh Issa Bin Nasser Al-Ismaily katika kitabu chake; ZANZIBAR: Kinyang’anyiro na Utumwa, anaweka wazi makundi ya wabara yaliyoingia Zanzibar tangu enzi za kale.


Anasema, namnukuu; “…Tukiweka kando uhamiaji wa udohoudoho tunaona kwamba Waafrika kutoka Bara walihamia kwa wingi Zanzibar mara tatu.


(i) Mara ya kwanza katika karne ya 16 pale Wapotugizi Wareno) walipowapeleka watumwa Jambang’ombe, Pemba.


(ii) Mara ya pili ilikuwa mwaka 1893 kama inavyoonekana katika ripoti ya John Middleton ya “Land Tenure in Zanzibar ” ambayo inasema kuwa wafalme Sayyid Bin Majid Said na Sayyid Barghash Bin Said walipokuwa na mashamba makubwa na alipokufa Sayyid Ali Bin Said mashamba hayo yaliwekwa chini ya uangalizi wa Idara ya Ziraa.


Idara hii ileleta uhamiaji wa Waafrika wa Bara na kuwaruhusu kufanyakazi katika mashamba ya Serikali na yale yaliyokuwa ya ukoo wa kifalme.


(iii) Mara ya tatu ya uhamiaji kutoka Bara ilikuwa katika mwaka 1930 walipopelekwa Zanzibar wakiwa vibarua katika ujenzi wa gati (ZANZIBAR : Kinyang’anyiro na Utumwa uk. XXXIX).


Hivyo, wabara kule Visiwani walikwenda kikazi, sasa wameloea huko wala hawajui hata asili za makwao huku Bara. Aidha, ipo mifano ya wazee kama vile  Mzee Hassan Nassoro Moyo, Edington Kisasi, Saidi Natepe, Mohamed Mfaume, Abdallah Balozi (alikuwa Mkuu wa Mafunzo), Mzee Ali Hassan Mwinyi, Brigedia Generali Adam Mwakanjuki, Mzee Meja Jenerali Hamisi Hemedi Nyuni,  Mzee Meja Jenerali Juma Maneno Mheza; hawa wote ni wa asili ya Bara, lakini sasa ni Wazanzibari – utawatenganishaje na Bara?


Kwa kuelezea namna makundi mbalimbali ya wabara yalivyoingia Zanzibar tena kwa awamu tatu tofauti ni dhahiri kukiri kuwa kuna uhusiano mkubwa tena wa damu kati ya wakazi wa pande hizi mbili za Muungano.


Mwarabu anawaita wananchi hao Waafrika na kwa usahihi kabisa anajitofautisha wazi kuwa Mwarabu siyo Mwafrika kwa hiyo ni wakuja tu, ni mgeni.


Katika kitabu chake anasema hivi, namnukuu tena; “Maelezo niliyoyatoa hapo juu ingawa ni ya kweli mtupu wa taarikh, huenda yakafahamika vibaya na kuleta sura ya kuwachuja au kuwabagua watu kwa kutokana na taarikh zao katika kufika Zanzibar . Haya matamshi yanaashiria “guilly, conscienceness” ya Mwarabu”.


Lakini anaendelea kulaumu yale Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 kwa maneno kama hivi – “ijapokuwa Mwarabu alipotolewa Zanzibar aliacha nchi hiyo katika hali ya neema na usalama, lakini katika muda wote tangu Mapinduzi yale kila siku kunazidishwa chuki na bughudha hizi na zile dhidi ya Waarabu kwa uzushi huu na ule au kwa vitimbwi hivi na vile”.


Tazama (ZANZIBAR : Kinyang’anyiro na Utumwa” uk . XL ibara ya pili na ya tatu).

Hapo kwa maneno namna hiyo kweli ni uzalendo wa Uzanzibari au kuna kilio cha kupokonywa ulaji? Watu namna hii wanaweza kuutakia Muungano mema kweli? Mbona wana mtimanyongo?

 

Aidha, pale African Association ya Zanzibar ilipowasiliana na chama cha African Dancing Association cha Dodoma kwa barua ya Aprili 22 1936, Wana AA Zanzibar waliona umuhimu wa kuwahimiza Watanganyika kuwa na chama au kufungua tawi la African Association upande wa Bara.


Mwaka 1939 ulifanyika mkutano wa pamoja na viongozi wa matawi ya AA Zanzibar na Bara. Mwenyekiti wa mkutano huo alikuwa Mtanganyika kutoka tawi la Tanganyika African Association, Dar es Salaam . Tangu hapo uhusiano umekuwa ukifanyika mara kwa mara baina ya viongozi wa vyama hivyo hadi mwaka 1957 Mwalimu Nyerere alipokaribishwa katika kikao namna hiyo mjini Zanzibar Association, kwa ajili ya kuunda ASP.


Mwaka 1977 vyama vya TANU na ASP vikasiliba uhusiano ule kwa kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa mtiririko namna hii inawezekanaje kubagua mbara na yule wa Kisiwani hata useme Muungano unakandamiza wa Visiwani? Hao wanaofanya hivyo si wenzetu, bali ni wageni kutoka Arabuni.

 

Bila shaka kila msomi wa historia anajua haya, hivyo basi kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar mnamo Aprili 26, 1964 hakukuwa bahati mbaya, bali kulikuwa ni mlolongo wa uhusiano wa zama hizo kati ya Watanganyika na Wazanzibar tangu karne ya 16.


Haya yote yameelezwa kwa kifupi ili hatimaye ieleweke kwamba hakuna haja wala sababu kwa Wazanzibari kugombea madaraka kwa kupitia Serikali ya mseto au shirikishi.


Kama alivyoeleza Mzee Mwalimu Yusuf Halimoja katika Gazeti la Mtanzania toleo Na. 4354 la Aprili 13, 2008 uk.10 kwa kusema; “KUGAWANA MADARAKA SI SULUHU YA MWAFAKA”. Kuwa hilo siyo suluhisho la mpasuko wa kisiasa Visiwani Zanzibar.


Madaraka ni sehemu mojawapo ya mgogoro, lakini kikubwa ni Wazanzibari kujitafiti kulikoni? Chuki, visasi, uhasama na kutokuaminiana kunatokea wapi?

1313 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!