Tunaojua historia ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, hatusiti kutamka wazi kwamba Mwasisi huyo wa Taifa letu huenda akaking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) siku si nyingi zijazo.

Watanzania sasa tunaadhimisha miaka 13 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere. Lakini kwa ukweli usiopingika, Serikali yetu inayoundwa na CCM haijaonesha kumuenzi kwa vitendo. Viongozi wengi wanamuenzi kwa maneno tu!


Serikali inachokifanya kwa sasa ni kumuenzi kinadharia; kama vile kutukumbusha hotuba zake kupitia redio TBC Taifa, na baadhi ya viongozi kutaja kwa nadra uadilifu wake.


Uadilifu ni tabia au hali ya kutenda haki na kutopendelea. Mwalimu Nyerere ndiye mtu pekee anayetajwa kumiliki tabia hiyo kwa kiwango kisichotiliwa shaka wakati wa uongozi wake katika chama na Serikali, kama si katika maisha yake kwa jumla.


Mwalimu Nyerere ndiye Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika, Mwenyekiti wa kwanza wa CCM na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Enzi za uongozi wake, Mwalimu huyo alijenga na kusimamia kwa vitendo misingi iliyowezesha wananchi kunufaika na huduma bora za kijamii kwa haki na usawa.


Mfano, wananchi walipata kwa usawa huduma za elimu na afya. Enzi hizo hayakuwapo matatizo ya ubaguzi, mizengwe na ubabaishaji katika utoaji huduma kwenye ofisi za umma kama ilivyo siku hizi.

Leo Mwalimu Nyerere akifufuka anaweza asiamini macho na masikio yake, kuona na kusikia yanayotendeka katika ofisi za umma nchini.


Baadhi ya watumishi wa Serikali wamejaa kiburi, wamekaidi misingi ya kuhudumia wananchi kwa kiwango kinachostahili.


Imefika mahali ambapo viongozi wetu wanaelekea kuzika kabisa misingi ya haki na usawa iliyojengwa na Mwalimu Nyerere. Watoto wa wanyonge ni kama hawathaminiwi katika nchi hii, wananyima haki ya kupata elimu ya kutosha!


Serikali yetu imeamua kuigeuzia kisogo misingi ya Mwalimu Nyerere. Masharti ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga vyuo vikuu ni kikwazo kwa watoto wanaotoka familia maskini.


Watoto wanaotoka familia tajiri ndiyo wenye fursa kubwa ya kunufaika na mikopo hiyo kwa vile wazazi wao hawashindwi kumudu gharama za fomu, ada na usafiri wa kufika vyuoni kwa wakati.

Jitihada kubwa za kutafuta Uhuru, kujenga nchi, kumiliki uchumi na kuinua wanyonge, zilizofanywa na Mwalimu Nyerere zinaonekana kuangukia katika mikono ya viongozi wanaoelekea kusahau kuwa nchi hii ni ya Watanzania wote.


Matatizo ya ukosefu wa huduma bora za elimu, afya, maji na katika ofisi za polisi na mahakama kwa Watanzania bila ubaguzi yanaendelea kulitafuna Taifa letu, huku viongozi wa Serikali ya CCM iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere wakiyaona na kuyasikia bila kuchukua hatua zinazostahili.

Nyerere alionesha njia na mfano wa uongozi bora uliojaa uadilifu, uaminifu, usawa na haki kwa wote akiamini itazingatiwa na viongozi watakaomfuata hata baada ya kutangulia mbele ya haki. Lakini mambo yanakuwa ndivyo sivyo.


Ndio maana ninashawishika kuamini kwamba inaweza isiwe rahisi kwa Serikali ya CCM kupata ujanja wa kukwepa hukumu mbaya ya kulaaniwa na Mwalimu Nyerere ikiwa haitagutuka na kujisahihisha kabla haijachelewa sana.


Kosa la kutelekeza misingi bora iliyowekwa na Mwalimu Nyerere linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kushawishi Watanzania kuona hawana sababu ya kuendelea kukipatia CCM madaraka ya nchi.


Hukumu ya kulaaniwa na Mwalimu Nyerere inaweza kuking’oa madarakani chama hicho na hatamu kushikwa na chama kingine cha siasa kitakachozingatia na kutekeleza kwa ukamilifu misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa.


Hakuna lisilowezekana chini ya jua. Chelewa chelewa utakuta mwana si wako. Majuto ni mjukuu.

Message sent.


999 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!