Oktoba 14, mwaka huu imeangukia siku ya Bwana, yaani Dominika – Jumapili. Imekuwa sasa ni kawaida kwa kila mwaka siku hii Tanzania tuna mapumziko ya kitaifa kumuenzi Baba wa Taifa.

Karibu kila gazeti hutoa toleo maalumu la kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

 

Mwaka huu unakuwa ni wa 19 kwa Watanzania bila Baba wa Taifa. Nimekuwa nikiandika makala siku kama hii katika Gazeti la JAMHURI tangu mwaka 2014.

Imetokea mwaka huu Uhuru Publications walitoa changamoto iandikwe makala maalumu kuonyesha matendo ya kipekee kuhusu Mwalimu Nyerere.

Basi, nami katika kupoka au kujibu changamoto ile nimeandika makala ndefu huko na kuwasilisha kabla sijaondoka Dar es Salaam kuja India kwa matibabu.

Katika hali hiyo sikuweza tena kuandika makala katika gazeti hili.

 

Pili, kwa masikitiko hapa nami niwajulishe wasomaji wa makala zangu kwa siku hiyo Oktoba 14, ningali kitandani katika Hospitali ya Apollo huku India katika mji wa New Delhi. Hivyo sitaweza kushuhudia maombolezo ya mwaka huu kiualisia ‘physically’ kwa Mwalimu wangu na ambaye ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika hali ya unyonge kama hiyo, basi naomba Gazeti la JAMHURI walau linionyeshe kushiriki kwangu katika maombolezo hayo kwa kuchapisha picha hizi zinazoonyesha Mwitongo. Jumba la kaburi na kaburi lenyewe – picha ambazo zilipigwa Januari 7, 2018.

 

Jirani na jumba hilo (MAUSOLEUM) ya Mwalimu, kuna Jumba la Makumbusho ya Mwalimu Nyerere.

Humo kuna mavazi ya Baba wa Taifa, zawadi kemkemu alizopokea kutoka nchi mbalimbali wakati wa uhai wake, picha za Baraza la Mawaziri ambalo ndilo Baraza la Kwanza la Mawaziri, na mambo mengine mengi ya kihistoria.

Basi, nashauri wasomaji wa Gazeti la JAMHURI wenye kujiweza wajaribu kutembelea Mwitongo, Butiama kuyaona hayo. Ni elimu ya kutosha katika historia. Hiyo nayo ni namna mojawapo ya kumuenzi Mwalimu na Baba wa Taifa letu.

 

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA LIHIMIDIWE (AYUBU 1:21)

919 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!