Wiki hii nchi imeingizwa katika mjadala mrefu usio na tija. Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe nadhani amehemka tu, akasema ikibidi atakifuta Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS). Kauli ya Dk. Mwakyembe imetoka muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kuwataka wanasheria wanachama wa TLS kujiepusha na siasa.

Rais Magufuli Februari 2, alionya hatari ya TLS kuingiliwa na kutumika kufanikisha malengo ya kisiasa. Alisema anazo taarifa kuwa baadhi ya wanasiasa wanataka kugombea nyadhifa ndani ya TLS kwa nia ya kufanikisha malengo yao. Akasema TLS inapaswa kubaki kuwa taasisi huru, isiyo na fungamano wala kuwa chombo cha harakati za kisiasa.

Sitanii, nakubaliana na Rais Magufuli katika hili. TLS ni sawa na madaktari. Hatupaswi kufika mahala mgonjwa ukaingia katika chumba cha upasuaji, ukawaza: “Hivi mimi nilikuwa msimamizi wa kituo cha kura pale Buguruni A, iliposhinda CUF, CCM au CHADEMA na daktari aliyepangiwa kazi ya kunifanyia operesheni nilimtangaza kuwa ameshindwa katika uchaguzi ule, sasa hatanilipizia kisasi kwa kuacha mkasi tumboni kwangu kweli?”

Mfano huu ni sawa na wanasheria. Naomba kuwaza kwa sauti. Hivi kweli leo Wakili Msomi kama Tundu Lissu, anaweza kumtetea kwa ufanisi aliyekuwa mgombea ubunge Temeke kwa tiketi ya CCM akashindwa, Zuberi Mtemvu kwa nia ya kumwezesha apindue matokeo ya upinzani kuiweka CCM madarakani?

Si Lissu tu, najiuliza hivi kweli Wakili Msomi, Dk. Pindi Chana, aliyekuwa Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Mjumbe wa Kamati Kuu na sasa Balozi anaweza kwenda Kigoma Kusini kumtetea aliyekuwa mgombea ubunge wa NCCR Mageuzi, David Kafulila aliyeshindwa na mbunge wa CCM? Tusaidiane kuwaza tu na tupeane jibu lisilo na upendeleo.

Hata hivyo, katika siku hiyo Rais Magufuli alikwenda mbali. Sikubaliani na kauli aliyoitoa kuwa mawakili wanaotetea wahalifu basi nao wakamatwe na kufunguliwa mashtaka. Kwa ruhusa yake tu, naomba kumpa mfano wa askari aliyekamatwa Arusha, aliyekuwa anawabambikia watu kesi za bangi. Ikitokea fursa ya kuzuia mawakili kutetea watu, askari wa aina hii na watu wengine wapo wengi. Watu wataumizwa bila hatia. Naomba wazo hili kwa mawakili liwekwe kando.

Sitanii, nimepata shida mno na kauli ya Dk. Mwakyembe kuwa ataifuta TLS. Kauli kama hiyo ingetolewa na Waziri ambaye taaluma yake ni Injinia, ningemsamehe, ila si Mwakyembe. Huyu amekuwa mwalimu wa sheria kwa muda mrefu. Anafahamu kuwa TLS haikusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani, hivyo si kampuni wala NGO unayoweza kuamka asubuhi ukatangaza kuifuta.

TLS imeanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 307 ya Mwaka 1955 iliyorasmishwa na Bunge baada ya Uhuru kupitia Sheria ya Judicature and Application of Laws Act (JALA) ya Mwaka 1961. Anatambua kuwa yeye ni Wakili kwa mujibu wa Sheria ya Mawakili Na 341 ya Mwaka 1955 na Kanuni zake za Mwaka 2015, hivyo alipaswa kufahamu kuwa TLS si chombo cha kuamka asubuhi ukakifuta.

Sitanii, kinachonipa shida zaidi ni sababu ya nia ya Mwakyembe ya kutaka kuifuta TLS. Eti anataka kuifuta TLS kwa sababu Wakili Msomi, Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu ametangaza nia ya kugombea Urais wa TLS. Kama ni TLS kuwa kwenye siasa, sidhani kama Lissu ndiye wa kwanza kuwa Mbunge na akashika wadhifa ndani ya TLS.

Dk. Pindi Chana niliyemtaja hapo juu, hadi hivi ninavyoandika makala hii ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Masuala ya Sheria ya TLS. Sijasikia Pindi Chana akitangaza kujiuzulu Ujumbe wa Kamati Kuu CCM. Haiwezekani TLS ikaonekana ni ya kisiasa pale tu Lissu alipotangaza nia ya kugombea urais wa taasisi hiyo, ila wakati Chana ni mjumbe wa Kamati nyeti ya TLS hazikuwapo siasa.

Sitanii, ushauri wangu ninaoutoa kwa dhati kabisa. Tanzania ni nchi ya mfumo wa vyama vingi. Hadi hapo tutakapofuta mfumo huu na kurejea mfumo wa chama kimoja, kwa sasa tujiweke sawa kuhakikisha tunaishi kama Watanzania anavyotuasa Rais Magufuli bila kujali itikadi za vyama, vinginevyo tukiona huyu wa Upinzani au CCM ni safi na huyu wa CCM au Upinzani hafai, tutapanda mbegu ya chuki ambayo tutajuta milele sisi na vizazi vyetu. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri