Mwekezaji katika migodi ya madini ya ujenzi, Majaliwa Maziku, anadaiwa kumlaghai Kamishna wa Madini nchini Tanzania, Paul Masanja, ili kufanikisha azma yake ya kupora ardhi ya wananchi kinyume cha sheria ya madini.

Maziku, ambaye ni mkazi wa Kata ya Kalangalala mjini hapa, anadaiwa kukiuka Sheria ya Madini Na. 14 ya mwaka 2010 kifungu cha 95 na 97 kinachomtaka mwekezaji mwenye leseni kufanya shughuli zake baada ya kukidhi matakwa ya sheria hiyo.

Imeelezwa kuwa Maziku anataka kupora ardhi ya wananchi wa Kijiji cha Nyantorotoro ‘A’, Kata ya Kalangalala wilayani Geita na kwamba mfanyabiashara huyo alimshawishi Masanja aliyeamuru wananchi hao kuondolewa kwa nguvu kwenye maeneo yao bila fidia wakati Mahakama ilikwishawapa haki.

Taarifa zinasema kwamba Maziku na Masanja walikutana mjini Geita Juni 26, mwaka huu kisha waliongozana hadi kwenye eneo lenye mgogoro kijijini Nyantorotoro ‘A’ ambako pia walipita kwenye eneo lenye mgogoro.

“Huu mgogoro ni wa siku nyingi, nimejaribu kupambana kwa kuwatumia baadhi ya viongozi wa Serikali lakini hakuna jipya zaidi ya kutumia muda wangu mwingi na hata kutumia pesa zangu, mtu ambaye umebaki na unayeweza kunisaidia ni wewe mheshimiwa,” kilisema chanzo chetu kikinukuu baadhi ya maneno ya kujitetea ya Maziku kwa Kamishina Masanja.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea eneo lenye mgogoro, Masanja anaripotiwa kukutana na baadhi ya wananchi na baada ya kusikiliza madai yao, alimshauri mwekezaji Maziku kuwalipa fidia ili afanye kazi zake kwa uhuru.

“Ndugu yangu nikushauri tu kwamba ili ufanye kazi zako kwa uhuru zaidi, ongea na wananchi wa maeneo haya uwalipe fidia, ndiyo njia rahisi itakayoweza kutatua mgogoro huu,” alisikika Masanja akimwambia Maziku, tamko ambalo lilipokewa kwa shangwe na baadhi ya wananchi waliofika kumsikiliza.

Katika hali ya kushangaza, Julai 2, mwaka huu, Kamishna Masanja ama kwa kushawishiwa na mwekezaji Maziku au kwa kutumia rungu alilonalo, aliamua kupindisha amri ya Mahakama na kuandika barua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie, ikimtaka kuhakikisha wananchi hao wanaondolewa kwa nguvu kwenye maeneo yao bila kulipwa fidia.

Barua hiyo Kumb. Na. DA.55/171/01 yenye kichwa cha habari ‘Mgogoro katika eneo la leseni PML 000229LZ-000238LZ zinazomilikiwa na Ndugu Majaliwa Paul Maziku’ pamoja na mambo mengine katika kipengele cha tatu inasema.

“Aidha, suala hili lilifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Geita ambapo Oktoba 25, 2012 Hakimu D. K. Kamugisha alitoa hukumu kuwa wananchi hao (wavamizi) wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo ili kupisha shughuli za uchimbaji zitakazoendeshwa na mmiliki wa eneo hilo.” Imeongeza; “Kupitia hukumu hiyo ya Mahakama, Jeshi la Polisi liliagizwa kutekeleza amri hiyo.”

 

DC atekeleza maagizo ya Kamishna

 

Oktoba 9, mwaka huu Ofisa Madini Mkoa wa Geita, Pius Lobe, alifika eneo lenye mgogoro akiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, SSP Ibrahim, kwa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mangochie.

Pamoja na mambo mengine, OCD Ibrahim ambaye alikuwa ameongozana na lundo la askari polisi wa kada ya chini, aliwatisha wananchi hao akiwataka kutokanyaga tena kwenye maeneo hayo na atakayebainika atakiona cha mtema kuni.

Kutokana na hali hiyo, kuanzia Oktoba 9 hadi sasa mwekezaji huyo anafanya shughuli zake chini ya ulinzi mkali wa polisi, huku baadhi ya wananchi wanaokatiza jirani na eneo hilo wakiishia mikononi mwa polisi na kuwekwa ndani.

 

Ukweli wa uamuzi wa korti

Wakati barua ya Kamishna Masanja ikisisitiza kuwa Mahakama ilimpa haki mwekezaji Maziku na wananchi kutakiwa kuondoka eneo hilo, gazeti hili limebaini kuwa maelezo ya Kamishna Masanja katika barua yake yana utata.

Mwandishi wa gazeti hili amesoma kwa makini uamuzi mdogo (Ruling Exparte) uliotolewa na Mahakama hiyo pamoja na hukumu yenyewe na kugundua kuwa Mahakama hiyo iliwapa haki wananchi hao na si vinginevyo.

Taarifa zinasema kwamba Oktoba 25, 2012 Maziku alifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na siku hiyo hiyo Mahakama hiyo ilitoa uamuzi wa upande mmoja (ruling exparte) ambao wananchi waliamuriwa kutofanya shughuli zozote kwenye eneo lenye mgogoro.

Januari 28, mwaka jana, Mahakama hiyo ilitoa uamuzi na kufafanua kwamba wadaiwa (wananchi), wana haki kwenye ardhi yao na kwamba mmiliki wa leseni ana haki kwenye madini, lakini anapigwa marufuku kuanza kazi bila kutimiza matakwa ya Sheria ya Madini Na. 14, 2010 kifungu cha 95 na 97” vifungu hivyo vinazungumzia malipo ya fidia.

Baada ya kupata fununu za barua ya Kamishna Masanja kwamba ameandika barua kwamba wananchi walishindwa mahakamani ilhali si kweli, wananchi hao waliamua kuwasiliana na kamishna moja kwa moja kupitia simu yake ya kiganjani na kumweleza, kwani vielelezo vya kimahakama havisemi kama barua yake ya Julai 2, 2014 inavyosema.

Septemba 30, mwaka huu mmoja wa wananchi hao, Seveline Malugu Magese, alifika jijini Dar es Salaam na kufanya kikao na viongozi wa Ofisi ya Kamishna Masanja, kikao ambacho pia kilihudhuriwa na kamishna mwenyewe.

Baada ya kikao hicho, Masanja alimwagiza msaidizi wake kuwaandikia wananchi hao barua ya kuwaondoa hofu kutokana na makosa aliyoyafanya ya kupindisha hukumu ya Mahakama, mara baada ya kuona vielelezo vya kimahakama na kugundua ‘aliingizwa mkenge’.

Barua hiyo (nakala tunayo), yenye Kumb. Na. DA.170/181/02 ya Oktoba 1, 2014 yenye kichwa cha habari ‘Malalamiko ya wakazi wa Kitongoji cha Nyantorotoro ‘A’, dhidi ya Bw. Majaliwa Maziku’ pamoja na mambo mengine inasema:

“Mgogoro wenu ulifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Geita pia Mahakama ya Ardhi ya Geita, ambapo haki za wananchi wanaomiliki ardhi na haki za mmiliki wa leseni ya madini zilifafanuliwa kwa mjibu wa hukumu ya Januari 28, 2013.”

Kipengele kingine katika barua hiyo kimegusia jinsi mwekezaji Maziku alivyofanya makubaliano yasiyo rasmi na baadhi ya wananachi, na kuwalipa fidia ambayo hawakukubaliana nayo ili apate eneo la kuweka mtambo wake wa kusaga kokoto lakini haikutengua barua yake ya awali iliyopindisha amri ya Mahakama”.

Barua hiyo, iliyokuwa na lengo la kujisafisha na kuwapoza wananchi kwa uamuzi aliokuwa amekwisha kuufanya na ambao umesainiwa na Injinia John Nayopa kwa niaba ya Masanja, ilisema, “Naomba ieleweke kwamba barua ya Kamishna wa Madini ya Julai 2, 2014 ilijikita katika kudhibiti uchimbaji haramu wa madini alioushuhudia ukiendeshwa na wananchi katika eneo la Nyantorotoro ‘A’ alipotembelea eneo hilo Juni 26, 2014.”

“Aidha, imeelezwa kwenye barua yetu kuwa mmiliki wa leseni ya madini aendeshe shughuli za uchimbaji madini kwa mjibu wa sheria. Hiyo ni pamoja na kuzingatia vipengele namba 95 na 97 vya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi kadiri inavyostahiki.”

Usikose sehemu ya pili ya ‘Nyundo ya Wiki’ wiki ijayo ambako tutawaletea namna Masanja ‘alivyosaliti’, historia ya mgogoro, kauli ya ofisa madini, tamko la mwekezaji, neno la kamanda wa polisi na mengine mengi.

1586 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!