Wiki iliyopita nilibainisha kuwa kiini cha tatizo la ufisadi wa nchi hii inaonekana hakijabainika; ndiyo maana tunahangaika na matokeo badala ya kiini.
Kutokana na hilo nilisema huenda tatizo la ufisadi wa nchi hii halipo katika mapigo ya kutisha kama yanavyocharazwa na wanasiasa.

Katika kuhitimisha nilieleza tatizo la habari nyepesi  linalotusumbua sana Watanzania. Huku mitaani kuna kitu kinachoitwa “redio mbao”. Kupitia redio hizi unaweza kusikia habari za kusisimua na kushangaza.

Kupitia redio mbao unaweza kusikia, “Mbunge fulani wa viti maalumu amepata ubunge kwa kuhonga ngono”, “Waziri fulani anatembea na msanii fulani”, “Tajiri fulani anatumia ushirikina kupata mali alizonazo n.k”. Habari nyepesi zina sifa kuu mbili; zinavutia kusikiliza, na zinaaminika kirahisi.

Tatizo lake ni kuwa huwezi kuzikanusha wala kuzithibitisha kirahisi. Kwa maana hiyo, habari nyepesi zinapotufikia Watanzania wengi ambao ni wavivu wa kutafiti na kuchunguza mambo-zinaleta sumu mbaya sana.

Wakati fulani nilikuwa Tunduma, mji ulio mpakani mwa Tanzania na Zambia na wenye harakati za kibiashara mkoani Mbeya. Hapo nikakutana na habari nyepesi zilizozagaa mitaani kuhusu kampuni moja ya mafuta. Nikasikiliza watu wakisema kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na mtoto wa mmoja wa vigogo wakubwa serikalini.

Kwa ujasiri kabisa wakawa wakieleza kuwa fedha za kuanzisha kampuni hiyo zimekwapuliwa serikalini. Hasira zao zilionyesha kuwa wapo tayari hata kuyachoma moto magari ya kampuni hiyo wakati wowote wakipata nafasi. Nikiwa njiani kurudi Iringa ndani ya basi nilimopanda, nikakutana na habari zile zile nilizozisikia Tunduma.

Kila tukipishana na gari la mafuta la kampuni ile nilisikia abiria tofauti wakisema, “Ona (wanamtaja kwa jina) huyo…amenunua haya magari mia moja na unaambiwa ameagiza pia mabasi mia moja”.  Ngoja Chadema iingie madarakani, watanyang’anywa kila kitu na wakaozee jela,” abiria mwingine alidakia na kukuza mjadala.

Hadi nashuka Makambako na kuliacha basi likiendelea na safari, nilikuwa nimesikia mtoto huyo wa kigogo akiwa ni mmiliki wa hoteli mpya, maghorofa mapya na kampuni karibu katika kila mkoa nchini Tanzania. Kama nilivyosema awali, tetesi kama hizi ni vigumu mtu kama mimi ninayesikia, kuzikanusha au kuzithibitisha; labda mhusika mwenyewe.

Hata hivyo, wakati mazungumzo yakiendelea kuhusu kampuni ile ya mafuta, niliwauliza “maripota” wa habari ile, “Hii kampuni imeanzishwa lini?” Asilimia mia moja walinijibu hivi, “Imeanzishwa baada ya baba yake (huyo kigogo) kuingia serikalini”.

Habari hiyo hata mimi ilinisisimua kweli kweli kiasi ambacho nikaona ngoja niitafiti hii kampuni ambayo kwa mujibu wa redio mbao inaonyesha imeota kama uyoga. Nilishtushwa sana na kitu nilichogundua. Kampuni hiyo inaonyesha ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 katika nchi jirani. Ni kampuni iliyoingia nchini kabla hata huyo kigogo hajaingia serikalini na imesambaa katika nchi zaidi ya saba Afrika Mashariki na Kati.

wa haraka haraka nikabaini mambo mawili. Mosi, inaonekana watu wengi wanazo taarifa nusu, zilizopikwa au za ushabiki wa kisiasa kuhusu kigogo huyo (na vigogo wengine) kuhusu kampuni hiyo pamoja na kampuni nyingine zinazohusishwa na viongozi serikalini. Pili, nikatambua kuwa kuna sumu mbaya ya kuunganisha umasikini na uadilifu wa viongozi.

Hebu fikiria kinachoweza kutokea pale vigogo wa serikali na familia zao wanapohusishwa na umiliki wa kampuni au biashara fulani! Kwanza, vigogo hao na familia zao wanahukumiwa kuwa ni wezi pasipo hata uthibitisho, pili kuna hatari inayowapata wajasiriamali ambao ni wamiliki halisi wa kampuni zinazotuhumiwa.

Uzoefu unaonyesha kuwa biashara ikihusishwa na wizi wa kodi za wananchi; moja kwa moja walipakodi (wananchi) huichukia biashara husika na wamiliki wake. Siku ukisikia maandamano ya vurugu uwe na uhakika watu watatembea na petroli na viberiti ili kuchoma mali wanazodhani viongozi wa serikali wameiba fedha na kuzipitishia kwa wafanyabiashara fulani fulani.

Wakati wa mgogoro wa baada ya uchaguzi nchini Kenya, baada ya Raila Odinga kumtisha Mwai Kibaki aachie kiti cha urais bila mafanikio; Odinga aliibuka na mbinu ya kibiashara katika kumshinikiza Kibaki. Odinga akapiga mbiu kwa wafuasi wake wote kususia bidhaa na huduma zinazotolewa na kampuni zinazomilikiwa na Kibaki na washirika wake.

Wafuasi wake walitii na kampuni hizo ambazo zilikuwa zaidi ya 50 zilikumbana na hasara ambayo hazitaisahau. Pamoja na mambo mengine, msukumo wa hasara hii ulimshinikiza Kibaki kukubali yaishe ‘kiaina’ kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Wana heri wenzetu Wakenya ambao ubepari uliota mizizi kabla na baada ya uhuru wao. Nchini Kenya kiongozi hapati tabu kuonyesha wazi biashara na kampuni anazomiliki na wananchi wanajua kwa uwazi kuwa waziri mkuu anamiliki hisa fulani kwenye kampuni fulani; mke au mtoto wa rais anamiliki biashara fulani.

Hapa Tanzania tuna blanketi la Ujamaa (ambao umeshajifia) kiasi ambacho kiongozi anapomiliki biashara au kampuni, kwanza yeye mwenyewe anaogopa. Anakimbia kivuli chake mwenyewe! Viongozi wa Tanzania wanapoanzisha biashara au kampuni wapo tayari kutumia majina ya ndugu au jamaa zao wa karibu ilimradi tu wasijulikane, kwa sababu wanataka wananchi waendelee kuwaona ni waadilifu!

Sasa najiuliza, itakuwaje siku Tanzania tukipatwa na mgogoro kama wa Kibaki dhidi ya Odinga? Hapa patakuwa hapatoshi kwa sababu orodha ya kampuni zitakazohususiwa itazikumba zilizomo na zisizokuwamo. Na hili nalibashiri kwa sababu habari nyepesi kuhusu umiliki wa viongozi wa kampuni mbalimbali zimesambaa na zimeaminiwa.

Na kwa kuwa Watanzania wengi (wakiongozwa na wanasiasa) hawaamini katika mafanikio ya kiuchumi; huenda ikaenda mbali zaidi ya kususia kununua bidhaa na huduma.

Nimesema “hawaamini” katika mafanikio ya kiuchumi nikijifunza kutoka katika lile sakata la waziri kumiliki nyumba ya kifahari. Kuna mwanasiasa mmoja nilimsikia akisema, “Kijana mdogo kama yule, ameingia kwenye uwaziri juzi tu anapata wapi fedha nyingi kiasi hicho hata aweze kununua hekalu lile?”

Hoja ile ilionekana kuungwa mkono na vyombo vingi vya habari na kushadadiwa. Kilichoonekana mali zilizopotea katika wizara ya waziri yule ndizo alizotumia kujenga hekalu lile. Ina maana kuwa wengi wameona haiwezekani kwao ndiyo maana wanaamini haiwezekani kwa wengine.

Sikusikia wanasiasa wala vyombo vya habari vikilitazama sakata la umiliki wa nyumba ile kwa upana wake. Kama waziri yule alieleza kuwa ana biashara zake ni wangapi walijishughulisha kuchunguza makadirio ya faida anayozalisha katika biashara zake?

Je, biashara anazomiliki waziri yule haziwezi kumuwezesha kuchukua mkopo benki unaoweza kujenga hekalu lile? Je, kwa kutumia marupurupu na mshahara wake, waziri huyo hawezi kupata mkopo benki na kujenga au kununua hekalu lile?

Sasa chukua faida anayopata kwenye biashara zake, changanya na mkopo anaoweza kupata kwa kutumia dhamana na biashara zake, changanya na mshahara, marupurupu na mkopo anaoweza kupata kwa kutumia mshahara wa uwaziri; je, haiwezekani kujenga hekalu la Sh bilioni 1.5 au la takribani shilingi milioni 700 kama alivyosema mwenyewe?

Huu utamaduni wa kuyatazama maendeleo ya viongozi au familia zao kisha kuyaunganisha na ufisadi ipo siku kitanuka ‘live’ kama wanavyosema watoto wa “facebook”. Leo viongozi wa serikali ya CCM ni waathirika wa mtazamo huu, lakini sumu hii haitakihurumia chama chochote kitakachoingia madarakani baada ya CCM.

Ninapoendelea naomba nieleweke kuwa sitetei wezi wa mali za umma (tena wanapothibitika mahakamani ni heri hata wanyongwe), lakini nataka tuwekane sawa ili tusichanganye juhudi binafsi za viongozi au mwananchi wa kawaida kujikwamua kiuchumi; na ufisadi.

Na laiti tusipoamua kuliweka suala hili sawa, tutaendelea kuzalisha viongozi wezi kwa sababu ya kukosa uwezo wa kutumia vichache (mshahara) kuzalisha vingi ambao ndiyo msingi wa dhana ya ujasiriamali. Badala yake wataendelea kuiba.

Tuonane wiki ijayo.

0719 127 901, [email protected]

By Jamhuri