Enzi za ukoloni, Wafaransa walitawala zaidi nchi zile za Afrika Magharibi. Mtindo wao wa kutawala ulikuwa tofauti sana na ule wa Waingereza tunaolijua sisi huku Afrika Mashariki.

Kwa Wafaransa waliwachukulia Waafrika wasomi kama wenzao ndiyo maana Waafrika wasomi waliweza kuwa hata maraia wa Ufaransa na pia waliweza kustahili kuwa Wabunge wa Bunge la Ufaransa. Mwalimu Julius Nyerere akiwakejeli kwa kuwaita wavaa makoti ya “mende”.

Hii ilitokana na Waafrika hao kuiga lile vazi la koti kubwa nyuma (mgongoni) limepasuliwa ambako koti hilo mbele lilikuwa kama kinusu koti kile cha Kiarabu. Basi waheshimiwa wabunge wale wa kutoka Afrika waliyavaa makoti hayo kwenye dhifa zote za kule Paris n ahata nchini mwao.

Hii tabia ya kuiga mila na desturi ya Kizungu haikumfurahisha Mwalimu, lakini Waafrika wale wa nchi za Afrika Magharibi waliyathamini mavazi na mila za Kifaransa mradi waonekane kama Wazungu Wafaransa wenyewe. Kumbe Mfaransa Mzungu aliwaona Waafrika wale kama malimbukeni vile.

Pili, Waafrika wale walipenda kuiga miondoko (mannerism) na misemo (lafidh) ya Kifaransa. Lakini matendo yao yote yalitofautiana sana na matendo ya Wazungu Wafaransa wenyewe.

Hapo ndipo Wafaransa wakawabatiza Waafrika wale wa kutoka nchi za makoloni yao huko Afrika Magharibi kwa kuwaita “Le grande enfante” wakimaanisha Mwafrika kama “toto kubwa” kimaumbo linaonekana kubwa, lakini kimatendo ni kama watoto kabisa. Kwanini wawaite hivyo?

Kwa kawaida mtoto ana tabia za kulia lia, kuombaomba, kudai atendewe hivi au vile na mama yake na pengine kuendelea kunyonya hata kama mkubwa. Vi-tabia hivi vya kudekadeka Wazungu waliviona kwa Waafrika wasomi wale. Wakitamani uzungu- kimavazi, kimiondoko na kimilo ndipo kwa kuwakebehi tu, Wafaransa waliwalinganisha Waafrika wasomi wale kama watoto tu kifikra ndipo wakawaita Waafrika hawa ni “matoto makubwa” ndiyo hilo jina la hapo juu “MWAFRIKA BADO “LE GRANDE ENFANTE”.

Tusikasirike na kuona eti tunadharauliwa, hapana! Waafrika wengi ndivyo tulivyo au ndivyo matendo yetu yanavyotutambulisha. Tumesoma kama wao, lakini kimatendo tunafanana na watoto tu. Hapa kwetu mipasho inasema “MTU MZIMA HOVYO”.

Kwanza, tunapenda sana kunung’unika na kudai hili au lile kwa kusema mbona hatutendewi hivi au vile kama wanavyotendewa kule Ulaya au Marekani.

Pili, tunaamini bila kudai kitu, hakuna kinachoweza kupatikana kama ni haki au stahili yetu.

Tatu, tukubali jamani Waafrika tu malimbukeni wa ustaarabu na demokrasia ya Magharibi. Ulinganisho wetu wa demokrasia ni ule wa nchi za Magharibi, kamwe hatuigi Mashariki wala hatuonei fahari tamaduni za Mashariki (oriental cultures).

Mzungu alipofika huku Afrika alipata ardhi yetu kwa kutuhadaa na nguo, shanga, na hata vioo kutuonyesha sura zetu. Machifu wetu walilainika na kufurahia zawadi zile hata kudiriki kuuza ardhi yetu kwa wageni wale. Historia inasema hivyo. Sasa tamaa au tabia na mazoea yale ya ulimbukeni yanafika hata leo miaka 55 ya Uhuru wetu, bado tunatamani tuonekane katika vioo siku hizi tunaita “runinga”. Bila kuonekana humo, ati tunadiriki kudai wananchi wananyimwa haki zao za msingi za kuona wawakilishi wao wamesema nini bungeni. Hilo linakuwa sasa dai la wananchi. KUONEKANA BUNGE “LIVE” hapo demokrasia itakuwa imekamilika.

Mimi haliningii akilini, kusikia baadhi ya tuliowachagua mwaka jana kwenda kupeleka SHIDA zetu bungeni wanasusa kutoa hizo shida eti kwa sababu wananchi sasa wamenyimwa haki yao ya kuona shughuli za Bunge “LIVE” kama miaka iliyopita! Ninajiuliza kutoa SERA MBADALA, KUTAMKA BUNGENI SHIDA ZA MAJIMBONI, hakutoshi mpaka RUNINGA ZIONESHE LIVE? Waingereza wanauliza: “Is that really an Issue?”

Bunge limekuwapo tangu ukoloni. Hapakuwa na runinga. Hizi TV zimeruhusiwa miaka ya hivi karibuni tu. Iweje leo tuambiwe ni haki muhimu ya mwananchi?

Kwa mtu wa kijijini ambako hakuna umeme, hana runinga hivyo, issue ya kuona yanayotendeka bungeni kwake haipo. Wenye runinga ni sisi wa mijini tu! Hili ni kundi la walionacho na ni TABAKA dogo la wenye uwezo. Tabaka la walionacho wakikosa kuonekana ndipo haki za wananchi zinakosekana?

Hebu hapa niulize mwaka 1958/1959 mpaka 1960 tulipofanya uchaguzi wa MSETO, kulikuwapo RUNINGA? Bunge letu la UHURU 1961 tuliliona? Wakati Mwalimu Nyerere anakabidhiwa HATI ZA UHURU – “INSTRUMENTS OF INDEPENDENCE” kulikuwapo runinga Watanganyika wakaona? HAPANA! Kitu kilichokuwapo ni REDIO- nayo ilianza miaka ya hamsini na kitu. Na sote mikoani tulisikia, nini kilisemwa pale Uwanja wa Uhuru na matokeo ya kusikia kwetu tuliserebuka kufurahia huo Uhuru wetu. Mbona hatukumuona mume wa Malkia, Prince Phillip akimkabidhi Baba wa Taifa hiyo hati ya Uhuru? Je, uhuru tulipata au hatukupata?

Leo hii, upinzani na wengine wenye mawazo ya kikabaila wanataka tuamini kuwa demokrasia inaminywa kwa kutokuonekana “LIVE” mijadala ya Bunge. Hebu tukomae kifikra sisi watu weusi. Ni kweli bila runinga mtu huwezi kutoa mawazo “mbadala” ya yale mawazo ya Serikali? Are we really being serious on this?

Usiku wa Desemba 08, 1961 katika Uwanja wa Uhuru Baba wa Taifa alikuwa na haya ya kusema: “I have listened to your Royal Highness’s expressions of goodwill and to those which you have brought to us from her Majesty, and I have received those INSTRUMENTS. Which are the embodiment of my country’s freedom with the deepest emotion. This is the day for which we have looked so long, the day when every Tanganyikan can say, ‘I am a citizen of a sovereign independent state’”! (Nyerere: Uhuru na Umoja sura 33 uk. 42 – Receiving Instruments of Independence)

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi maneno ya Baba wa Taifa yalisema: “Nimesikiliza matamshi yako mtukufu, yenye kututakia mema, na nimepokea hati kutoka kwa mtukufu Malkia, yenye kutamka Uhuru wa nchi hii kwa moyo mkunjufu sana. Hii ndiyo siku tuliyoingojea sana, ni siku kila Mtanganyika anaweza kusema, ‘Mimi ni raia wa Taifa huru’”. Shughuli hii muhimu ilisikika katika redio na kamwe haikuonekana “LIVE” tukaona Baba wa Taifa alipokabidhiwa hiyo hati ya Uhuru wa nchi yetu hii.

Ninakubaliana na mgombea urais wa Republican kule Marekani, Donald Trump pale anapowabehua viongozi wa Afrika kwa maneno kama haya: “I think there is no shortcut to maturity and in my view Africa should be recolonized”;  yaani anafikiri Waafrika hatujapevuka na bado tunahitaji kutawaliwa kikoloni.

Mei 1974 Baba wa Taifa aliwaambia wana kongamano pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam maneno namna hiyo hiyo aliposema: “Africans should be mentally liberated”.  Inawezekanaje kiongozi mkuu unaacha kujibu mapigo ya hotuba ya Waziri Mkuu kwa kuonesha mawazo mbadala ya kuendeleza Taifa unakazania, hatutoi maoni wala mawazo yetu kwa vile Serikali imebinya uhuru wa kuona “live”mijadala ya Bunge hili.

Hapo ndipo Wafaransa wanatuita Waafrika “matoto makubwa”, Donald Trump anasema “no shortcut to maturity”. Matusi kama hayo si tunajitakia sisi wenyewe?

Nilipata kusoma mwenye gazeti moja, nafikiri Jambo Leo toleo No. 2404 la Alhamisi, Aprili 07, 2016 uk. 4 nikakuta maneno haya: “Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe amepongeza kitendo cha Rais John Magufuli kuelekeza fedha za sherehe za Muungano katika huduma za jamii na kwamba kitendo hicho kinamfanya aonekane kifikra ni mwenzetu ila kimwili na kiitikadi ni CCM”.

Ndugu Mbowe alinukuliwa akisema kuwa katika miaka yote ya yeye kuwa kiongozi wa upinzani bungeni hotuba zake zimekuwa zikizungumzia upunguzaji wa matumizi yasiyo ya lazima, sherehe za Muungano zikiwa mojawapo.

Namnukuu tena, aliendelea kusema: “Unajua ukimwangalia Magufuli anaonekana kifikra ni mwenzetu ila kiitikadi na kimwili ni CCM hivyo kwa hilo nampongeza kwani ndio mipango yetu siku zote” (Soma kwa ukamilifu Jambo Leo Toleo 2404 la Alhamisi, Aprili 07, 2016, uk. 4 wote).

Baada ya kuona namna Mwenyekiti wa CHADEMA alivyokuwa na mtazamo chanya kwa Rais wa Awamu hii ya Tano nikajua Bunge la safari hii litakuwa na mtazamo endelevu kwa Taifa.

 

>>ITAENDELEA

1371 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!