lipumbaNdugu Rais kuna kiongozi mmoja alitamka bungeni kuwa Burundi isiitishe Tanzania, la sivyo tutapeleka jeshi kuiangamiza yote.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliitembelea Burundi. Huko aliulizwa na mwananchi mmoja kwanini Tanzania ilitaka kuivamia Burundi. Maneno hayo yalitamkwa na kiongozi wa juu wa serikali ya Tanzania tena akiwa bungeni.

Katika kumjibu, Mwalimu Nyerere alisema: “Usidhani kuwa viongozi wapumbavu wako hapa Burundi peke yake; hata kwetu Tanzania viongozi wapumbavu wapo!”

Tukiwa tunatafakari kauli hiyo ya Baba wa Taifa kuwa hata hapa kwetu viongozi wapumbavu wapo tuunganishe na kauli ya Spika wa Bunge aliyesema, “Nini ulevi wa Kitwanga! Mnamshangaa Kitwanga? Wako wabunge wanakunywa na kujidunga madawa (dawa) ya kulevya! Wako wabunge wanavuta bangi! Wako wabunge wanaokunywa viroba na hasa wakati wa kipindi cha mchana wanakuja bungeni wakiwa wamelewa!”

Wakati hayo yakijiri, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba anasema anatengua mwenyewe barua aliyoiandika ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho na sasa anarejea katika nafasi yake.

Wakati wa Azimio la Arusha nchi hii ilikuwa na Tume ya Bei.

Viongozi wetu wakaivunja na sasa kuna vitu kama EWURA ambavyo si tume, si nini, lakini kazi yake ni ile ile ya Tume ya Bei waliyoivunja!

Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alijenga viwanda vingi na vingine vilivyokuwa si vya serikali akavitaifisha.

Alipokuja Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa akaviuza na vingine akavibinafsisha bila mpangilio wowote. Wakati tukiandika maandiko haya Bunge la Jamhuri lilikuwa linajadili bajeti ya nchi chini ya Uenyekiti wa Naibu Spika asiyependwa na wengi waliomsusa.

Kweli jengo la Bunge lilikuwapo na viti na vitu vingine; lakini wabunge wenyewe walikuwa 85 tu. Na kati ya hao wabunge 85 hatujui walevi walikuwa wangapi. 

Wananchi wakiyaunganisha haya yote na mengine, wana haki ya kujiuliza nchi hii ina viongozi wa aina gani?

Katika hali kama hii akitokea mbunge akasema wao wasikatwe kodi ya asilimia tano katika mamia ya mamilioni ya shilingi ya kiinua mgongo chao, bali iongezwe shilingi 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli potelea mbali kama kwa kufanya hivyo kutawaongezea ugumu wa maisha Watanzania masikini, wananchi wamweke katika kundi gani?

Halafu akatokea mbunge akataka mnara wa askari uvunjwe na badala ya kusema angalau basi iwekwe sanamu ya shemeji yetu kama ana mke ili watu wamjue kuwa hatawaliwi na mfumo dume anatoa wazo mfilisi kabisa, wananchi wamweke kundi gani?

Ndugu Rais wasaidie watu wako. Viongozi aina hii wananchi wawaweke kundi gani? Kati ya viongozi wapumbavu ambao Mwalimu Nyerere alisema wapo au kati ya wabunge walevi aliosema Spika Job Ndugai? Wajinga ni sisi na ndiyo tuliwao. Tunaendelea kuita mbwa, ng’ombe! Na wajinga zaidi watawapigia mpaka saluti. Hawa ndiyo viongozi wetu wa mwendokasi!

Kama Ibrahim Lipumba anatumika, basi anayemtumia hamjui Lipumba. Mkapa akiwa Rais aliuliza, “Ni maprofesa gani hawa?” Akajijibu mwenyewe, “Hawa ni maprofesa uchwara!” Umeongoza chama mihula minne mafanikio yako wabunge wawili tu Bara. CUF ndani ya UKAWA kilichokutoa uchaguzi mmoja tu wabunge zaidi ya 10. Na kwa mara ya kwanza inaongoza halmashauri sita. Mafanikio ambayo bila UKAWA, CUF isingeyapata.

Ndugu Rais ni uamuzi wa UKAWA kukataa kumteua kuwa mgombea urais ndiyo uliomfanya aseme anasutwa na nafsi yake na kuamua kuususa na uenyekiti wenyewe wa CUF. Kilichomfanya aondoke siyo kuteuliwa ndugu Edward Ngoyayi Lowassa kuwa mgombea urais kupitia UKAWA la hasha! Hata kama angeteuliwa Seif Sharif Hamad kuwa mgombea urais wa Tanzania bado angesema nafsi yake ingemsuta na angeondoka!

UKAWA bado upo na uamuzi ule ule, kilichobadilika nini? Wanawema wote ambao wanadhani upinzani ukiwa na nguvu utasaidia kuimarika kwa demokrasia katika nchi yetu wasiichae CUF peke yake kumkabili Ibrahimu Lipumba. Mwanamwema mmoja akaniambia Mwalimu Mkuu, huyu sasa ni sawa na bomu la kujitoa mhanga ambalo CCM imejifunga kiunoni kuukabili upinzani.

Ndugu Rais Benjamin William Mkapa; Rais wa Awamu ya Tatu akiwa mgeni rasmi wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere kwenye Tamasha la Nane alisema anajutia kukosa kuweka mpangilio katika kubinafsisha na kuuza kampuni na viwanda vya nchi hii.

Alipowaomba Watanzania wamsamehe, bila kuchelewa Jenerali Ulimwengu akamkandamiza akasema anawashangaa viongozi wetu kupata busara baada ya kustaafu. Kuomba kuna kukubaliwa na kuna kukataliwa. Sasa Mkapa awaambie Watanzania, kama hawataki kumsamehe wamfanye nini ili yaishe?

Sasa baba na wewe bwana! Unasema Tanzania ya Magufuli itakuwa ni ya viwanda, ah! Binti yangu angekuwa na uwezo wa kukufikia nina hakika kwa hili angekuambia, “Ah, Baba!” Nikisema uongo binti yangu haniambii baba umesema uongo, anasema, ah, baba! Lakini akiniambia ah, baba ujumbe unafika kwangu kuwa amegundua kuwa nimesema uongo.

Ndugu Rais kila nikiifikiria CCM bila Abdulrahman Kinana sipati jawabu. Nilipokuona kanisani kwa Mchungaji Anton Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ ukanikumbusha kuwa huyu ndiye kiongozi wa kidini aliyekuwa jasiri kuikemea roho ya kishetani iliyoletwa na wana wa ibilisi kupandikiza chuki kati ya watu wa Mungu. Mchungaji Anton Lusekelo alitamka hadharani kama mtu aliyejawa na upako akasema: “Aliyeleta wazo la vua gamba hakufikiri sawa sawa!” Aliyeshabikia chuki kati ya watu wa Mungu, na ayaonje mateso ya ulimwengu huu wa Muumba wetu

katika siku zake za mwisho! Kinana kama nabii aliyetumwa na Mungu ndiye aliyekuja kuinusuru nchi hii isiingie katika machafuko. Akaukomesha ujinga huo!  Baba mimi ni nani hata nikuchagulie watendaji? Sijaja hapa kumtafutia mtu kazi. Nimekuja hapa kuwatafutia hawa masikini wa Mungu kiongozi ambaye yuko tayari kuwasikiliza. Kama

Kinana angepata Mwenyekiti wa kufanana naye, leo Watanzania wangeishi katika umoja, upendo na udugu ule ule walioishi wakati wa Baba wa Taifa bila ujinga wa utukufu wala huu upumbavu wa uheshimiwa!

1258 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!