Mwaka mmoja wa Magufuli madarakani Tusimsifu wala tusimhukumu

Naujadili utawala wa Rais Magufuli kutimiza mwaka mmoja. Kwa kuchagua kwa makusudi maneno mawili – tusimsifu wala tusimhukumu – wengine wanaweza kushangaa!

Lakini ngoja nikumbushie kisa cha mtaalamu kutoka Japan aliyepelekwa Kigoma. Huyo mtaalamu kila alipoona eneo jipya alilopelekwa Kasulu, Kibondo, Manyofu na maeneo mengineyo, alimwaga chozi na kutikisa kichwa, akisema Watanzania mna utajiri wa ajabu.

Kwenye sherehe ya kumuaga alisema ingetokea wakazi wa Tokyo wakahamishiwa Kigoma na wakazi wa Kigoma wakahamishiwa Tokyo, ndani ya miaka mitano Tanzania ingeikopesha Japan.

Huyo hakuwa mgeni wa kwanza kuustaajabia utajiri wetu asilia ambao wenyewe hatuna jicho la kuuona wala fahamu za kuutambua. Tunalia juu ya hali ngumu ya maisha, makali ya umaskini kuongezeka wala hatujui tutakavyoukomesha.

Myahudi mmoja aliyeishi nchini mwetu kama mtaalamu wa kilimo na ufugaji wa kuku, kila tulipogusia uchumi wa Tanzania, alijihami akisema “mind you, I am the only Jew in this country.” Alitaka nisimwingize kwenye ukosoaji kwa sababu ndiye Myahudi pekee aliyebahatika kuwako nchini Tanzania. Wayahudi wengine wote walifukuzwa mwaka 1967 Tanzania ilipovunja uhusiano wa kibalozi na Israel.

Huyo Myahudi alikuwa akiniambia waziwazi kwamba “ninyi Watanzania mnapolalamikia umaskini na matatizo ya uchumi wenu mnakufuru, kiuhalisia mnadeka, hamna matatizo ya kuwafanya mlie.” 

Aliendelea kusema; “Sisi Wayahudi tuna upungufu wa ardhi, tunaligeuza Jangwa, tunalirutubisha ili lilimike, tunazalisha nchi kavu kutoka baharini (to claim land from the sea), tuna vita kwa saa zote 24 na hatutarajii vita hiyo iishe leo wala kesho, tumezingirwa na maadui pande zote, tunailinda mipaka yetu wakati wote kwa gharama kubwa, lakini bado tunaijenga nchi.

“Wayahudi wanaotoka sehemu mbalimbali za dunia, wanapoingia nchini wakitokea uhamishoni hawajui hata lugha ya Kiyahudi, inabidi serikali igharamie kuwafundisha, wengine huja wakiwa hawajui kusoma wala kuandika inabidi wasomeshwe hata kama ni watu wazima, wanapatiwa nyumba, chakula na kutegemezwa hadi wamudu maisha.”

Kila alivyonisimulia matatizo ya Waisraeli wa sasa ndivyo nilivyopata simanzi moyoni kwamba kumbe sisi Watanzania tunapomlilia Mungu tunafanana na mtoto anayedeka, hatujafikia hatua ya kulia. Kwa sababu tumezingirwa na neema nyingi na fursa tele ambazo walimwengu wengine hawanazo na wakituangalia wanazitamani wakituonea wivu jinsi Mwenyezi Mungu alivyotupendelea. 

Yawezekana huo wingi wa rasilimali ndiyo uliochangia kutupofusha tusiuone utajiri wetu ambao wageni wanauona, badala yake tumejielekeza kwenye utajiri wa aina moja tu wa fedha taslimu.

Kwa kukosa fedha taslimu, mtu anajiona maskini lakini hatari inayoinyemelea Tanzania ni kwamba hao wageni wanaouona utajiri wetu hatimaye watakuja kama wawekezaji, ila kiuhalisia watakuja ili kuvuna hicho tusichokiona. Watakuja kujinufaisha na utajiri wetu wakiendelea kutupumbaza kwa fedha taslimu ambazo haziwezi kuuondoa umaskini unaolitesa Taifa.

Mtu anaweza kuubaini umaskini wa kiroho kwa hao wachache wanaofanikiwa kupata mamilioni ya dola kwa namna wanazozijua wao, wengi wameishia kuzificha kwenye mabenki ya nje.

Hiyo ni ishara ya wazi kwamba mgeni hata akimwaga mabilioni ya dola barabarani, ana uhakika hao watakaoziokota mwisho watazirudisha kwenye benki za Ulaya na Marekani, fedha zitarudi kwao na Mtanzania atabaki na umaskini wake.

Ninapoujadili utawala wa mwaka mmoja wa Rais Magufuli, nalazimika kujiweka mbali na washabiki, nauchukia ushabiki wa siasa na ushabiki wa dini, kwa sababu nauona hauna manufaa kuanzia kwa washabiki wenyewe hadi kwa Tanzania kama Taifa.

Mshabiki yeyote daima huwa siyo mkweli wala haukubali uhalisia, kwa kuukataa ukweli shabiki anaukataa uhuru, kwa kuwa kila anayeukataa ukweli analazimika kuukumbatia uwongo. Kila mwenye kuukubali uwongo umwingie hadi kwenye utamaduni wake hujitia yeye mwenyewe kwenye utumwa asiouelewa. Hakuna uhuru ndani ya uwongo kwa sababu ni ukweli peke yake ndiyo umwekao mwanadamu huru.

Kwa hiyo, naziepuka pande zote mbili yaani mashabiki wanaomsifu na kumtukuza Rais wakijifanya kumtetea, na hao washabiki wanaomlaumu na kumlaani wakiukosoa utawala wake na kujaribu kuonesha mambo kadhaa wanayoona hayaendeshwi vizuri.

Yawezekana wanaomtetea wanahami ulaji wao, hata hivyo; ushabiki wao haumsaidii Rais Magufuli wala hauinufaishi Tanzania kama nchi kwa kuwa ushabiki wao hauielekezi nchi kwenye suluhisho. Vivyo hivyo. mashabiki wa upande wa pili yaani wakosoaji wanaolaumu na kulaani kwamba kuna mambo hayaendeshwi vizuri, wanafanya hayo katika misingi mibovu ya kutetea maslahi binafsi. Wakosoaji wengi walitamani ungeingia madarakani utawala ambao ungewanufaisha wao kama watu binafsi na siyo kuwanufaisha Watanzania katika ujumla wao.

Mashabiki wa kawaida (laymen) wanaolalamikia mzunguko wa fedha wanadai chini ya uongozi wa Magufuli fedha imeadimika. Hawa wanajenga hoja zao wakijikita kwenye hisia tu ambazo kimsingi ziko mbali na uhalisia wa mambo kama ulivyo.

Lipo tabaka la wasomi – maprofesa na madaktari bingwa wa fani mbalimbali kama siasa, uchumi na sheria ambao wamezungumzia jinsi utawala wa Magufuli ulivyoshindwa ama ulivyoharibu. Hata hivyo, nao hawatoi suluhisho wala hawaoneshi njia mbadala za kumfanya Mtanzania aelewe nini kinapaswa kufanyika ili Tanzania yetu itoke kwenye hali mbaya na kusonga mbele kuelekea kwenye ubora. Ni wasomi wasioonesha njia ya kuifikisha Tanzania kwenye neema.

Wataalamu wanaoishia kulaumu au kulaani tu bila kuonesha njia ya kuifikisha Tanzania kwenye neema wanawachanganya wananchi kwa sababu wanatoa kauli zisizotoa suluhisho.

Mtaalamu asiyetoa suluhisho anajiweka kwenye daraja moja na washabiki maana utaalamu wa kweli unaelekeza pale mambo yalipokosewa na pia unaonesha njia au namna ya kusawazisha na kurekebisha mambo yaliyokosewa.

Kati ya mwaka 1960 na 1970, Tanzania ilipoendesha siasa za uhuru na ujenzi wa Taifa jipya, ikitoka kwenye mfumo wa ukoloni hadi kwenye mfumo mpya, wasomi hawakutoa mchango wao wa kitaalamu katika kuwezesha Tanzania kubadilika. Wasomi na wataalamu walisusa kwa sababu hawakuuafiki kidhati utawala wa Nyerere pia hawakuipenda siasa yake ya Ujamaa wala hawakuzikubali sera zake za uchumi.

Msomi mmoja aliyeitwa Profesa Alli Mzrui alijipambanua kuwa mkosoaji wa sera za Nyerere hadi siku moja Nyerere akalalamika akisema; “Nimeitwa kanibali wa kisiasa na kufananishwa na mlaji wa nyama za wanadamu wenzake, kwa sababu moja tu ya utaifishaji.”

Profesa Mazrui aliandika makala iliyopewa uzito kwenye magazeti kadhaa ya Uingereza na Marekani. Makala hiyo ilibeba kichwa kilichosema ‘Political cannibalism.’ Marekani na Uingereza ziliipinga vikali sheria ya kuweka watu kizuizini pasipo kuwafikisha mahakamani.

Sheria hiyo ilianzia Ghana kwenye utawala wa Rais Kwame Nkrumah, lakini Nkrumah mwenyewe alikuwa akiitetea kwamba hali halisi ya tatizo lililoikabili Ghana baada ya muda mfupi tangu ipate uhuru ndiyo iliyowalazimisha wao kama watawala kubuni utaratibu huo wa kumweka mtu ndani pasipo kumfikisha mahakamani.

Kwenye mji wa Acraa na miji mingine mikubwa nchini Ghana, hali ya ujambazi ilikubuhu na kutishia maisha ya watu kiasi cha kuwafanya wananchi waanze kuhoji kama serikali ya uhuru, inao uwezo wa kuwalinda kama walivyolindwa na serikali ya mkoloni!

Kutokana na uwezo mdogo wa jeshi la polisi kukusanya ushahidi wa kumthibitisha jambazi sugu mahakamani, washitakiwa wa ujambazi wengi waliachiwa huru na waliendelea kuwaumiza raia wema, ndipo utawala wa Nkrumah ukaona suluhisho pekee lililokuwa limesalia ni kuwakamata hao waliojulikana kuwa majambazi sugu na kuwaweka kizuizini pasipo kuwafikisha mahakamani. Marais wengine wa nchi za Afrika wakaiga mfano wa Ghana, wakawaweka kizuizini wapinzani wao wa kisiasa.

Wengi waliokosoa sera ya utaifishaji walisema dola ilikuwa inadhulumu mali za watu kwa kuwanyang’anya watu mali zao walizochuma kihalali, lakini bado wakosoaji hawakutoa suluhisho kwamba huyo mwenye mali na mtaji mkubwa anapoutumia mtaji wake na utajiri wake kuwanyonya maskini aliowazidi nguvu kiuchumi, ilitakiwa lifanyike nini ili kudumisha haki katika maisha ya watu.

Rais Magufuli amerithi Tanzania iliyoharibika, kwa bahati mbaya mharibifu mkuu ni Mtanzania mwenyewe aliyejiona yuko huru ndani ya mifumo wa kigeni wa utandawazi na soko huria. Watanzania walitaka mabadiliko kwa sababu walikinaishwa na jinsi mambo mengi yalivyoendeshwa hovyo, waliumia kuona rasilimali za nchi zikiporwa na wageni ilhali wenye nchi wakibakia masikini, ndipo walio wengi wakatamani uje utawala unaoweza kudhibiti hayo.

Uhalisi wake ni kwamba Watanzania walihitaji kiongozi mkali atakayesimamia utaratibu wa kuondoa mabaya yaliyowakinaisha, siku zote ubaya haundoshwi kwa kufanya vizuri bali mara nyingi ubaya unaondoshwa kwa kufanya mambo vibaya zaidi. Kihistoria, hakuna aliyewahi kuushughulikia ubaya kitakatifu. Yesu alikuwa mtu mwema na asiyekuwa na dhambi lakini kwa kuwa aliuchukia uovu alipolisafisha hekalu hakutumia upole wala wema wake, bali aliwatoa nje kinguvu waliofanya biashara hekaluni. 

Mtu akipenda kutumia Kiswahili cha mitaani anaweza kusema Yesu aliwatoa nje ‘kishenzi’ hakutumia upole wala utakatifu, alitengeneza kikoto cha kamba akazipiga meza za waliobadilisha fedha, akatimua akiba zao, akapindua meza na kumwaga fedha chini, akawasukumizia nje wauza njia na kuyaswaga nje kinguvu makundi ya kondoo, akawashutumu akisema mmeigeuza nyumba ya Baba kuwa pango la wanyang’anyi.

Je, ni unyang’anyi gani uliofanyika hekaluni? Ni wazi alizungumzia biashara za hao waliobadilisha fedha, aliwaona waliouza njiwa kwa ajili ya dhabihu na waliobadilisha fedha za Wayahudi waliotoka mataifa mbalimbali ili kuja kuhiji Yerusalemu, walikuwa wakinyang’anya kupitia mfumo uliomlazimisha mwenye kuhiji kununua njiwa ama kondoo, mfumo uliomlazimisha abadilishe fedha ya kigeni kuipata sarafu ya Kirumi iliyohitajika, na mengine mengi ambayo akili ya kawaida haikuyaona kama udhalimu.

Ndipo wengine wakamuuliza Yesu wakisema ni ishara gani hii utuoneshayo unavyoyafanya haya? Kiuhalisia, walimaanisha ile ilikuwa ishara ya ubabe na ushenzi wa kutojali wala kutothamini mali zao.

Kwa hiyo, kutokana na hali halisi ambayo Rais Magufuli aliirithi nchi, ni wazi asingeanza na gia ya upole wala asingefanya mambo kwa mazoea. Kama angeendeleza mambo yaliyozoeleka asingeeleweka, ilipasa Magufuli aietendee haki Tanzania kwa kufanya mambo yanayofanana na kitendo cha Yesu alichofanya katika kulisafisha Hekalu. 

Ilibidi Rais Magufuli aanze kuisafisha nchi kwa ukali na kupitia hizo pilikapilika za kuondoa mabaya yaliyozoeleka na ambayo yaliwanufaisha baadhi ya Watanzania wenzetu, lazima makosa madogo madogo yawepo, lazima maumivu yawepo, pia lazima lawama ziwepo kwa sababu hakuna baya linaloondoshwa kitakatifu.