Ndugu Rais, mtu akikutana na mtu anayedhani amelewa, amwambie umelewa.

Kama hajalewa atampuuza tu. Ole wake kama atakuwa kweli amelewa.

Atayaoga matusi yake. Ataanza na tusi halafu atamuuliza umenilewesha wewe? Hakijaeleweka bado Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amekutana na nani.

Baba, ili kuonekana kama simlengi mtu nanukuu maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu, miaka 14 iliyopita.

Inapotokea yakawa vilevile na yanatokea sasa hapo ndipo utukufu wa Mwenyezi Mungu unapojidhihirisha kwa maana amewajalia baadhi ya waja wake karama zake. Jina lake lihimidiwe.

Baba, nitaendelea kuililia nchi yangu; kuwalilia maskini wenzangu wa nchi hii; na kukulilia Rais wangu huku nikijililia na mimi mwenyewe mpaka hapo pumzi yangu ya mwisho itakapoutoka mwili wangu. Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu ukurasa wa 14, imeandikwa, “Mwalimu Mkuu wa Watu alikuwa nyumbani kwake akiendelea kuuguza majeraha yake aliyoyapata akiwa mikononi mwa polisi. Majeraha yalijaa karibu mwili mzima. Alikuwa amefungwa bandeji kubwa kichwani. POP ilifungwa katika kiwiko chake cha mkono wa kulia na kwenye goti la mguu wa kushoto.

Jicho lake la kulia lilikuwa limevimba. Lilitoa machozi mfululizo.

Alitembea kwa msaada wa magongo. Alizungumza kwa matatizo kutokana na kupoteza meno kadhaa mdomoni mwake na kubakiwa na machache tu, mengi yakiwa magutu na papachi. Alikuwa akikohoa damu na kula kwa shida.

Mavune yake yalikuwa makali sana…Bwana mageuzi alimtania paroko Ivo, ‘Baba Paroko ulipotezaje sikio lako wakati wa mahojiano na polisi?’

“Kabla Paroko hajajibu Mwalimu Mkuu alijibu, ‘Kupoteza sikio peke yake ni bahati yake. Vyombo vya dola au usalama wa serikali (Taifa) wamefikia mahali kuua raia wema kama nguruwe. Wengine wamepoteza uhai wao kwa utajiri wao, wengine kwa umaskini wao, na wengine kwa kusema ukweli wao. Wangapi wamefia ndani ya chumba cha mahojiano? Wangapi wameuawa katika misitu yetu?’

“Bwana mageuzi alimuuliza Mwalimu Mkuu nini kifuate baada ya maandamano ya amani kushindwa. Naye alimjibu, ‘Kiwanda kuondoka lazima kiondoke hata kama itatakiwa sadaka kubwa zaidi. Ama kinaondoka kiwanda, ama tunaondoka sisi.’

“Walipojaribu kuona uwezekano wa kulitumia Bunge, Bwana Mageuzi alikuja juu na kusema, ‘Mwalimu Mkuu, Bunge la sasa siyo Bunge kwa maana halisi ya Bunge. Bunge la sasa ni sawasawa na mchezo wa kuigiza.

Utadhani ni watoto wanaocheza kombolela. Linafanya kazi kama kamati ya chama tawala. Bunge limegeuzwa sehemu ya mijadala ya mizaha na kuwa mhuri wa mizaha hiyo kwa faida ya viongozi. Limekuwa chombo cha kuvunja katiba ya nchi kwa kupitisha sheria kandamizi kwa ajili ya kuwanufaisha watawala…serikali inaundwa na watu ili iwatumikie kwa namna wanavyotaka. Kwa kuwa Bunge ndio uwakilishi wa watu hao, basi kwa maana hiyo Bunge liko juu ya Serikali kwa mantiki ya demokrasia na uwakilishi.

“Spika wa Bunge kuwa mwanachama wa chama cha siasa imekuwa ni sababu tosha ya mijadala ya kisiasa na uchama bungeni. Baadhi ya wabunge wachovu wameligeuza Bunge kuwa jukwaa la kusisitiza jinsi walivyo waaminifu kwa serikali na kwa rais. Wanapumbazwa na tamaa ya kuchaguliwa kuwa mawaziri au kuwekwa katika sehemu zenye maslahi zaidi. Wanasahau majukumu yao ya kulinda demokrasia na haki za

wananchi. Wanaodhani chama chao kitatawala mpaka Yesu atakaporudi hawajasoma historia. Wabunge wa namna hii hawawezi kuidhibiti serikali wala kumwambia mfalme kuwa yuko mtupu.

“Baadhi ya mawaziri wamechoka kiakili na hivyo hupata taabu ya kufikiri kile wanachotaka kukisema hadharani. Baadhi yao hutoa majibu mepesi kwa maswali mazito wanayoulizwa. Majibu yasiyokidhi mahitaji ya nchi, lakini yenye nguvu ya kuwachanganya wananchi. Katika utawala bora hawa wangewajibishwa.”

Paroko alimwambia Mwalimu Mkuu, “Ubunge sasa ni biashara kama zilivyo biashara nyingine. Wabunge sasa ni watu wa mshahara. Hakuna mchungaji wa kondoo pale. Siku moja tutakuja kusikia spika mwenyewe amekuwa mwenyekiti wa bodi wa haya makampuni ambayo zamani tuliyaita ya kibepari. Wanatenda dhambi ya mauti. Hawataikwepa hukumu. Siku ya kusimama mbele ya haki itakapofika, hawataiona huruma ya Mungu, na wala mwanga wa milele hautawaangazia. Bwana awasamehe wabunge hawa kwa maana hawajui watendayo…wabunge wanapodai maslahi zaidi, spika wa Bunge huwa wa kwanza kuunga mkono kwa kuwa naye ni mbunge. Kwa vile maslahi ya Bunge hutolewa na Serikali, basi Spika naye hujidhalilisha mbele ya Serikali na hivyo kuufanya mhimili huu wa Bunge kukosa mwelekeo.

“Hapa Mwalimu Mkuu utaona kuwa ukuu wa Bunge na uhuru wa Bunge

vimepotea. Bunge limepoteza heshima yake. Wabunge waadilifu wanapohoji mwenendo wa Serikali huhukumiwa na mahakama ya Kamati ya Bunge ya Maadili na kanuni za Bunge. Katika hali kama hii itasaidia nini suala hili kulipeleka bungeni?” Mwisho wa kunukuu.

Baba, nimelazimika kunukuu maneno haya ya zamani katika kitabu hicho ili isije kuonekana kama nimemlenga mtu. Wananchi wapime haya yaliyoandikwa miaka 14 iliyopita na hali ya Bunge letu sasa ili wapate kujua kama kuna mtu amelewa.

Mwanamwema kutoka mbali aliniandikia, “Mwalimu Mkuu maandiko yako yakijakusomwa na kizazi kijacho, watagundua kuwa wale uliokuwa unaishi nao hawakujua kama walikuwa na nabii.’’

Katiba, Ibara  ya 143 (6) inasema, katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3), na (4) ya ibara hii, CAG hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali lakini… hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama…ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa katiba hii au sivyo.

Wakati amri ya kufungwa pingu mtumishi wa Mungu CAG, mwanamwema Mussa Assad ikitolewa waliokuwa wanamsikiliza walizivuta kumbukumbu za kampeni za mwaka 2015 ambako mgombea alikuwa amempiga mshindani wake rungu la kichwa lililomwangusha chini kifudifudi na kumfanya azimie!

Kama lengo ni kuwatumikia wananchi kamwe hakuwezi kutafutwa kwa unyama kiasi hiki. Wananchi wapime nani amelewa. Hawa ndiyo baadhi ya viongozi wetu!

1000 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!