Katika siku za karibuni imekuwapo mitafaruku kadhaa bungeni. Tumesikia habari za Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwa na mikwaruzano na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson. Nakumbuka Dk. Tulia alivyokuwa mbunge wa kwanza kuteuliwa katika vile viti 10 vya Rais. Nakumbuka nguvu kubwa ilivyotumika kutaka awe Spika wa Bunge, lakini kura hazikutosha.

Ni baada ya kuangushwa uspika ndipo akateuliwa kwa kasi wanayoiita ‘Vodafast’ kuwa Mbunge wa Kuteuliwa, kisha likawapo shinikizo awe Naibu Spika na akawa. Tunakumbuka Dk.Tulia alivyosimamia kesi ya mpigakura kukaa mita 200, kisha Mahakama katika hali ya mshangao ikatoa hukumu ya kitu ambacho hakikuwa sehemu ya maombi.

Serikali ilitaka wapigakura wakae mita 200 baada ya kupiga kura, lakini Mahakama kwa mshangao wa wengi ikatoa amri kuwa si mita 200 tu, bali anayemaliza kupiga kura aende nyumbani. Hapo ndipo umaarufu wa Dk. Tulia ulipoanza kusikika. Wengi walianza kusema huenda alitunukiwa zawadi baada ya kesi hiyo kwa kupewa fursa ya kuwa Naibu Spika.

Lakini katika kuthibitisha kuwa hana uzoefu, tumesikia alivyomwita Mbunge Bwege. Hata kama ni kweli Bwege ni jina halisi la mbunge huyo, na kama alitaka kufanya utani basi alipaswa kuazima busara ya Spika wake. Ndugai aliwahi kumuuliza mbunge huyo akisema: “Umesema unaitwa nani vile?” Yule mbunge akatamka mwenyewe “Bwegeeeee,” watu wakaishia kucheka na hakuna aliyenuna.

Leo tunashuhudia Dk. Tulia akiruhusu wabunge kumwaga matusi kwa wabunge wenzao ukumbini. Wanadiriki kusema wengine ni vichaa na majalada yao yako Mirembe. Mtu huyu anayemwita Tundu Lissu kichaa, kimsingi ubunge wake umeandikishwa kwa kalamu ya risasi, kwa maana kwamba hata wapigakura hawajajua kama ndiye mbunge wao.

Sitanii, hawa akina Tulia inawezekana wamedanganywa. Hawajipi hata fursa ya kulifahamu vyema Bunge. Sina uhakika miaka 20 iliyopita hawa wabunge walikuwa wapi. Kama ilikuwa wanafuatilia Bunge wangeweza kufahamu kuwa sasa wanaelekea kujimaliza. Wangefahamu aliyofanya aliyekuwa Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Eliakimu Simpassa!

Simpassa aliligeuza Bunge kama mali yake. Alitaka alichosema yeye tu ndiyo kiwe sahihi. Wananchi kadhaa aliwashurutisha kwenda bungeni kuhojiwa. Upinzani alitaka kuuminya kwenye chandarua kama mbu. Niliwahi kumwambia kuwa afanyayo yatamtenganisha na wapigakura, naye akaniambia hivi: “Bwana mdogo, huko jimboni kwangu wananipenda kama ubwabwa.”

Leo sina uhakika sana kama Simpassa anakumbukwa katika anga za siasa. Nachelea kusema Dk.Tulia anajichimbia kaburi la kisiasa. Anayoyafanya kutukana wabunge wenzake, kuruhusu matusi yakavurumishwa bungeni hadi wabunge wanawake wa Upinzani wakasusa Bunge, hayana afya kwa demokrasia ya nchi hii.

Sitanii, naomba nitumie fursa hii kumshauri Rais John Magufuli. Haya wanayofanya akina Dk. Tulia yana athari katika uongozi wako. Unaweza usiyaone leo, lakini yanapunguza kasi ya utendaji wako. Badala ya watu kushughulikia masuala ya msingi kama ukusanyaji kodi, kujenga mifumo ya uwajibikaji, kuondoa wafanyakazi hewa, Bunge linakutengenezea majipu.

Kwa muda wa mwezi sasa, Bunge limezua mjadala wa kurusha matangazo ‘live’ au la. Mjadala huu sidhani kama ulikuwa na faida yoyote kwa Taifa letu. Muda tunaoutumia kujadili umuhimu wa kurusha ‘live’ au la matangazo ya Bunge, ungetumiwa kwa mambo mengine. Anayofanya Dk. Tulia na kuzua mijadala isiyo na tija nachelea kusema matendo yake yanashabihiana na hujuma.

Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Hapa katikati kwa kupitia Dk. Tulia, naona Bunge limejipa kazi ya kuusimamia Upinzani. Nikisema ‘Bunge’ hapa nazungumzia kiti cha Spika. Nakubaliana na dhana iliyozungumzwa hivi karibuni kuwa si vyema sana hizi nafasi za Spika na Naibu wake kushikwa na mtu asiye na uzoefu wa masuala ya Bunge.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipata kusema kuwa mtu akikushauri jambo la kijinga na ukalifanyia kazi sawa na alivyokushauri anakuona ni mjinga. Sitaki kuamini kuwa Dk. Tulia anashauriwa, na kama ni kweli anashauriwa huenda anafanyia kazi ushauri huo bila kuupima.

Kwa kweli kwa nchi yetu ilipofika sasa, nadhani hatupaswi kurudishwa nyuma. Tulikwishapiga hatua katika eneo la utawala bora. Utawala wa sheria ni sehemu ya utawala bora. Kwamba wabunge na wananchi wanapaswa kufahamu sheria au kanuni zilizopo na kanuni au sheria hizo zikatumika kwa usawa bila ubaguzi.

Katika mabunge ya 9 na 10, Tanzania iliweza kuwa na Bunge linaloisimamia vyema Serikali. Kwa bahati mbaya naziona juhudi za makusudi zinazolenga kubomoa misingi iliyojengwa na mabunge mawili yaliyotangulia. Wapo pia wanaowaza kusema kwa mwenendo huu uliopo wa Bunge kutorushwa ‘live’, Naibu Spika kujipanga kushambulia wapinzani, huenda hili likawa Bunge lisilo na umaarufu kuliko mabunge yote yaliyotangulia.

Zipo taarifa kuwa Naibu Spika, Dk. Tulia, ameigeuza kazi ya Unaibu Spika kuwa kazi ya kudumu. Wakati Spika na Naibu Spika wanapaswa kuwa katika Ofisi za Bunge vinapokuwapo vikao, na kuwaacha Katibu wa Bunge na Sekretariati ya Bunge ndiyo wawe wanafanya kazi za siku hadi siku, inaelekea kwa Dk. Tulia hili ni kinyume.

Sitanii, yanayoendelea katika Bunge ni maandalizi tosha ya kuligeuza Bunge kuwa uwanja wa mapambano. Ndiyo, tunafahamu kuwa baada ya uchaguzi siasa huhamia bungeni. Ni matarajio yangu kuwa siasa hizi za bungeni zinapaswa kuwa za kujenga uchumi na si juhudi za kubomoana kisiasa. Kuruhusu siasa za vyama zikatawala bungeni kutalikosesha Taifa fursa ya aina yake.

Miaka mitano iliyopita nilipata kuandika. Nilisema Tanzania inahitaji Rais anayeweza kufanya uamuzi. Ni kwa bahati mbaya wakati wa kampeni kilichoendelea ni vijembe vya kisiasa juu ya uamuzi mgumu na uamuzi sahihi. Nikiri kuwa tumempata Rais anayeweza kufanya uamuzi mgumu na tumeshuhudia mara kadhaa akifanya hivyo kupitia sera ya majipu.

Kinachonipa shida; inaelekea baadhi ya watu kwa makusudi wanamshauri Rais afanye uamuzi wanaofahamu fika kuwa, ama unavunja sheria, au unamgombanisha na wananchi. Narudia na kusisitiza, kuwa uamuzi wa kutorusha ‘live’ matangazo ya Bunge, binafsi naona ilikuwa hujuma kwa Rais. Ni kwa mantiki hiyo ukija uamuzi mwingine kama huo unawafanya wananchi kutopendezwa na uongozi wa Rais Magufuli, kitu ambacho nisingependa kitokee katika muda mfupi wa yeye kuwa madarakani.

Leo tupo katika mkutano wa tatu wa Bunge la 11 Bunge. Napata tabu kama mwenendo ni huu hali itakuwaje kufika mkutano wa 17 au 20 mwaka 2020 tutaona zaidi ya Waitara kumsogelea mbunge mwenzake. Naamini ni vyema sasa ustaarabu utawale ndani ya Bunge. Wabunge wajue kuwa matusi si nguzo ya kuwaongezea ushindi katika uchaguzi ujao.

Wafahamu kuwa matusi hayatawaongezea shibe Watanzania. Imani yangu ni kuwa wabunge wote ndani ya CCM na upinzani wanapaswa kujielekeza katika kuwawezesha Watanzania kujikwamua kiuchumi. Leo tunalo tatizo la sukari. Inawezekana wenye viwanda hawakutoa taarifa sahihi serikalini. Unaweza kukuta waliidanganya Serikali kusema wanayo sukari ya kutosha wakati hawana.

Binafsi naamini kuwa Naibu Spika Tulia anapaswa kutulia kidogo akaendesha mjadala wa kuwezesha kupatikana sukari kwa uhakika. Mwishoni mwa wiki wakati naandika makala hii, nimepita katika duka moja hapa Kamanga, Mwanza. Muuza duka akasema alikuwa na kilo 20 za sukari, lakini imeuzwa ndani ya muda mfupi haijapata kutokea. Kufikia saa 2 asubuhi ziliishaisha na watu waliendelea kumiminika kutaka kuuziwa sukari.

Wakati nahitimisha makala hii, nimepata taarifa za Bunge kuruhusu matangazo ya Bunge ya ‘live’ kupitia TBC2. Nasema hii ni ishara njema katika kuelekea usikivu, lakini bado nasisitiza kuwa si vyema kuzifungia taarifa hizi kwenye TBC2 pekee. Waruhusiwe wote wenye uwezo wachukue matangazo hayo na kuyarusha moja kwa moja.

Sitanii, Bunge halina cha kuficha. Wakati nahamasisha matangazo ya Bunge kurushwa ‘live’, nashauri Rais Magufuli amtupie jicho Dk. Tulia amtulize kidogo. Mwenendo wake na kasi aliyonayo asiporudishwa kwenye msitari, atalipeleka Bunge la Tanzania tusikokupenda. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ingia moyoni mwa Dk. Tulia ajue kuwa ana wajibu wa kutumikia Taifa na si kupambana na Ukawa.

By Jamhuri