magufuli1Nabii Joseph Buberwa, ametoa mwito kwa mamlaka zinazohusika kumwezesha kuonana na Rais John Magufuli.

Anasema yeye si nabii kama manabii wengine wa kisasa waliojaa duniani, wakidai wanahubiri injili na kufanya miujiza mbalimbali.

Katika mahojiano maalumu na JAMHURI, Buberwa anasema: “Mimi si nabii ambaye nataka kuwa na kanisa au kikundi cha waumini na kutegemea sadaka za waumini na kuanza kuwahubiria na kufanya miujiza. Mimi ni nabii maalumu kwa kutimiza makusudi maalumu ya Mungu ambayo yanapaswa kuanza kutokea duniani katika kipindi cha kizazi hiki, kama ambavyo gharika ya wakati wa Nuhu ilikuja na kupita.”

Anasema yeye ni nabii aliyetabiriwa na Mungu wa Kweli, Mungu Muumba, karibu miaka 3,500 iliyopita kupitia Nabii wake Musa, wakati akiwa katika Jangwa la Sinai akiwaongoza wana wa Israeli kuelekea Kanaani baada ya kuwakomboa kutoka utumwani Misri.

“Ulikuwa mwaka wa 1473 KWK katika Jangwa la Sinai, katika maono Mungu alimpatia Musa unabii huu ambao ulinukuliwa katika andiko la Kumbukumbu la Torati 18:18,19 unaosema: ‘Nitawainulia wao nabii kutoka katikati ya ndugu zao, kama wewe; nami nitaweka maneno yangu katika kinywa chake, naye atasema nao yote nitakayomwamuru. Na itatukia kwamba mtu ambaye hatasikiliza maneno yangu ambayo atayasema katika jina langu, mimi mwenyewe nitamtaka ajibu’.”

Nabii Buberwa anamwomba Rais Dk. Magufuli, Tanzania na dunia kufanya kile anachosema kufunguka akili na kuelewa kuwa sasa unabii huo wa Kumbukumbu 18:18,19 kwa sasa umepata utimizo.

“Kila unabii ambao Mungu aliutoa ndani ya maandiko yake una wakati utatimia kulingana na ratiba yake Mungu na kwa njia yake.

“Unabii huo umetimizwa kwake tangu Machi Mosi, 2009 saa 7 mchana. Tarehe hiyo ni siku ambayo Mungu alifungua kipindi cha Mahakama ya Mungu wa Kweli hapa duniani, kipindi kilichotangazwa kwa miezi sita na mimi mwenyewe katika Televisheni ya Star Tv.

“Mungu aliniamuru kukifunga rasmi kipindi hicho tarehe 30/08/2009, siku ambayo ilikuwa ni siku yangu ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 40 kamili. Ni kama Musa alipotimiza miaka 40 alipewa maono ya kuwakomboa wana wa Israeli (ukitaka kuona maagizo ambayo Mungu aliyatoa kupitia mimi katika mahakama hayo fungua YouTube na andika, ‘nabii Buberwa,’ utaletewa vipindi mbalimbali vya Mahakama ya Mungu nilivyotangaza),” anasema.

Nabii Buberwa anasema jambo kuu analofanya ni kumhimiza Rais John Magufuli kumpatia nafasi ya kuonana naye ana kwa ana kwa kuwa ana maagizo makubwa tangu mwaka 2012 kutoka kwa Mungu kwa faida ya Tanzania na dunia.

“Kila jambo lina wakati wake. Wanadamu tumeishi karibu miaka 2,000 bila ya dunia kushuhudia maagizo ya moja kwa moja kwa watawala wa dunia kutoka kwa Mungu. Watawala wa ndani ya kipindi hiki wamekuwa wakitawala kulingana na utashi wao au wakiongozwa na katiba za nchi zao.

“Watu wa imani zote wanakubali matukio mbalimbali yaliyofanywa na Mungu hapa duniani kwa kupitia baadhi ya watu, manabii na mitume. Kama tukio la gharika ya nyakati za kina Nuhu, Mungu alimpa maagizo Nuhu asimamie kazi ya kujenga safina na papo hapo akampa jukumu la kuonya watu juu ya gharika. Watu wa nyakati zake walimpuuza hadi mwisho, ikasababisha gharika- waliokoka watu wa familia yake waliomtii yaani watu wanene tu. Wanadamu wengine wote duniani, wa kipindi chake waliangamizwa kwa sababu ya ubishi wao.

“Pia, sote tunakumbuka visa kama vya akina Abrahamu, Yakobo, Isaka, Ayubu n.k. na jinsi Mungu alivyowatumia katika nyakati zao. Kuna nabii Musa ambaye amenukuliwa katika andiko la hapo juu kuwa alipewa maono na Mungu kuinuliwa nabii kama yeye kwa ajili ya ukombozi wa ndugu zake wa wakati unaokuja na ambako unabii huo umetimizwa kwa Buberwa.

“Nabii Musa wa nyakati za kale aliagizwa na Mungu kwa Farao awape ruhusa watu wake Israeli. Farao alikaidi mara zote ambazo Musa alimfikishia agizo la Mungu la kuwakomboa Israeli. Matokeo yake ni Farao na taifa lake la Misri kupata mapigo kumi hadi Farao alikubali kushindwa na Mungu na hatimaye akawapa ruhusa Israeli wakatoka, wakiongozwa na Musa kwa niaba ya Mungu.

“Vivyo hivyo kwa sasa Mungu amenipa maagizo ambayo lazima yasikilizwe kwanza na mtawala mkuu wa Serikali ya Tanzania, yaani Rais kama ambavyo Mungu alimtuma Musa kwa Rais wa Misri, Farao kwa wakati huo,” anasema.

Nabii Buberwa anasema tangu Septemba, 2012 alianza kuiandikia Ikulu juu ya kusudio la kumuona Rais kwa ujumbe maalumu wa Mungu; lakini utawala wake ulipuuza kusudio hilo hadi mwisho wa utawala wake.

“Utawala wa Mheshimiwa Kikwete tokea wakati huo alipopuuza maagizo ya Mungu ya kukutana naye; utawala wake ulianza kupata misukosuko ya kiutawala na kiuchumi na utengano wa taifa. Ulikuwa ukidorora kila siku hadi alipomaliza utawala wake kwa aibu kama ambavyo nabii (yeye Buberwa) alimtabiria.

“Sasa Mungu ameagiza maagizo ambayo angepaswa kuyasikiliza Mheshimiwa Kikwete akapuuza, yanapaswa kusikilizwa na mtawala mpya wa sasa wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli,” anasema.

Anasema kabla na baada ya Rais Magufuli kuingia Ikulu, ameomba kwa njia za mbalimbali, zikiwamo za makala, juu ya kusudio la Mungu la kumuona na kumpa maagizo ambayo yatafanya Tanzania kuwa taifa kubwa duniani na dunia kupata ukombozi.

“Taifa linapaswa kujivuna kuwa tumepata kiongozi anayependa watu wake na taifa, lakini pamoja na nia njema aliyonayo Rais John Magufuli, kama atapuuza maagizo ya Mungu kwa ajili ya kukomboa watu wake duniani bado utawala wake hautafanikiwa.

“Uchumi wa nchi hautuweza kukua kwa kiwango kikubwa na bado nchi itaendelea kukumbwa na migogoro midogo kwa mikubwa hadi hapo Rais atakapokubali kukutana nami ndipo taifa litapata dira ya maisha bora kwa taifa na watu wake,” anasema.

Anaongeza: “Kama makala zilizowahi kuandikwa magazetini na taarifa kupelekwa Ikulu, ni kwamba Mungu anataka kuelekeza Tanzania na dunia kwa kupitia utawala wa Tanzania, kwa kutumia hekima ya Mungu. Kwa mara ya kwanza kwa dunia; vita itakoma duniani ndani ya kipindi kifupi.

“Mungu ana ajenda ya kukomesha njaa, umasikini, uovu, ugaidi, rushwa na ufusika duniani kwa watu wake ndani ya miaka 10 iliyobaki baada ya 14 tokea Novemba 5, 2012. Sasa, makusudi haya hayawezi kuanza kutimia bila protokali ambayo Mungu anataka kufuatwa, ambayo ni mtawala anayetawala Tanzania kuhabarishwa kwanza mipango hiyo.

“Wakati wa Musa wa kuwakomboa wana wa Israeli, haikuwezekana kuwatoa Israeli kutoka Misri bila ya ruhusa ya mfalme wa wakati huo, yaani Farao. Mungu alikuwa ana uwezo wa kuwatoa wana wa Israeli nchini Misri kwa nguvu bila kusubiri ruhusa ya mtawala mkaidi na mwenye dharau- Farao, lakini hakuwatoa hadi Farao kwa kauli yake alipowaaambia akina Musa kuwa sasa watoeni Israeli.

“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania na ndugu yangu Rais, Mheshimiwa Magufuli; Mungu anaweza kutimiza mambo yote anayotaka kwenye taifa hili na duniani, lakini amechagua kufuata protokali ya kueleza makusudi yake kwako, ukiwa mtawala wa taifa hili ambalo litakuwa mratibu wa mipango yake duniani.

“Mungu hatatimiza hata inchi moja ya makusudi yake bila kwanza Rais John Magufuli kuelezwa na kuyaidhinisha makusudi hayo. Mungu anataka kuleta mabadiliko duniani kwa sababu ni mabadiliko ambayo yamekuwa katika ratiba yake ya kiunabii. Nani ambaye angepaswa kukabidhiwa jukumu hilo ni uchaguzi wa Mungu mwenyewe,” anasema.

Anasema kwa makusudi yake, Mungu amemchagua yeye ambaye ni Mwafrika na ambaye ni Mtanzania kusimamia mipango maalumu ya Mungu kwa dunia kama alivyomchagua Musa wa Israeli.

Kama watu wanaangalia sura yangu na mapungufu yangu; ni kwamba Mungu huwa hatizami sura wala kasoro ya mtu, bali huwa anaangalia moyo wa mteule wake.

“Kama ni mabadiliko ya Mungu, kuwezekana au kutowezekana ni kwamba yanawezekana kwa asilimia mia moja kwa sababu ndani ya siku 60 za kwanza za uongozi wako Rais Magofuli; mabadiliko mengi yametokea ndani ya taifa hili, chini ya utawala wako ukiwa mwanadamu.

“Je, Mungu atashindwa kukomesha vita ndani ya miaka minne iliyobaki na kuondoa njaa duniani ndani ya miaka 10? Ni kwamba Mungu hatashindwa. Basi naomba nafasi ya kukuona Rais wetu Mheshimiwa John Magufuli ili tuzungumze, ili kuzuia mabalaa zaidi kulikumba taifa letu, Amen,” anahitimisha Nabii Buberwa.

By Jamhuri