Mwekezaji wa Kampuni ya Petrofuel Tanzania Limited, amemwomba Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati mgogoro wa kibiashara unaoipotezea Serikali mapato ya wastani wa Sh bilioni 4 kila mwezi kutokana na ubabe wa watu wachache, JAMHURI limeambiwa.

Satish Kumar, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Petrofuel ameliambia JAMHURI kuwa Kampuni yake kwa sasa inapoteza biashara ya wastani wa Sh milioni 300 hadi 400 kwa siku kiasi ambacho kingeiwezesha kampuni hiyo kulipa kodi iliyotajwa hapo juu na kuendelea kuajiri wafanyakazi Watanzania wapatao 150.

 Juni 24, 2016 kampuni ya Petrofuel siku hiyo wakiwa ofisini kwao wanaendelea na biashara, ghafla walivamiwa na kundi la ‘mabaunsa’ waliofunga ofisi na kurusha vitu nje huku wakituhumiwa kuiba baadhi ya mali. Inaelezwa kuwa walifanya hivyo bila kibali cha Mahakama. Kikosi cha Kutuliza Ghasi (FFU) nacho kilishiriki kadhia hii.

 “Tangu Juni 24, 2016 biashara zetu zimefungwa. Wafanyakazi tunao tunaendelea kuwalipa mishahara kutokana na vyanzo vyetu vingine kwa tabu. Tunapoteza mauzo, tunapoteza kodi ya serikali, tumewekeza mtaji mkubwa kujenga miundombinu, lakini tunahangaishwa bila kujua hatima yetu.

“Tumeambiwa kuna mgogoro wa kiwanja kati ya Kassam na Educational Book Publishers, sisi tunasema hatutaki kuingilia taratibu za Mahakama ingawa nazo tunaona hakuna kinachoendelea kwani tangu tufungue kesi hakuna maelezo au hatua yoyote iliyofikiwa kutoka mahakamani zaidi ya mazuio ya awali (preliminary objections) yanayozuia kesi kuanza kusikilizwa licha ya kupelekwa chini ya hati ya dharura.

 “Nimefikia uamuzi wa kumwomba Mheshimiwa Rais John Magufuli aingilie kati mgogoro huu, turuhusiwe kuingia katika ofisi zetu. Turuhusiwe kuendelea kuuza mafuta na bidhaa mbalimbali, hawa wenye mgogoro wao wakihitimisha sisi tutatekeleza matakwa ya Mahakama, lakini si kwa utaratibu huu waliofanya wao wa kutumia FFU nje ya utaratibu kutufurusha ofisini tukiwa wapangaji halali. Mheshimwa Rais Magufuli tunaomba utusaidie,” anasema Satish.

Wiki iliyopita gazeti hili limechapisha habari zikionyesha kuwa tajiri mwenye ukwasi wa kutisha anayeishi jijini Dar es Salaam ameamua kulitumia Jeshi la Polisi kutekeleza matakwa yake, kwa kuvamia ofisi za wapangaji na kufunga biashara zao bila kibali cha Mahakama.

Kampuni ya Petrofuel (T) Limited ilipangishwa na ndugu Hasham Kassam, ambaye aliwapa mkataba wa pango na anadai kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja chenye hati Na. 186074/21, lakini baadaye ikatokea kampuni ya Educational Books Publishers Limited, ikaddai yenyewe inamiliki kiwanja hicho pia kilichoko Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.

 Kampuni ya Educational Books Publisher, inamilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), anayetajwa kuwa na vitega uchumi kadhaa jijini Dar es Salaam na anayedaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa maafisa wa serikali.

Kampuni ya Petrofuel imepeleka malalamiko yake ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo nayo imeyashusha ofisini kwa Waziri Mkuu, aliyeitisha kikao kati ya wadau wenye mgogoro jijini Dodoma na kujadili mgogoro huo kisha wakubaliane jinsi ya kuumaliza.

Waliporejea jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliitisha kikao cha wadau kuwasuluhisha, ila katika kutafuta suluhu akatoa hitimisho kuwa Petrofuel watafute jinsi ya kuondoa mafuta yao yaliyopo kwenye ofisi zao zilizofungwa na mabausa wakishirikiana na FFU.

Pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani kati ya Kassam na Educational Book Publishers wakigombea uhalali wa umiliki wa kiwanja, huku kila mmoja akiwa na hati, Sirro alikiambia kikao cha pamoja kuwa Educational Book Publishers ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho.

Kampuni ya Petrofuel (T) Limited ilipeleka Mahakama Kuu hati ya kuomba kuzuia kuondolewa katika kiwanja hicho. Katika shauri hilo, kampuni ya Petrofuel na nyingine ya Isa Limited, zimewashtaki Educational Books Publishers Limited, Wilson Ogunde na Yono Auction Mart and Court Brokers.

 Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Lugano Mwandambo, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Julai 21, mwaka jana. Uamuzi wa au kutoa, au kutotoa hati ya zuio ulitarajiwa kutekelezwa wiki mbili baadaye, lakini hadi mwaka huu haujatolewa.

Kampuni hiyo inasema uvamizi na kufunga ofisi zao ulifanywa kwa nguvu na hivyo kusababisha hasara kubwa ya mali na fedha.

“Uamuzi wa kutuondoa katika eneo linalozungumzwa katika shauri hili litatusababishia hasara ya kati ya Sh milioni 200 hadi Sh milioni 400 kwa siku. Waliingia hapa na mashine zinazotumia gesi kukata milango pamoja na makufuli,” inasomeka sehemu ya shauri hilo.

Katika shauri hilo, kampuni ya Petrofuel (T) Limited inasema kuna matangi sita ya mafuta ya dizeli yenye lita 278,000 pamoja na vipuli vya mitambo na magari kwa ajili ya migodi ya madini.

 Kampuni hiyo inasema endapo haitaruhusiwa kuokoa mali hizo, itafilisika kutokana na kutopewa fidia na taasisi za kifedha.

Kamishna Sirro ambaye Oktoba 12, 2016 aliitisha kikao ofisini kwake Dar es Salaam kuhusiana na suala hilo, kwa sasa ameliambia JAMHURI kuwa suala hilo limekwisha, wakati bado suluhu haijapatikana.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Sirro mwenyewe, Naibu Kamishna wa Polsi, Hezron Gimbi, Gilles Mroto, wakili wa Educational Book Publishers, Wilson Ogunde, mmiliki wa Educational Book Publishers, Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), Wakili wa Petrofuel, Dk. Masumbuko Roman Lamwai na Makamu wa Rais wa Petrofuel, Mshamsham D. Mfuru.

Katika barua ya Mwanasheria wa Petrofuel, Dk. Lamwai kwenda kwa Sirro ya Oktoba 18, 2016, yenye Kumb No. PETRO/2016/14, Dk. Lamwai anamkumbusha Sirro kutekeleza aahadi yake ikiwamo kuiomba radhi Kampuni ya Petrofuel na kuwarejesha katika jengo walikotolewa.

“Kamishna Sirro alisema wazi kuwa kuhusishwa kwa polisi katika kuwaondoa [Petrofuel] kwa amri ya Naibu Kamishna wa Temeke, hakukuwa sahihi na bila hati yoyote ya mahakama.

“Kamishna Sirro alisema kuwa kuondolewa kulikofanyika Juni 24 [2016], kulikuwa kinyume cha sheria. Aliomba radhi kwa niaba ya FFU na Jeshi la Polisi. Aliahidi pia kuchukua hatua za kinidhamu kwa waliohusika.

“Kamishna Sirro alisema pia kuwa amewasiliana na Mahakama na hakukuwapo amri yoyote kutoka mahakamani iliyoruhusu kuwaondoa [Petrofuel],” inasema sehemu ya barua ya Lamwai inayonukuu kumbukumbu za kikao cha Oktoba 12, 2016.

 Wakili wa Kampuni ya Educational Book Publishers, Wilson Ogunde, amesema miongoni mwa uamuzi uliofikiwa katika kikao na Kamishina Sirro baadhi ya Wafanyakazi wa Petrofuel waliomba kwenda kufunguliwa ofisi kuchukua hati zao za kusafiria na kinachotakiwa sasa ni Petrofuel kuondoa mafuta yaliyopo kwenye matangi.

“Baada ya kufanyika uchunguzi wa mgogoro huo, Kamada Sirro alibainisha kuwa baada ya Serikali kupitia nyaraka zote eneo hilo ni la Educational Book Publisher… Polisi walikuja eneo la tukio baada ya kupata taarifa kuwa kuna mgogoro na walifika kwa ajili ya kuwaondoa watu wa Educational Book Publisher,” anasema Ogunde.

Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), alipotafutwa na JAMHURI, alisema kwa ufupi: “Mtafute wakili wnagu ndiye azungumzie yote hayo.”

Kampuni ya Petrofuel inasema haioni mwanga kwani kila kona inayokwenda ufumbuzi ilioutarajia iwe kwa njia ya kimahakama au kiutawala haioni ukizaa matunda, hivyo wameomba Rais Magufuli aingilie kati waweze kuendelea na biashara yao ya mafuta yaliyopo kwenye matangi ambayo yanaweza kulipuka wakati wowote na waendelee na biashara hadi mkataba wao wa pango utakapomalizika.

Wiki iliyopita Ofisi ya Waziri Mkuu, iliahidi kuwa inaendelea na mchakato wa kulishughulikia suala hili, hivyo ikaahidi kulitolea majibu mara watakapokamilisha hatua muhimu.

1841 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!