Sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala haya ilihoji kama kipo chama chochote cha wazee kushughulikia kilio chao, kuwasemea na wakasikika kama Umoja wa Vijana au Umoja wa Wanawake (UWT), au Umoja wa Wafanyakazi (TUCTA), au Umoja wa Wazazi (TAPA)? Mwandishi aliuliza, kwanini hali namna hiyo itokee kwa wazee? Mbona wapo wazee wasomi wengi tu wenye uwezo mkubwa wa kuongoza? Endelea.

Hapa natoa historia ya vyama vya wazee katika nchi hii. Kwanza kabisa ni kile chama cha TAA (Tanganyika African Association) kilichobuniwa na wazee wa Tanganyika tangu mwaka 1929. Hiki ndicho kilichokuja kugeuzwa mwaka 1954 na kuwa TANU (Tanganyika African National Union).

 

Kilianzishwa na wazee wa nchi hii kama historia inavyoonesha.

 

Baada ya Uhuru hapakuwahi kubuniwa chama chochote cha wazee maana ilionekana hakihitajiki. Polepole wazee walipokuwa wanang’atuka makazini, likajitokeza wazo, je, nini kifanyike ili wazee watambulike? Hapo ndipo mwanzo wa kuonekana ipo haja ya kuwa na chama cha wazee katika nchi. Tumeanzaje kuunda chombo namna hii?

 

Mwaka 1989 kilitokea chama cha kimataifa kule Uingereza kinachoitwa HELPAGE INTERNATIONAL (HAI) kilialikwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwenda kusaidia wazee wa huko. Mwaka 1990 HelpAge International ilifungua ofisi zake Unguja. HAI ilionesha kuna haja ya kupata chombo cha wazee kitaifa. Ndipo mwishoni mwa Oktoba 1992 waliendesha warsha ya kitaifa katika Hoteli ya Karibu, maeneo ya Oysterbay, Barabara ya Haile Selassie karibu na Morogoro Store jijini Dar es Salaam.

 

Mapendekezo ya warsha ile yaliunda chama cha wazee cha kitaifa na walikiita Saidia Wazee Tanzania (SAWATA). Ikateuliwa kamati ya uongozi wa muda ya chama hicho cha wazee kwa dhamira ya kuandaa Katiba ya chama na hatimaye kukiandikisha serikalini kama NGO (Non – Governmental Organisation) chenye mtazamo wa chama cha kitaifa cha wazee wa nchi hii ya Tanzania.

 

SAWATA iliandikishwa rasmi serikalini kwa Msajili wa vyama hapa nchini Machi 21, 1994 na kupata hati ya Usajili Na. S 8039. Kuanzia hapo HelpAge International wakawa bega kwa bega na SAWATA katika mambo ya wazee. Mwaka 1994 HelpAge International walihamia Dar es Salaam, wakiwa bado katika harakati za kuwashughulikia wazee wa nchi hii wakifanya warsha elimishi juu ya uzee na kuzeeka.

 

HAI na SAWATA walitumia ofisi moja waliyopanga katika jengo la Umoja wa Vijana, ghorofa ya I vyumba Na. 85 na 87. Pango la nyumba likalipwa na HAI katika mpango wake wa maendeleo. Waliafiki kukiimarisha chama kile cha wazee na walitamka hivi, nanukuu; “…One of our highest priorities has been and remains that of fostering the growth and development of a National Age – Care Organisation known as Saidia Wazee Tanzania (HAI TANZANIA PROGRAMME REVIEW 1991 – 1996 uk. 11).

 

Miaka ile ya mwanzo mwanzo HAI ilijitolea sana kuimarisha chama cha wazee. Walikitafutia miradi, walikipa nyenzo na walisaidia kupata uongozi wa kitaifa. Walikipatia mradi wa basi dogo la kufanya daladala, waliwapa gari dogo aina pick up kwa shughuli za utawala na walisaidia kuunda bendi ya wanamuziki ya wakongwe iliyoitwa Wazee Jazz kama mradi wa kuwapatia fedha (income generating projects).

 

Bendi ile ilipelekwa mpaka Uingereza katika kuitambulisha kama kitegauchumi cha wazee wa SAWATA. Huo kweli ulikuwa mwanzo wa kuwajengea wazee (chombo cha kutoa sauti ya wazee katika Taifa hili).

 

SAWATA ikaanza kuenea katika nchi yetu. Tawi kubwa lilifunguliwa kule Karagwe wakati ule wa matatizo ya Rwanda. Wakimbizi wengi waliingia Karagwe, na walihitaji NGO ya kuwahudumia. SAWATA ikajitokeza kwa nguvu chini ya HAI na kufungua tawi la kuwahudumia wakimbizi wale wa Rwanda.

 

Huu ulikuwa mradi mkubwa sana kwa HAI na SAWATA na uliwaingizia fedha za kuridhisha. Matawi kadhaa yalifunguliwa katika nchi nzima. Kukawa na matawi Bukoba, Kasulu, Musoma, Dodoma, Iringa, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tabora, Shinyanga na kwengineyo.

 

HelpAge International ikaona maendeleo ya kuridhisha, basi HAI wakapenda kukabidhi uongozi wa uendeshaji shughuli zote za SAWATA kwa wazee wananchi. Loo! balaa lilianza hapo.

 

Licha ya kuwa na miradi kadhaa ya uzalishaji mali kama vile basi la daladala, wazee Jazz Band na wakimbizi wa Rwanda, uongozi wa wazee wananchi ukakomba fedha zoote fyuuu! HAI ilipotaka kuona hesabu za SAWATA (Audited Accounts) wazee wale hawakuwa na cha kueleza. Mamilioni ya fedha za SAWATA yaliliwa na wazee ‘wajanja’ wale. Hapo HAI wakagutuka. Kumbe Waafrika ndivyo walivyo!

 

Waliamua kuisusa SAWATA wakawaachia ile ofisi pale Jengo la Umoja wa Vijana na madeni kibao! HAI wakatafuta ofisi zao mpya kule Regent Estate ambako mpaka leo wapo.

Bila kuongeza chumvi au kama anavyosema ndugu yangu Deodatus Balile katika zile makala zake “SITANII” katika Gazeti la JAMHURI, nasema hivi HelpAge International walidhamiria sana kuwaundia wazee wa Tanzania chama cha wazee ili kiwe ndiyo sauti yao, lakini jamani sisi wazee wa Tanzania hatubebeki!

 

Pamoja na kutafuna mamilioni ya fedha za SAWATA na kushindwa kabisa kujiendesha, Wizara ya Ustawi wa Jamii wakiungwa mkono wa HAI hao hao walijitahidi kutuweka sawa mara kadhaa bila mafanikio.

 

HAI ilitukusanya wazee katika warsha mbalimbali tuunde chombo cha kutetea wazee. Mwaka 1999, mwaka wa wazee kitaifa duniani HAI walishirikiana na wizara kutuwezesha kusherehea kitaifa Siku ya Wazee Duniani ambayo ni Oktoba mosi. Wakakusanya wazee kutoka vyama kadhaa vya wazee; British Legion, SAWATA matawi mbalimbali humu nchini, GOIG, Good Samaritan, Social Concern, Women Group na kadhalika, tukajaribu kusherehekea Siku ya Wazee kitaifa hapa nchini. Mgeni rasmi alikuwa Mzee Rashidi Kawawa pale Karimjee Hall, Dar es Salaam.

 

HAI ilitukutanisha tena katika vikao mbalimbali wakati wa kuandaa Sera ya Wazee nchini. Wizara ya Ustawi wa Jamii kwa bidii kubwa sana wakiwezeshwa na hiyo HAI, hatimaye Sera ikapatikana. Septemba 21, 2003 katika Ukumbi wa Karimjee, Mheshimiwa Mudhihir Mudhihir, Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Jamii, aliizindua Sera ya Wazee na mimi nilibahatika kuwa Mwenyekiti wa kikao kile kilichoandaliwa rasmi na Wizara ikishirikiana na HelpAge International kuzindua hiyo Sera ya Wazee.

 

Bado wazee hatukuweza kuona umuhimu wa kupata sauti ya wazee katika nchi yetu! Tuna vyama vya wazee zaidi ya 40 katika nchi hii. Ni utitiri wa vyama vya wazee. Kila kimoja kinaona kina haki ya kutetea kikundi cha wazee wake chenyewe.

 

Nitajaribu kuvitaja baadhi ya vyama vyenyewe. Kuna SAWATA iliyobuniwa na HelpAge International. Ina matawi nchi nzima – Karagwe, Bukoba, Rukwa, Temeke, Ilala, Kinondoni, Dodoma, Kigoma, Kasulu, Mara, Tabora. Lakini haina makao makuu! Kila tawi ni asasi inayojitegemea. Sijui hata namna ya kulieleza hili. Kuna MORETEA wazee wa Morogoro, TEWOREC wazee wa Tanga, SHISO wazee wa Iringa, wastaafu wa Mtwara, IRAHOPEGA – wazee wa Kiomboi-Iramba, SOPF wazee wa Songea, chama cha wastaafu wa Arusha, chama cha wastaafu wa Lindi, Good Samaritan, Social Service Kinondoni, Social Concern Agency, wazee wa Dar es Salaam, PUT vigogo wastaafu Nyerere Foundation Dar es Salaam, PADI – wazee wa Songea, TALFAE wazee wa Shinyanga, GOIG, wazee akina mama wa Mbezi Kinondoni, MAPERECE wazee wa Magu, Wazee ni Hekima Mwanga, WAAP Kibaha, na vingine nimevisahau.

 

Sote sisi shabaha yetu ni moja ile ile ya kuwatetea wazee. Lakini tumeshindwa kuwa na mfumo unaoeleweka na uongozi mmoja wa kutetea wazee wa nchi hii.

 

Itaendelea

1134 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!