Ndugu Rais, imenilazimu niisemee kidogo makala yangu ya wiki iliyopita iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Kipi kianze’. 

Imenilazimu kufanya hivi kutokana na ukweli kwamba kuna baadhi ya wasomaji hata kama ni wachache, au hawakuupata ujumbe uliokusudiwa au kwa makusudi wanaonekana wazito kuelewa.

 Jingine ninalotaka lieleweke ni kwamba ndugu Rais, kwa wewe kuwa Rais wa nchi yetu, umekuwa ndiyo baba wa sisi wote. Naliandika hili kwa sababu kuna baadhi ya wenzetu wanadhani wewe ni Rais wao peke yao au ni Rais wao zaidi. 

Pia natambua wako wengine wanaosema, ‘Ah! Wa nini?’ Wewe ni Rais wa sisi wote. Na kwa maana hiyo wewe ni baba wa sisi wote!

Kuna mwanamwema mmoja aliniandikia ujumbe ambao naona ni vema na wasomaji wetu wengine wakausoma. Aliandika hivi, “Ugumu wa kazi ya urais ni wa kweli kama Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alivyosema…..ni mzigo! Akishangaa watu wanaokimbilia Ikulu…. Watu kama nyie mnaochanganya mambo ndo mnasababisha ugumu wa kazi ya Rais. 

Hoja ya upungufu wa pensheni inapaswa kufuata njia yake na ununuzi wa ndege kadhalika. Hatujasikia kama hela za MSD na pensheni zimechukuliwa kununulia ndege.

Mwambie mbunge wako akumbushe bungeni tuboreshewe pensheni zetu”. Ndugu Rais huu ni mfano mzuri wa mtu kusoma maandiko ya wengine au kwa harakaharaka au juu juu, na kisha ukatoka mweupe bila kujua kilichoongelewa.

Anasema, “Mwambie mbunge wako akumbushe bungeni tuboreshewe pensheni zetu”. Hakuna palipoandikwa kuwa pensheni haitoshi pamoja na kwamba pensheni haitoshi. Yaonekana huyu ndugu haelewi kuwa Bunge akiwamo mbunge wangu na Rais wangu wakati ule akiwa waziri limeishafanya kazi yake. 

Bunge liliagiza kima cha chini cha pensheni kiongezwe kutoka shilingi 50,000 kwa mwezi kuwa shilingi 100,000 kwa mwezi. Kilichoongelewa katika maandiko yale ni nyongeza ya shilingi 50,000 iliyoidhinishwa na Bunge ambayo wastaafu wa TTCL peke yao ndiyo bado hawajaongezewa. Je, si haki ya wastaafu wa TTCL kumlilia Rais kama baba yao awaulize viongozi wa TTCL kwa nini hawajatekeleza uamuzi wa Bunge hadi leo?

Na huyu si kwamba anampenda saana Rais wetu, la hasha! Ni uelewa mdogo tu! Wasimpomlilia baba yao, wamlilie nani katika nchi hii? Ndugu Rais, wahurumie watu wako, wazee wastaafu wa TTCL! Mwaka sasa wanangojea nyongeza ya sh. 50,000 na haijulikani wataongezewa lini!

Huyu ndugu anasema, “Hatujasikia kama hela za bohari ya dawa (MSD) na pensheni zimechukuliwa kununulia ndege.” Kwa uelewa wake, lolote ambalo yeye hajasikia basi halikutendeka. Hata hivyo hakuna mahali katika yale maandiko palipoandikwa kuwa fedha za MSD na pensheni zimechukuliwa na kununulia ndege. Badala yake tulikushukuru ndugu Rais kwa kununua ndege mbili.

Ndugu Rais, labda kilichomchanganya ni ule ushauri uliotolewa kwako kuwa kabla ya kununua ndege nyingine kubwa zaidi na ghali zaidi, angalia kwanza afya ya wananchi wako. MSD imesema hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa nchini ni asilimia 53 tu! Na kwamba kati ya aina 135 za dawa muhimu zinazohitajika, ghalani, zipo aina 71 tu ya dawa hizo.

Hali hii si hali ya kusimama hadharani na kutamba kuwa fedha za kununulia hiyo ‘midege’ tunayo. Kwamba tuna fedha nyingi kiasi cha kuwapiga ‘tanchi’ matajiri wa dunia waliokuwa wamekwisha tia ‘oda’. Hakuna anayeweza kutusifia kwa tambo hizo wakati tunao upungufu wa dawa muhimu hospitalini.

Ndugu Rais, wananchi bado wana machungu wakikumbuka wakati ule MSD walipositisha utoaji dawa katika hospitali za Serikali. Masikini wengi walipoteza maisha yao hata kwa magonjwa ambayo wangepona kama wangepatiwa dawa kama zingekuwapo. Fedha zilizokuwapo ila, zilielekezwa kwa safari za nje, ambazo tija yake kwa wananchi bado inaacha maswali.

Makala ilitoa angalizo kwako ndugu Rais kuwa pamoja na kwamba kuongeza ‘midege’ mikubwa miwili ni jambo jema sana, lakini kuzingatia kwanza afya za wananchi na hasa masikini na wanyonge ni muhimu na busara zaidi. Ikumbukwe kuwa hiyo ‘midege’ watapanda wenye pesa zao. Masikini wa nchi hii ambao ndiyo wengi wataishia kusikia miungurumo yake itakapokuwa inaruka juu ya vichwa vyao.

Ndugu Rais, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inaidai Serikali Sh. bilioni 142 ikiwa ni gharama za dawa na vitendanishi vilivyosambazwa. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Sako Mwakalobo, anasema hadi sasa Serikali imeishalipa Sh. bilioni 10 na deni halisi limebaki ni Sh. bilioni 142.

Katika hali kama hii haiwezi kuwa ni busara kutamba kuwa tuna fedha nyingi huku tukizitumia fedha hizo kununulia midege na kuwaacha masikini wetu wakipukutika kwa kukosa dawa katika hospitali zetu!

Ndugu Rais, tunapoyasema haya ndugu yetu anasema, “Watu kama nyie mnaochanganya mambo ndo mnaosababisha ugumu wa kazi ya Rais.” 

Kazi ya urais kama ilivyo kwa kazi nyingine, haiwezi kuwa ngumu kwa yeyote anayetosha! Ni mzigo kwa maana ya kuwa, ni jukumu. Hata ukipewa sindano kuipeleka mahali ni mzigo. Mzigo na uzito ni vitu viwili tofauti! Ni busara ndugu Rais ukawachukulia kwa tahadhari waganga njaa hawa!

1102 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!