Unaweza kutumia miaka 20 kujenga haiba yako mbele ya jamii lakini sekunde tano tu zinatosha kukiharibu kile ulichokijenga kwa miaka 20.                                                                                 

Mtu mmoja alikuwa akisafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani kwenda Yeriko aliona kaburi moja limeandikwa: “Njia ya Mungu imepungukiwa watu wa kuipita.”

Inawezekana ni kweli, jambo la msingi ni sisi tulio hai kuipita njia ya Mungu bila kujali ni watu wangapi wanaipita ama wanakwepa kuipita.

Tuyahurumie maisha yetu yajayo kwa kuipita njia ya Mungu, tusikubali kuyaweka maisha yetu rehani kwa kukwepa kuipita njia ya Mungu.

Safari ya utakatifu inaanzia duniani, tuianze. Kama hatuwezi kuipita njia ya Mungu, ni dhahiri kwamba hatuwezi kuwa watakatifu. Njia ya Mungu ndiyo njia sahihi ya kuishi hapa duniani.

Njia ya Mungu ni njia ya kuishi maisha ya msamaha, njia ya Mungu ni njia ya kuwasaidia wasiojiweza. Njia ya Mungu ni njia ya kuishi maisha ya sala, njia ya Mungu ni njia salama na njia iliyojaa upendo, amani, furaha, unyenyekevu, undugu, umoja na mshikamano.

Katika makala hii tutapata fursa ya kutafakari umuhimu wa kuishi maisha ya upendo, unyenyekevu, huruma na namna ya kuepuka kuishi maisha ya majivuno, kiburi na hasira.

Sote tumewahi kuwaona watu wakikasirika, bila shaka na sisi wenyewe tumewahi kukasirika pia. Huenda tukasema kwamba hasira ni mbaya hivyo hatupaswi kukasirika, lakini mwingine anapotukosea huenda tukahisi tuna sababu nzuri ya kukasirika.            

Gazeti la JAMHURI, Toleo No. 346 lilichapisha makala yangu iliyokuwa inasema: ‘Maisha yasiongozwe na hasira.’

Msomaji mmoja alinitumia ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani unaosomeka: “Ndugu William, hasira imeyaumiza sana maisha yangu, sitaki mtu yeyote akutane na jehanamu hii niliyoipitia mimi, hasira imenitengenezea mazingira ya upweke.

Miaka 10 iliyopita mke wangu aliniacha, aliniacha kwa sababu nilikuwa nikimpiga sana. Aliniambia hivi: ‘Nakuacha si kwa sababu wewe si mwanamume, nakuacha kwa sababu hasira yako itaniua,’ akaniacha.

Miaka miwili baadaye nilioa tena mwanamke mwingine, huyu hakuweza kunivumilia hata kidogo, tuliachana baada ya kuishi miezi minne tu. Baada ya kuachana na mke wangu wa pili sijaoa tena.

Naogopa tena kuachwa kwa sababu ya hasira yangu. Ukweli ni kwamba hata kazini kwangu mahusiano yangu na wafanyakazi wenzangu si mazuri, hasira inanitesa sana.

Hadi sasa sina familia, sina marafiki wa kudumu, najaribu kujipendekeza kwa watu lakini bado wanaogopa kujenga urafiki na mimi. Nateseka sana.”

Hayo ndiyo maisha anayoishi mwenzetu. Kwa hakika anaishi maisha ya mateso, tayari hasira imemsababishia majeraha ya kimawazo na hisia za wasiwasi.

Tayari hasira imemsababishia maumivu ya roho na nafsi, anahangaika. Je, wewe pia ungependa uishi maisha ya namna hiyo? Usithubutu, ishi maisha rahisi. Yape maisha yako picha ya upendo, yape maisha yako picha ya msamaha, yape maisha yako picha ya huruma na unyenyekevu.

Imeandikwa: Msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi na wala msikae na hasira kutwa nzima (Efeso 4:26-27).

Hasira inatesa, hasira ni hasara katika maisha, hasira katika maisha ni donda ndugu, hasira inaumiza. Hasira inaua.

Sir Edmund Hilary, anasema: “Epuka hasira uwe na maendeleo.” Muonekano wa mtu mwenye hasira ni tofauti na muonekana wa mtu mnyenyekevu.

Maendeleo ya mtu mnyenyekevu ni tofauti na maendeleo ya mtu mwenye hasira. Roho nyenyekevu ina urembo mkubwa sana na Mungu hainyimi kitu chochote.

Hasira ni shetani, hekima ni Mungu. Kila kitu kimo ndani yetu. Hasira imo ndani yetu, hekima imo ndani yetu.

Atomu ni matofali ya ujenzi wa kila kitu ulimwenguni likiwemo jua na miili ya wanadamu. Ndani ya atomu kuna nguvu chanya na nguvu hasi. Miili yetu imetengenezwa na atomu na katika kila atomu kuna nguvu chanya na nguvu hasi.

Hivyo, tuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo mazuri na tuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo mabaya. Mtu akikutukana mwambie asante, akikupiga mwambie asante, akiendelea kukupiga, pigana.

Geuza hasira yako kuwa hekima kwa faida yako na kwa faida ya wengine.

By Jamhuri