Magazeti kadhaa yameripoti kwamba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Musukuma, amewaambia wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Nyawilimilwa kilichopo Kata ya Kagu, kwamba hatakuwa tayari kupeleka maendeleo katika kata hiyo kwa sababu inaongozwa na Diwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Tumeambiwa kwamba chanzo cha kauli hiyo kali ni kutokana na swali la mwananchi Etanga Tito. Wakati mwenyekiti akitoa kauli hiyo nzito, miongoni mwa waliokuwa wakimsikiliza ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Moses Minga, na Ofisa Mipango wa Wilaya hiyo, Frank Makonda.

Amenukuliwa akisema, “Nilitumia gharama kubwa sana wakati wa uchaguzi uliopita wa udiwani, lakini wananchi wa kata hii mkanisaliti na kumchagua Lukondo Mkukura wa Chadema. Mlifanya hivyo kwa sababu zenu wenyewe na hii inatokana na ninyi wenyewe kuendekeza makundi na ukabila. Kwa hiyo naomba mkome kabisa na hayo ndiyo matunda ya kuchagua upinzani.

 

“Kutokana na tabia mliyoifanya, niko tayari kumzuia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya asiwaletee fedha za ruzuku zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ili liwe fundisho kwa watu wengine wanaoacha kuchagua CCM na kuchagua vyama vya siasa vya upinzani, husasani Chadema.

 

“Chadema hawana uwezo wa kuwaletea maendeleo katika kata hii na ni vigumu pia na mimi kuwaletea maendeleo ama kuruhusu miradi ya maendeleo ije kwenu. Huenda nifanye hivyo kwa huruma tu ya chama changu, kwa sababu nyingi wenyewe mlichagua shetani, acheni mkome.”

 

(Tukitaka tunaweza kujiuliza alitumia gharama ya kufanyia nini).

 

Baada ya kuwaona wananchi wakiwa wamepigwa ‘ganzi’, Makonda alisimama na kuwahakikishia kuwa kero ya ukosefu wa zahanati inayowakabili, Halmashauri yake itaitatua.

 

“Msiwe na wasiwasi, zahanati yenu itakamilika na mtaondokana na matatizo yanayowakabili,” Makonda aliwaambia wananchi hao katika mkutano ambao licha ya kuwa ni wa kiserikali, uliendeshwa ndani ya Ofisi za CCM.

 

Hadi naandika makala hii, Musukuma hajajitokeza kukanusha habari hizo. Hii haina maana kwamba hajapata taarifa kwamba zimeandikwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Ukimya wake unathibitisha kuwa alichokisema ndicho kilichoandikwa. Pengine si ajabu kwamba anasikitika kwa kutorusha makombora makali zaidi ya hayo ili ujumbe uwafikie walengwa!

 

Kama kweli Mwenyekiti wa chama kinachoongoza Serikali anaweza kutoa kauli za unyanyapaa kiasi hiki, itoshe kumweka kwenye kundi la viongozi wapuuzi. Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la Pili, iliyotungwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam, inamtaja mpuuzi kuwa ni, “Mtu mwenye tabia ya kufanya mambo yasiyokuwa na maana; mtu asiyestahili kufuatwa mambo yake.” Kwa maneno mengine, mtu mpuuzi ni bahaimu.

 

Kwa kuzingatia tafsiri hii, na kama kweli Musukuma hayo yaliyoandikwa na kutangazwa yalitoka kwenye kinywa chake, basi ana kila aina ya sifa inayomfanya astahili kuitwa mpuuzi.

 

Sisi tunaolilia umoja wa Taifa letu, mara zote tulipojaribu kuwakosoa watawala (si viongozi) wa CCM, tumeonekana kuwa ni wapinzani. Kuwa mpinzani, kwa baadhi ya watu wenye akili za kina Msukuma, maana yake ni kosa kubwa! Mfumo wa siasa wa vyama vingi ulirejeshwa nchini mwaka 1992. Kuwapo kwa mfumo huo kunatoa uhuru kwa kila mwananchi mwenye akili timamu na sifa stahiki, kujiunga katika chama chochote cha siasa kinachomfaa.

 

Isitoshe, mtu yeyote mwenye sifa zilizoainishwa kwenye Katiba na sheria mbalimbali nchini mwetu, ana sifa za kuamua kumchagua nani awe kiongozi gani, bila kujali anatoka chama gani.

 

Mara kadhaa kumekuwapo malalamiko ya msingi kabisa kutoka kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani ya kwamba wananchi katika maeneo yenye viongozi wa kuchaguliwa kutoka vyama tofauti na CCM, wananyanyaswa kwa kunyimwa huduma kadhaa za maendeleo.

 

Aprili, mwaka huu, nilikuwapo bungeni wakati Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alipomwuliza Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu hali hiyo katika maeneo yanayoongozwa na wapinzani.

 

Pinda akasema Serikali inatoa fedha za maendeleo bila ya ubaguzi wa itikadi, lakini ukweli  ni kwamba hali ni tofauti kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, kutokana na madiwani wa CCM kutaka kata zinazoongozwa na upinzani zisipewe miradi mipya ya maendeleo.

 

Mbowe alimtaka Pinda atoe msimamo wa Serikali kutokana na kauli zilizowahi kutolewa na mawaziri kadhaa, kama vitisho kwa wananchi kuwa wakiwachagua wapinzani hawatapata maendeleo.

 

Katika Wilaya ya Serengeti, Kamati ya Madiwani baada ya uchaguzi iliweka misimamo wa kutopitisha fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa, huku wanafunzi wakilazimika kukaa zaidi ya miezi saba nyumbani hadi ujenzi ulipokamilika kwa michango ya wazazi na wadau wa elimu.

 

Katika kikao cha Bajeti cha Madiwani kilichoketi Aprili, mwaka huu, madiwani hao ambao wengi wanatoka CCM walipendekeza miradi ya ujenzi wa barabara katika Kata za Nyansurura na Machochwe, zinazoongozwa na upinzani ziondolewe na badala yake zipelekwe kata zenye madiwani wa CCM.

 

Ndugu zangu, nimejaribu kurejea haya mambo kutokana na kauli hii ya Musukuma ambayo kivitendo inatekeleza dhana ya kuwatenga wananchi ambao kwa uhalali wa Katiba ya nchi, wameamua kuwachagua viongozi wanaowataka.

 

Musukuma amesema, “Huenda nifanye hivyo (awasaidie) kwa huruma tu ya chama changu, kwa sababu ninyi wenyewe mlichagua shetani, acheni mkome.”

 

Maneno haya ni matusi mazito kweli kweli kwa wananchi wa Kata ya Kagu na wapenda demokrasia nchini kote. Kuifananisha Chadema au vyama vya upinzani na shetani ni matusi yaliyovuka mpaka. Nitashangaa kama kweli wanachama, wafuasi na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani watamwacha Mwenyekiti huyu bila kumfikisha katika Mahakama.

 

Miradi mingi ya maendeleo, hasa inayotekelezwa na Serikali Kuu au Serikali za Mitaa, ni matokeo ya kodi zinazolipwa na Watanzania wote. Hakuna barabara inayojengwa kwa fedha za wanachama wa CCM. Hakuna zahanati zinazojengwa kwa fedha za kitu kinachoitwa chama tawala. Mfuasi wa Chadema anapokunywa soda au bia, analipa kodi kama ilivyo kwa wale wa CCM, UDP, CUF au hata wasiokuwa na ushabiki au uanachama wa chama chochote cha siasa. Kodi zote zinakusanywa bila kujali itikadi ya Mtanzania.

 

Kama hivyo ndivyo, ni lazima maendeleo nayo yasambazwe katika Taifa letu kwa uwiano. Tena basi, kuna vijiji, kata na majimbo yenye wana-CCM wengi, lakini kwa kutowakubali wagombea wa chama hicho, wakati wa uchaguzi waliamua kuwachagua wanachama wa vyama vingine. Kuwaadhibu wananchi kwa kudhani kwamba waliomkataa mwana-CCM si wana-CCM, ni upuuzi wa kifikra. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 hakusita kutamka wazi kuwa kura yake ya ubunge Jimbo la Musoma Vijijini alimpa Balozi Paul Ndobho aliyekuwa NCCR-Mageuzi. Akamnyima mgombea wa CCM kwa sababu aliamini hakuwa na sifa.

 

Kwake Mwalimu, Tanzania ilikuwa zaidi ya CCM. Kwake chama hakikuwa na maana zaidi kuliko masilahi ya nchi na wananchi. Hawa wapuuzi wanaohubiri kuwatenga wananchi walioamua kuwachagua wapinzani, ndiyo hao hao wanaojiweka mbele wakitaka watambulike kuwa wanamuenzi Mwalimu.

 

Tanzania ni nchi yetu sote. Tulipoukubali mfumo wa vyama vingi, hata ukaweza kuingizwa kwenye Katiba, maana yake ni kwamba jambo hili ni la kisheria. Anapotokea kiongozi mwendawazimu akawaona walioikataa CCM kuwa ni watu hatari wasiostahili kutendewa haki kwa mujibu wa kodi wanazolipa, lazima tuungane kumkataa.

 

Chama Cha Mapinduzi sasa kina viongozi makini. Litakuwa jambo la busara sana kwa Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kutoa kauli ya kuwakemea vikali wana-CCM wanaohubiri ubaguzi wa kiitikadi. CCM haiamini katika ubaguzi. Viongozi aina ya Musukuma ni wa kuogopwa kwa sababu wanapandikiza mbegu ya chuki katika medani ya siasa nchini mwetu.

 

Lakini kubwa zaidi ni kwamba leo anaweza kuwaona Chadema kuwa ni wapinzani, lakini siku moja akashangaa kuona CCM ndiyo wanaokuwa wapinzani. Jambo kama hilo si la ajabu, isipokuwa linaingia kwenye vichwa vya watu wenye akili zisizofanana na za Musukuma. Nani alijua kuwa KANU itabaki kwenye makabrasha? Nani anayejua ilipo leo UPC ya Uganda? Wapi ilipo UNIP ya nchini Zambia? Lakini je, waliokuwa KANU, UPC, UNIP na vyama vingine si kweli kwamba bado wapo hai wakishuhudia watawala wa nchi wakiwa wengine? Kina Musukuma ni wa kupuuzwa.

 

By Jamhuri