Na Charles Ndagulla, Moshi

Mfanyabiashara Bosco Kyara na mwenzake Gabriel Mombuli, wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa magari katika nchi za Kenya na Tanzania wamesafirishwa kwenda nchini Kenya kujibu mashtaka ya wizi wa gari.
Kyara ni mkazi wa Makuyuni katika Mji Mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi Vijijini, wakati Mombuli ambaye anafanya shughuli za udereva, anaishi eneo la Majengo Shauri Moyo katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kabla ya kusafirishwa kwenda nchini Kenya, watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai na kusomewa mashtaka mawili likiwamo la unyang’anyi wa kutumia silaha na kupatikana na mali inayoaminika kuwa ni ya wizi.
Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa siku na muda usiojulikana mwaka huu huko Nairobi nchini Kenya, washtakiwa waliiba gari aina ya Nissan V8 lenye namba za usajili KCP 184R mali ya Kampuni ya Nisk Capital Limited.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Hawa Hamis, washtakiwa hao kabla na baada ya kuiba gari hilo walimtishia kwa bastola Luke Indechi Abboo.
Shtaka la pili ni washtakiwa hao kupatikana na mali inayoaminika kuwa ya wizi, ambapo Agosti 19, mwaka huu saa 1:30 usiku katika kizuizi cha Polisi eneo la Kwa Msomali, Wilaya ya Hai walikutwa na gari aina ya Nissan Patrol V8 lenye thamani ya Sh milioni 200 mali ya Kampuni ya Nisk Capital Limited ya Kenya.

JAMHURI limebaini kuwa washtakiwa hao walichukuliwa na polisi wiki iliyopita kutoka Gereza Kuu la Mkoa wa Kilimanjaro, Karanga na kupelekwa mahakamani ambako walifutiwa mashtaka na kusafirishwa kwenda nchini Kenya kupitia mpaka wa Tarakea.
Wakili Julius Semali aliyekuwa akimtetea mfanyabiashara Bosco Kyara, amelalamikia hatua iliyochukuliwa na polisi ya kuwasafirisha washtakiwa hao kwenda nchini Kenya bila kufuata taratibu za kisheria.
“Nilipata taarifa kutoka kwa mke wake (Haika), aliniambia wamenyakuliwa na kupelekwa Kenya, walipelekwa mahakamani polisi wakafuta jalada na kuwapeleka pale Tarakea na kuwakabidhi kwa askari wa Kenya,” amesema Wakili Semali.

Amesema yeye kama wakili aliyekuwa akimwakilisha mshtakiwa hakushirikishwa kwa namna yoyote na kwamba tayari amewasilisha barua ya malalamiko ofisi ya Wakili wa Serikali mjini Moshi kwa kile alichodai taratibu za kisheria hazikufuatwa.
Kwa mujibu wa wakili huyo, katika kubadilishana wahalifu wa makosa ya jinai kati ya nchi na nchi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ingeshirikishwa pamoja na yeye kama wakili anayemwakilisha mshtakiwa huyo lakini hilo halikufanyika.
Amesema tukio la mteja wake kupelekwa Kenya bila tararibu za kisheria kufuatwa limemuumiza, huku akidai hawezi kulisemea kwa kuwa tayari jambo hilo limeshafanyika na sasa wanachosubiri ni kauli kutoka ofisi ya Wakili wa Serikali.

Tangu kufikishwa mahakamani hapo kwa washtakiwa hao, upande wa mashtaka ulikuwa ukisisitiza kuwa zipo taratibu za kisheria zinazopaswa kufanyika washtakiwa wasafirishwe kwenda nchi nyingine kujibu mashtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, amethibitisha kusafirishwa kwa watuhumiwa hao kwenda nchini Kenya huku akiwataka wanaohoji mazingira ya kusafirishwa kwao wawasiliane na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) kupewa ufafanuzi.
Kamanda Issah amesema mbali na watuhumiwa hao kukabidhiwa kwa polisi wa Kenya, gari aina ya Nissan Patrol V8 lenye namba za usajili KCP 184R  ambalo lilikamatwa mikononi mwa watuhumiwa hao nalo limerejeshwa nchini Kenya.

By Jamhuri